Beki la kazi kuifuata Simba Misri

SIMBA inapambana kuweka mambo sawa katika maeneo mbalimbali ya uwanjani ikiwa kambini nchini Misri, ambapo ikiwa huko imeshambulisha vichwa kadhaa vya maana tu katika kikosi chake vinavyosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Msimbazi.

Taarifa mpya ni kwamba timu hiyo inapambana kumalizana na beki mmoja wa kati ili akaungane na kikosi hicho kilichopo Cairo, kikijifua kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.

Eneo hilo la ulinzi ni mojawapo ambalo kwa mashabiki wa timu hiyo linawaumiza vichwa kwani limeondokewa na mabeki kadhaa akiwamo Che Malone Fondoh aliyetua USM Alger na Hussein Kazi aliyeachwa kisha akaenda zake Namungo FC.

Lakini, kama hiyo haitoshi ni kwamba Valentin Nouma, beki na winga wa kushoto amesepa huku nahodha Hussein Tshabalala akitimkia Jangwani alikojiunga na watani zao wa jadi, Yanga.

Si hivyo tu, pale nyuma Msimbazi kulikuwa na Kelvin Kijili, beki wa kulia aliyetimkia Singida Black Stars, hivyo kuliacha eneo la ulinzi likiwa na mapengo kibao.

Hali hiyo haijawashtua sana mabosi wa Simba kwani wameshaanza kuziba mapengo taratibu kwa kusajili nyota wapya, huku wengine wakitambulishiwa Misri walikopelekwa kujaribiwa kuona iwapo kazi wanaiweza – na kweli wakaiweza na kupewa mikataba.

Hapa nchini kwa muda mrefu sasa Simba imekuwa ikipambania saini ya Wilson Nangu, ambaye ni beki kisiki pale JKT Tanzania ili aende akazibe nafasi ya waliosepa na katika hilo wakati flani hapo kati JKT Tanzania ilieleza haendi kokote na kwamba keshaongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia.

Lakini, unaposoma hapa kuna moshi mweupe umeanza kuonekana katika jitihada za mabosi wa Msimbazi, kwani Simba imerejea kwa kasi JKT kuhakikisha inakamilisha usajili wa beki huyo aliye na mkataba mrefu utakaoisha 2028.

Taarifa za ndani zinasema Nangu aliyemaliza msimu uliopita na mabao mawili anaweza kuwa katika safari ya kwenda Misri kama mabosi wa pande mbili watafikia makubaliano ya kuuvunja mkataba ili JKT Tanzania ipate masilahi na mchezaji apate.

“Mazungumzo yanaendelea vizuri ya kuununua mkataba wake, hivyo kuna asilimia kubwa ya kukamilisha jambo hilo,” kimesema chanzo.