Mambo yameiva Dabi K’koo… Simba mtiti, Yanga mtiti

HUKO mtaani na katika mitandao ya kijamii kuna kelele nyingi za mashabiki wa soka wakitamani siku ziende haraka ili washuhudie Dabi ya Kariakoo ya kwanza kwa msimu wa 2025-2026.

Ndiyo, Simba iliyomaliza nafasi ya pili Ligi Kuu Bara, italazimika kuvaana na Yanga iliyobeba mataji yote msimu uliopita kuanzia Ngao ya Jamii, Ligi Kuu hadi Kombe la Shirikisho (FA).

Mechi hiyo ni ya Ngao ya Jamii itakayozindua msimu mpya wa mashindano ambao tofauti na msimu uliopita ilipohusisha klabu nne, safari hii inazikutanisha timu mbili tu – Simba na Yanga kwa kile kilichoelezwa ufinyu wa muda baada ya michuano ya CHAN 2024 kupigwa nchini.

Ipo hivi. Simba na Yanga zitakutana kwa mara nyingine katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuzindua msimu wa 2025 -2026, baada ya timu hizo kufunga msimu uliopita wa Ligi Kuu Juni 25 na Yanga kushinda mabao 2-0 na kutetea taji kwa msimu wa nne mfululizo kama ilivyokuwa kwa FA.

Mara baada ya Bodi ya Ligi kuachia kalenda ya mashindano kwa msimu ujao, mashabiki wa timu hizo wameanza kutambiana mtaani kwenye vijiwe vya kahawa na daladala sambamba na mtandaoni, kila mmoja akitamba kama vipi mechi ipigwe hata kesho kwa aina ya vikosi ilivyonavyo kwa sasa.

Simba kwa sasa ipo jijini Cairo, Misri ikijinoa kwa maandalizi ya msimu mpya na juzi ilicheza mechi ya pili dhidi ya ENPPI SC na kupoteza kwa mabao 4-3, baada ya awali ikiwa Ismailia, kushinda 2-0 dhidi ya Kahraba Ismailia, huku mastaa wapya na wa zamani kuonyesha uwezo mkubwa.

Yanga yenyewe imetoka Kigali Rwanda ilipoenda kushiriki Tamasha Maalumu la klabu ya Rayon Sports ‘Rayon Sport Day’ na kupata ushindi wa mabao 3-1 na kunyakua taji la kwanza mapema, huku nyota wa timu hiyo wakiupiga mwingi na kuwapa mzuka mashabiki wa klabu hiyo.

Kila upande unaamini una mziki wa kutisha wa kukabiliana na timu yoyote ikizingatiwa klabu hizo zinajiandaa pia na mechi za awali za raundi ya kwanza za Ligi ya Mabingwa msimu ujao, Yanga ikipewa Wiliete Banguela ya Angola wakati Simba ikipangwa na Gaborone United ya Botswana.

Ukiacha tambo za mashabiki na hata zile zinazotolewa na Maofisa wa Habari wa klabu hizo, ukweli ni Simba na Yanga zote zina majembe ya maana ambao wanaweza kuunda vikosi zaidi ya viwili vikiwa na ukali uleule.

Ukweli Simba na Yanga zimeonyesha jeuri kubwa hadi sasa katika usajili wa kutengeneza vikosi vya msimu mpya, kwani makocha wa timu hizo, Fadlu Davids na Romain Folz wanaweza kuuanzisha vikosi vya kwanza na wale wanaosalia nje nako wanaweza kukiwasha kwa moto uleule.

Kifupi, Simba na Yanga nje mtiti na ndani pia mtiti na kama ingekuwa inawezekana kwa wapinzani kuamua wangejichagulia wenyewe vikosi gani vya kuvaana nao.

Katika timu hizo mbili, unaweza kuwaunganisha mastaa wapya wasiopungua wanne, watakaounganika na wale saba ambao walibaki kutoka kwenye timu ya msimu uliopita na hapo utachagua wewe unataka kukutana na mziki gani.

Tuanze na Simba, iliyoonyesha kuwa na hasira ya kutaka kupindua meza kwa  msimu ujao, kikosi cha kwanza kinaweza kuwa na sura tatu hadi ya nne mpya katika safu ya ulinzi, ikiwa imeshasajili nyota wa eneo hilo watatu na kumwongeza Hussein Ally kutoka timu ya vijana anayemkosha Fadlu.

Mabeki wapya ni Msauzi Rushne De Reuck, Anthony Mligo na Nady Camara ambaye ni raia wa Guinea anayemudu pia kucheza maeneo mengine ikiwamo kiungo, winga na ushambuliaji.

Kwa upande wa Simba, kocha Fadlu ana nafasi ya kuanzisha kikosi cha kwanza chenye majembe ya maana, huku wengine wakisubiri benchi kuliamsha wenzao wakizingua uwanjani.

Safu hiyo itakuwa na kipa Moussa Camara akiwa na mabeki Shomari Kapombe ambaye anapigiwa hesabu kubwa za kuwa nahodha mpya, baada ya kuondoka kwa Mohammed Hussein Tshabalala aliyetimkia Yanga, lakini wana Camara, Rushine De Reuck ambao ni wapya na Abdulrazack Hamza.

