Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania kupitia Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imetupilia mbali maombi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ya kutaka kutenguliwa kwa amri ya Mahakama iliyotolewa Juni 10, 2025, ikikizuia chama hicho kutumia rasilimali zake kwa shughuli za kisiasa.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Hamidu Mwanga amesema amri hiyo inabakia kama ilivyo hadi kesi ya msingi ya kikatiba, inayohusiana na mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali ndani ya chama hicho itakapoanza kusikilizwa Agosti 28, 2025.
Kesi ya madai namba 8323/2025, ilifunguliwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Zanzibar), Said Issa Mohamed, kwa kushirikiana na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Walalamikiwa katika kesi hiyo ni Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa wa Chadema pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Katika hatua ya awali ya kesi hiyo, Mahakama ilitoa amri mbili; kwanza, kuizuia Bodi ya Wadhamini kufanya shughuli za kisiasa na pili, kumzuia Katibu Mkuu pamoja na wafuasi wa Chadema kutumia mali za chama kwa shughuli za kisiasa.

Wakili wa Chadema, Hekima Mwasipu amesema walifungua maombi ya kutaka amri hiyo itenguliwe kwa misingi ya kutopata haki ya kusikilizwa na pia mabadiliko ya hali ya utekelezaji wa amri hiyo, ambayo yamesababisha usumbufu kwa chama, ikiwa ni pamoja na kutokuwa na ufahamu wa mahali zilipo baadhi ya rasilimali za chama.
“Lakini Mahakama imeamua kuendelea na msimamo wake wa awali. Tumeambiwa kesi ya msingi itaanza kusikilizwa Agosti 28, 2025, saa 4:00 asubuhi,” amesema Mwasipu.
Katika uamuzi wake, Jaji Mwanga ameeleza kuwa hoja za Chadema hazikutosha kuifanya Mahakama ibadili amri yake.

Kuhusu madai ya upande huo kuwa hawakupata nafasi ya kusikilizwa, Mahakama imeeleza kuwa Chadema waliarifiwa kuhusu shauri hilo na Wakili Jebra Kambole alihudhuria na alieleza sababu za kutokuwepo kwa wanasheria wenzake.
“Mahakama iliendelea na usikilizwaji kwa sababu Wakili Jebra Kambole alikuwapo,” amesema Jaji Mwanga.
Kwa sasa, amri ya kuzuia matumizi ya rasilimali za Chadema kwa shughuli za kisiasa bado ipo palepale hadi kesi ya msingi itakapoamuliwa.