Dar es Salaam. Uzoefu unaonyesha kuwa wanafunzi wengi katika ngazi mbalimbali za elimu, wanahitimu bila kuwa na mwelekeo thabiti wa taaluma wanayotamani kuifuata.
Wakiwa wamezingirwa na presha za mitihani, matarajio ya wazazi, na soko la ajira linalobadilika kila uchao, vijana hawa hujikuta wakifanya uamuzi wa taaluma usioendana na vipaji, shauku wala ndoto zao.
Takwimu kwa mujibu wa utafiti wa shahada ya uzamili ya Sethy A wa mwaka 2017, zinaonyesha kuwa asilimia 84 ya wanafunzi nchini wanajikuta wakisoma fani ambazo hazihusiani kabisa na taaluma walizokuwa wameota au kupanga awali, huku asilimia 16 pekee ndio wanaoingia katika mwelekeo wa taaluma wanayoitamani.
Kwa mujibu wa wataalamu na wadau wa elimu, hali hii ni dalili ya wazi ya udhaifu wa mfumo wa shule katika kuwaandaa wanafunzi kwa maisha ya baada ya shule, si tu kitaaluma bali pia katika upangaji wa mwelekeo wa kazi kwa ujumla.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ushauri ya BNI Consulting na mchambuzi wa elimu, Isaa Baruti, anasema ipo haja kwa sasa wanafunzi wa Tanzania kufanya ziara katika maeneo mbalimbali, si tu kwenye mbuga za wanyama bali pia kwenye vituo vya polisi, hospitali na maeneo mengine ya kazi ili kuwawezesha kuuliza maswali yatakayowasaidia kuelewa aina ya kazi wanayotamani kufanya.
“Hapa Tanzania, imekuwa jambo la kawaida kuwaona vijana wakihangaika kufanya uamuzi kuhusu taaluma zao. Wanafunzi wengi wa shule wanapata ugumu kuchagua mwelekeo wa kazi unaolingana na maslahi yao, vipaji, shauku, haiba, malengo ya baadaye, na mahitaji yanayobadilika ya soko la ajira,” anasema.
Anaongeza kuwa shule zinapaswa kuwa na programu maalumu za ushauri wa kitaaluma, pamoja na vipindi maalum vya kuwaalika wageni kutoka kada mbalimbali kuzungumza na wanafunzi kuhusu taaluma na uzoefu wao kazini.
Mtafiti wa masuala ya elimu na jamii, Muhonyi Nkoronko, anasema kuna sababu nyingi zinazochangia wanafunzi kuchagua masomo au taaluma ambazo si chaguo lao la kweli, hali anayosema inachangiwa na mfumo wa shule, wazazi, jamii na hata marafiki.
“Wanafunzi wanachagua masomo bila kuzingatia uwezo wao wa ndani. Mwishowe, wanashindwa kuyasomea kwa kiwango cha juu au kuyatekeleza kwa ufanisi katika kazi,” anaeleza.
Anasisitiza kuwa kuna haja ya shule na wazazi kuunda mfumo mzuri wa kuwawezesha wanafunzi kuchagua masomo sahihi, ili wanapomaliza elimu yao wawe na uwezo wa kufanya kazi kikamilifu.
Anasema dunia ya sasa inahitaji watu wenye ujuzi wa kiwango cha juu unaolingana na mahitaji ya soko la ajira.
Kwa upande wake, mdau wa elimu ambaye aliwahi kuwa Meneja wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet), Nicodemu Shauri, anasema tatizo la wanafunzi kusoma masomo ambayo si chaguo lao, halitakoma hadi pale kutakapozinduliwa kampeni maalum ya kutokomeza elimu ya maneno bila vitendo.
“Suala la ufadhili wa masomo, kwa mfano kwenda kusoma nje ya nchi, ni mojawapo ya sababu zinazowafanya wanafunzi kusoma masomo ambayo si chaguo lao la kweli. Mara nyingi huchagua ili tu wapate nafasi ya kwenda nje. Vilevile, msukumo kutoka kwa wazazi ni sababu nyingine. Mzazi anapofanya kazi fulani, humlazimisha mtoto wake kufuata njia hiyo hiyo. Aidha, changamoto ya ajira ni miongoni mwa sababu zinazowafanya wanafunzi kuhama kutoka kwenye masomo waliyo nayo moyoni,” anasema.
Anaongeza kuwa, ingawa Serikali tayari imeanzisha mtalaa wa elimu ya vitendo (elimu ya amali), utekelezaji wake umekurupushwa kutokana na changamoto kadhaa zikiwemo miundombinu duni, uhaba wa vitendea kazi na idadi ndogo ya walimu, hali inayofanya iwe vigumu kuwahudumia wanafunzi wengi kwa ufanisi.
Shauri anashauri Serikali kuanzisha kampeni maalum ya kuimarisha elimu kupitia mfumo wa mkondo wa amali na mkondo wa jumla, akisema hatua hiyo itarahisisha kufikia malengo ya elimu yanayolengwa na Taifa.
Walimu na wanafunzi wanasemaje?
Baadhi ya walimu wa vyuo vikuu na shule za sekondari wanasema kuwa shule zinapaswa kuwa vyanzo vya mwongozo kwa wanafunzi katika kuchagua masomo au taaluma kulingana na maisha ya sasa na uwezo wao binafsi.
Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kibaha, Madam Aziza, anasema ni muhimu kuanzisha mfumo maalum wa kugundua na kukuza vipaji vya wanafunzi mapema.
“Ni vyema kuwa na mtalaa unaotambua vipaji vya wanafunzi tangu awali. Kwa mwaka huu 2025, baadhi ya shule tayari zimeanzisha mikondo ya amali na mikondo ya jumla. Hii inampa mwanafunzi wa kidato cha kwanza nafasi ya kuchagua mapema masomo anayoyapenda,” anasema.
Naye mwalimu Issa Selemani, anasema mfumo huo utawasaidia wanafunzi si tu kuwa bora kitaaluma, bali pia kujiamini na kutumia uwezo wao kwa manufaa ya jamii.
“Kama walimu, tunaona vipaji vya watoto mapema, wapo wa kisayansi, wa sanaa, michezo au hata uongozi. Mfumo rasmi wa kukuza vipaji ukianzishwa shuleni, utawasaidia wanafunzi kufanikisha maisha yao kwa njia bora,” anasema.
Mmoja wa wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Jangwani, anayesoma kidato cha sita, Magdalena Joseph, anasema:
“Nilikua na ndoto ya kuwa mjasiriamali tangu nikiwa darasa la sita, lakini nilipofika sekondari niliona mazingira ya shule na jamii yananisukuma kuchukua masomo ya sayansi kwa sababu nilikuwa na ufaulu mzuri kwenye masomo hayo.”
Anasema hajawahi kupata nafasi ya kupokea ushauri kuhusu ulinganifu wa vipaji vyake na masomo anayoyasoma, hali inayomfanya kuhisi kuwa amechagua mwelekeo wa maisha kwa shinikizo badala ya uamuzi wa ndani ya moyo wake.
“Sasa natamani ningekuwa kwenye mchepuo wa biashara au masomo ya sanaa,” anaongeza kusema Magdalena.