Tanzania kuwa kinara ajenda ya wanawake, amani na usalama

Dar es Salaam. Wadau wa amani na usalama nchini wameshiriki kwa pamoja mdahalo wa kujadili mpango kazi wa kitaifa wa kutekeleza ajenda ya wanawake, amani na usalama 2025-2029 unaotarajiwa kuzinduliwa kesho Agosti 19, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Dk Doto Biteko.

Siku moja kabla ya uzinduzi huo wadau mbalimbali wameshiriki katika mdahalo uliolenga kujadili mada ya namna ya kuifanya Tanzania kuwa kinara wa kikanda katika kukuza na kuendeleza ajenda ya wanawake, amani na usalama,.

Mdahalo huo uliofanyika leo Agosti 18, 2025 kwenye Chuo cha Ulinzi na Amani Tanzania, umeongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalumu, Dk John Jingu.

Akizungumza katika mdahalo huo, Dk Jingu amegusia mada kuu akibainisha namna ambavyo Tanzania inahitaji mwendelezo wa kuwa kinara wa kikanda katika kukuza ajenda ya wanawake , amani na usalama.

“Sisi kama wadau tunapaswa kujadili ni namna gani tutaendelea kuifanya Tanzania kuwa kinara wa ajenda hii,” amesema Dk Jingu.

Akielezea chimbuko la mpango kazi huo, Dk Jingu amesema miaka 25 iliyopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana na kuja na azimio 1325 ambalo lilieleza namna kunapotokea changamoto na migogoro ya kiusalama wanawake na watoto hasa wa kike wanavyokuwa waathirika wakubwa.

“Kwenye migogoro kama hiyo changamoto wanazozipata wanawake na wasichana ni tofauti na waume, kundi hilo linaathirika zaidi. Hivyo Baraza la Usalama wakataka dunia na mataifa yote kuutambua ukweli huo na kuuzingatia, pia wakataka kila taifa liwe na mpango kazi wa kutekeleza ajenda ya wanawake, amani na usalama 2025-2029,” amesema.

“Kuzinduliwa kwa mpango kazi huu hakumaanishi kwamba hatuzingatii masuala ya  jinsia kwenye masuala ya ulinzi na usalama, nchi yetu ina historia kubwa katika hilo kikanda na kimataifa.

“Ingawa tunapokuwa na mpango huu tunakwenda sambamba na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa hapa kwetu tunapozungumzia usalama tunazungumzia jeshi, ndiyo sababu kwenye vituo vyetu vya polisi kuna madawati ya jinsia, hivyo tunaendelea kutekeleza azimio hilo,” amesema.

Amesema madawati hayo ni mahususi kwa kutambua uhitaji maalumu yanapokuja masuala ya usalama kwa watu wanaotendewa isivyo salama, ambao wengi wao ni wanawake na watoto hasa wa kike.

“Hivyo, mdahalo unaofanyika leo na uzinduzi unaokwenda kufanyika kesho vitakuwa ni nyenzo muhimu kwenye jitihada zetu za ulinzi  na usalama, kikanda na kimataifa, hapa tulipo na tunakokwenda.

Alizitaja miongoni mwa nguzo za azimio hilo lililoidhanisha mpango kazi wa taifa kuwa ni kuzuia migogoro isitokee.

Akizungumzia mdahalo huo na uzinduzi wa mpango kazi uliofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wanawake (UN Woman) na wadau mbalimbali, Mkuu wa Chuo cha Ulinzi  na Amani Tanzania, Brigedia Jenerali George Itang’ale amesema mdahalo na uzinduzi wa mpango kazi huo vinakwenda kuweka historia si tu kwa nchi, bali kwa jeshi na chuo.

“Umetoa fursa kwa wadau kukutana na kujadili kuhusu wanawake, amani na usalama, hii ni historia kwetu,” amesema.

Naye mkurugenzi wa Jinsia kutoka Zanzibar, Siti Abbas amesema mpango kazi huo ni mkakati wa kutekeleza yale yaliyokusudiwa kwa vitendo.