BAADA ya Namungo FC kuinasa saini ya beki wa kushoto wa KVZ, Ally Saleh Machupa kuziba nafasi iliyoachwa na Anthony Mligo, beki huyo mpya amefunguka matarajio aliyonayo katika maisha mapya Ligi Kuu Bara.
Machupa anakuwa mchezaji wa pili kutoka KVZ kutua Namungo kipindi hiki cha usajili wa dirisha kubwa baada ya hivi karibuni kipa tegemeo Suleiman Abraham kuingia mkataba wa mwaka mmoja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Machupa amethibitisha kumwaga wino wa mwaka mmoja kuitumikia Namungo huku akisema yupo tayari kufanya kazi na timu hiyo ili kufikia malengo yake.
“Dili hili la kusaini Namungo lilipitia katika uongozi wa timu yangu na baadaye nilitafutwa kukamilisha. Siwezi kusema ofa yangu, hayo ni mambo ya ndani ila nimeshaingia makubaliano nao na matarajio yangu ni kufanya vizuri kutimiza malengo niliyojiwekea,” alisema Machupa.
Machupa alisema kutua timu hiyo ni hatua mojawapo ya kufika anapohitaji na anaiona ni sahihi ya kumfikisha anapotamani.
Mchezaji huyo ni mdogo wa beki wa zamani wa Simba na Coastal Union, Adeyum Saleh ambaye pia amewahi kucheza Yanga, Ihefu na Dodoma Jiji akitumika katika nafasi ya beki wa kushoto.