Eneo la kiungo kikosi hicho kitakuwa na Yusuf Kagoma, ingizo jipya Alassane Kante, Kibu Denis na Elie Mpanzu na Jean Charles Ahoua wakati mshambuliaji akiwa Jonathan Sowah.

Kwa upande wa Yanga jeuri waliyonayo ya kikosi cha kwanza kikiwa na ingizo moja la ulinzi, yaani Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, kwani langoni kama kawaida akakuwa Djigui Diarra, beki wa kulia ikishikiliwa na Israel Mwenda huku kati ikiwa na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Dickson Job.

Eneo la kiungo mabingwa hao watakuwa na watu wapya wawili, ikiwa na Mudathir Yahya, staa mpya Moussa Balla Conte, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua na Celestin Ecua ambaye naye ni mpya huku mshambuliaji akiwa Andy Boyeli.

Twende mziki wa pili wa Simba una balaa nao ukianza na kipa Yakoub Suleiman ambaye ni mpya akidaiwa anasubiri CHAN 2024 iishe atue Msimbazi, wakati kulia kuna David Kamata ‘Duchu’, huku ikielezwa kule Misri, kocha Fadlu anamjaribu kinda Ladack Chasambi kama beki wa kulia, lakini kuna Anthony Mligo upande wa kushoto, huku Chamou Karaboue na Semfuko Charles ambaye ni mpya wakikamilisha safu hiyo.

Eneo la kiungo kutakuwa na Mohammed Bajaber, Neo Maema, Morris Abraham ambao wote wapya, huku Awesu Awesu, Seleman Mwalimu na mshambuliaji atasimama Steven Mukwala, baada ya Leonel Ateba aliyedaiwa kuuzwa hapohapo Misri hivi karibuni, japo haijawekwa wazi ni timu ipi.

Kwa upande wa Yanga, ambao ni watetezi wa mataji yote ya ndani, wanajibu lao kwa mziki huo wa mnyama na itakuwa na kipa Aboutwalib Mshery, Kibwana Shomari, Chadrack Boka, Bakari Mwamnyeto na Abubakar Nizar ‘Ninju’ aliyesajiliwa hivi sasa kutoka JKU ya Zanzibar.

Eneo la kiungo kuna watu wa maana tu wakiwemo, Duke Abuya, watu wapya wanne Abdulnassir Mohammed ‘Casemiro’, Lassine Kouma, Mohammed Doumbia na Offen Chikola huku mshambuliaji akiwa Prince Dube.

Simba kule nje bado ina watu wakiwemo kipa Hussein Abel, Joshua Mutale, Mzamiru Yassin, Saleh Karabaka, mshambuliaji Valentino Mashaka, huku ikielezwa beki aliyekuwa JKT Tanzania, Wilson Nangu naye anaunda mziki wa Msimbazi na anaweza kuanzia kikosi chohcote kwa uwezo alionao, mbali na vijana kutoka timu za vijana za Wekundu hao.

Yanga nao watu wao wa nje watakuwa kipa Abubakar Khomeni, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Aziz Andambwile, winga mpya aliyetambulishwa rasmi jana Edmund John, Farid Mussa na Denis Nkane mbali na kina Shaibu Mtita na vijana wengine wanaojifua chini ya kocha Folz.

Licha ya timu zote kuwa na vikosi vilivyoonyesha uwezo mkubwa kipindi hiki, vikosi vikijifua kwa maandalizi ya msimu mpya wa mashindano ikiwamo Ngao ya Jamii, Ligi Kuu, Kombe la FA na Muungano kwa ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini zitakuwa na kazi mbele ya wapinzani wao.

Azam FC iliyopo chini ya kocha raia wa DR Congo, Florent Ibenge imeonekana kujipanga kwa aina ya wachezaji iliyowatambulisha hadi sasa wakiwamo wazawa na wale wa kimataifa ambao rekodi zao zinawabeba kuanzia kwa Japhte Kitambala, Papa Diallo Doudou, Issa Fofana na wengine.

Msimu uliopita Azam ilikuwa moja ya timu mbili zilizochukua pointi tatu mbele ya Yanga, pale ilipoifunga bao 1-0 kabla ya Tabora United kutonyesha mshono kwa kuifumua mabao 3-1, huku ikiokota pointi moja kwa Simba katika sare ya 2-2 baada ya awali kulala 2-0 visiwani Zanzibar.

Pia kuna Singida Black Stars ambayo ina kikosi cha maana chini ya Kocha Miguel Gamondi aliyerejea baada ya kutemesha kibarua wakati akiwa Yanga kutokana na vipigo hivyo viwili mfululizo kutoka kwa Azam na Tabora United.

Singida iliyomaliza nafasi ya nne msimu uliopita na kucheza fainali ya Kombe la FA kwa kuing’oa Simba katika nusu fainali kwa mabao 3-1 ni timu inayoonekana kuwa moto kwa majembe iliyoongeza licha ya kuwauza wachezaji wengine kadhaa akiwamo Josephat Bada na Jonathan Sowah.

Hapo ni mbali na Dodoma Jiji iliyobeba majembe ya maana, Mbeya City na Mtibwa Sugar zilizorejea katika Ligi Kuu, ukiacha Pamba Jiji, Namungo, JKT Tanzania, Coastal Union, Mashujaa, Tanzania Prisons, Fountain Gate na KMC iliyorudisha kocha Mbrazili Marcio Maximo nchini.