CHAN 2024: Sudan, Senegal kazi ipo Amaan Complex

HATUA ya makundi ya michuano ya CHAN 2024 inafikia tamati usiku wa leo Jumanne kwenye viwanja viwili tofauti, jijini Dar es Salaam na visiwani hapa wakati timu nne za Kundi D zitapepetana kusaka nafasi mbili za mwisho za kutinga robo fainali.

Jijini Dar es Salaam, Nigeria iliyoaga mapema michuano hiyo kwa kupoteza mechi mbili za awali mbele ya Senegal na Sudan, itakwaruzana na Congo, huku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar watetezi Senegal itakuwa na kazi mbele wa vinara wa kundi hilo, Sudan.

Sudan inaongoza msimamo kwa sasa ikiwa na pointi 4 kama ilizonazo Senegal, lakini zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, huku Congo ikiwa ya tatu na alama mbili zilitokana na sare ilizovuna katika mechi mbili zilizopita.

Sudan imefunga mabao matano na kufungwa moja, wakati Senegal imefunga mawili na kuruhusu moja na kuanzia saa 2:00 usiku zitakuwa na kazi ya kupambana hapa Unguja ili kusaka timu ya kwenda robo fainali baada ya makundi ya A, B na C kumaliza kupata wawakilishi katika hatua hiyo.

Kundi B limetoa timu za Tanzania na Madagascar, wakati Kenya na Morocco zenyewe zimepenya kutoka Kundi A, ilihali Kundi C lilimalizia mechi zao usiku wa jana na leo itakuwa ni zamu ya Kundi D ambalo ndilo lililokuwa na timu nne tu na lisilohusisha wenyeji tofauti na makundi mengine.

Fainali hizo za nane zimeandaliwa kwa ushirikiano baina ya Tanzania, Kenya na Uganda na kila moja ilikuwa kituoni kwake sambamba na nyingine nne kwa vile makundi yao yalikuwa na timu tano kila moja, huku Tanzania na Kenya zikimaliza kibabe kwa kuongoza makundi yao.

Sudan iliyotoka kuiduwaza Nigeria kwa kuifumua mabao 4-0 katika mechi iliyopita inapigiwa chapuo ya kupenya katika kundi hilo kwa aina ya soka ililoonyesha hadi sasa ikibebwa zaidi na nyota wengi kutoka klabu ya Al Hilal, lakini hata Senegal inayotetea taji sio timu ya kubezwa.

Hili ni pambano la tano kwa timu hizo kukutana tangu mwaka 2012, huku Senegal ikiwa kinara kwa kushinda mara tatu kati ya nne walizocheza awali, moja iliisha kwa sare, mechi iliyopigwa Machi 22 mwaka huu ikiwa ni ya kuwania Fainali za Kombe la Dunia 2026.

Kutokana na rekodi hiyo, ni wazi Sudan itakuwa na kazi mbele ya Senegal ikitaka kujivua unyonge iliyonayo mbele ya wapinzani wao, lakini kwa kurejea namba za CHAN 2024, Sudan inaonekana kuwa bora na leo ni mechi ya kisasi na vuta nikuvute, japo sare yoyote kwa timu hizo na zinaweza kuwavusha kwenda robo fainali, hasa kama Congo itabanwa na Nigeria, jijini Dar es Salaam.

Sudan itamtegemea kinara wao wa mabao, Abdelrazig Omer mwenye mabao mawili, lakini ikiwa na nyota wenye uwezo wa kubadili matokeo kama ilivyowashtukiza Nigeria waliowapasua mabao 4-0.

Senegal iliyotwaa taji la CHAN katika fainali zilizopita, itaendelea kubebwa na Christian Gomis na Layousse Samb wanaomiliki bao moja kila mmoja, ili kuhakikisha wababe hao wanapenya robo na kuendelea na kazi ya kutetea ubingwa.

Kwa mechi ya Kwa Mkapa, Nigeria ambao ndio wenyeji wa pambano itakuwa inakamilisha ratiba tu kwani hata ikishinda haiwezi kuisaidia kwa lolote, kwa vile haina pointi yoyote, tofauti na Congo Brazzaville na ushindi utaifanya ifikishe pointi tano na kusikilizia mechi ya visiwani.

Kama Senegal au Sudan moja ikipoteza mjini Unguja, itamaanisha aliyeshinda ataenda na Congo hatua ya robo fainali, lakini iwapo zitatoka sare na Congo itaibuka na ushindi itaangaliwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, iwapo kama itashinda kwa idadi kubwa ya mabao.

Kwa sasa Congo imefunga mabao mawili na kufungwa mawili, hivyo kuzidiwa na wenzao wawili wa juu ambao sare yoyote itakuwa na manufaa kwa vile wana tofauti nzuri ya mabao hususani Sudan.

Timu mbili kati ya hizo tatu zikivuka hatua hiyo, zitakutana na washindi wawili kutoka Kundi C kwa mechi za robo fainali zinazotarajiwa kuanza rasmi Ijumaa kwa Kenya kuvaana na Madagascar kuanzia saa 11:00 jioni, kabla ya mshindi wa kwanza wa Kundi C kuvaana na mshindi wa pili wa Kundi D.

Jumamosi itakuwa ni zamu ya mechi kati ya Tanzania dhidi ya Morocco kuanzia saa 11:00 jioni na saa 2:00 usiku mshindi wa kwanza wa Kundi D atamalizana na mshindi wa pili wa Kundi C.