Dar es Salaam. Katika dunia inayobadilika kwa kasi, watoto wanahitaji zaidi ya maarifa ya darasani ili kufanikiwa.
Wanahitaji kuwa wabunifu, wadadisi, na wenye uwezo wa kufikiri kwa kina na kwa njia tofauti.
Udadisi humwezesha mtoto kuuliza maswali, kuchunguza, na kutafuta maarifa zaidi; huku ubunifu ukimpa uwezo wa kutatua changamoto, kuunda mawazo mapya, na kuona fursa zisizo wazi kwa wengine.
Udadisi na ubunifu si vipawa vya kuzaliwa navyo pekee; ni sifa zinazoweza kuendelezwa na kuimarishwa kupitia mazingira bora, malezi sahihi, na ushirikiano wa karibu kati ya wazazi, walimu, na jamii.
Makala haya yanachambua mbinu bora na rahisi ambazo mzazi au mlezi, unaweza kutumia kuchochea mahiri au stadi hizi muhimu kwa mtoto.
Mtoto mdadisi huanza kwa kuuliza maswali. Badala ya kuona maswali haya kama usumbufu, mzazi au mlezi anapaswa kuyaona kama fursa ya kujenga fikra za mtoto.
Kuuliza maswali ya kuruhusu fikra kama, “Kwa nini unadhani jua hutoweka usiku?” kunamfanya mtoto afikiri, atafakari, na ajifunze.
Aidha, mzazi anapaswa kumuuliza mtoto maswali ya kufungua akili kama, “Ungeweza kubadilisha kitu chochote duniani, kingekuwa nini na kwa nini?”
Maswali haya huendeleza uwezo wa kutafakari kwa kina, huamsha udadisi wa kujua zaidi na huandaa mazingira ya ubunifu.
Udadisi na ubunifu huzaliwa kupitia uzoefu wa moja kwa moja. Watoto wanapopewa nafasi ya kugusa, kujenga, kubomoa na kujaribu tena, wanakuwa huru kufikiria nje ya mipaka ya kawaida.
Shughuli rahisi kama kutengeneza michezo ya kuigiza, kuchora picha za mawazo yao, au kuunda vifaa kutoka vitu vya nyumbani, huamsha ubunifu.
Kwa mfano, badala ya kumnunulia mtoto kigari cha kuchezea, mpe vifaa na mwelekeze atengeneze kigari chake mwenyewe kwa kutumia visoda, vijiti, na gundi.
Kwa njia hii, mtoto anajifunza zaidi kuhusu matumizi ya vifaa, uvumilivu, na ubunifu wa kutatua changamoto anazokutana nazo.
Usomaji wa pamoja sio tu njia ya kukuza lugha, bali pia ni kichocheo muhimu cha udadisi na ubunifu.
Vitabu humpeleka mtoto katika dunia ya kufikirika, na kumtambulisha kwa mawazo mapya.
Baada ya kusoma, mjadili na mtoto: “Ungekuwa mhusika mkuu, ungefanya nini tofauti?” au “Unadhani hadithi ingetokeaje kama ingetokea leo?”
Maswali haya huchochea uwezo wa kufikiri kipekee na kumwezesha mtoto kuhusisha masomo na maisha halisi.
Zaidi ya hayo, mtoto anaweza kuhamasika kuandika hadithi zake mwenyewe, kitu ambacho ni hatua mojawapo ya ukuaji wa ubunifu wa kisanaa na wa kihisia.
Kuwa mfano wa udadisi na ubunifu
Watoto hujifunza kwa kuiga. Mzazi anapojihusisha na shughuli za kujifunza kama kusoma vitabu, kutazama vipindi vya kielimu, au hata kujifunza jambo jipya, anamtia mtoto moyo kufanya vivyo hivyo.
Vilevile, kuonesha ubunifu kwa vitendo kama kuchora, kupika mapishi mapya, au kutengeneza vitu kwa mikono, kunamvutia mtoto kujihusisha na shughuli hizo.
Mtoto anapoona mzazi akifurahia kugundua mambo mapya, naye anahamasika kujifunza bila kushurutishwa. Hili huweka msingi wa kujifunza maisha yote.
Ubunifu huota mizizi katika mazingira ambako mtoto anajisikia salama kujieleza.
Mtoto anapojua kuwa maoni yake yanaheshimiwa, hata kama si sahihi au ya kawaida, atakuwa na ujasiri wa kusema, kuuliza na kujaribu vitu vipya.
Mzazi au mlezi anapaswa kuepuka kukosoa kila wazo la mtoto.
Badala yake, apewe fursa ya kueleza mawazo yake. Kwa mfano, mtoto akichora picha isiyoeleweka, badala ya kusema “Hii si nzuri,” unaweza kusema, “Ningependa kusikia kuhusu picha yako, hivi ni kitu gani unachotuonesha hapa?”
Maneno haya humtia moyo na kumwelekeza kuboresha bila kumvunja moyo.
Mshirikishe kutatua changamoto
Watoto wanaojifunza kutatua matatizo hukua wakiwa wabunifu na wachambuzi wa hali.
Kwa mfano, familia inapopanga bajeti ya safari au mpango wa mapumziko ya mwisho wa wiki, mtoto anaweza kuulizwa: “Tuna bajeti ya Sh20,000, tufanye nini tupate burudani?” Mtoto atajifunza kuangalia vipaumbele, kupanga na kutoa mawazo bunifu.
Hii si tu njia ya kumfundisha maisha ya kiuhalisia, bali pia ni nafasi ya kujenga uwezo wake wa kupanga mikakati na kufikiri kwa njia mbadala.
Dhibiti matumizi ya teknolojia
Teknolojia ni nyenzo muhimu ya maarifa, lakini matumizi yake yasipodhibitiwa yanaweza kudidimiza udadisi wa mtoto.
Michezo ya video na vipindi vya televisheni vinapotoa burudani ya haraka na isiyohitaji jitihada, mtoto anakosa fursa ya kuichangamsha akili yake mwenyewe.
Ni muhimu kuweka mipaka ya muda wa matumizi ya vifaa hivi, na badala yake mwelekeze mtoto kushiriki katika michezo ya kijamii, ya kubuni, au ya ujenzi wa fikra.
Teknolojia inaweza kutumika kwa njia chanya pia, kwa kuchagua vipindi vya kielimu, majaribio ya kisayansi ya kufuatilia, au programu za kutengeneza vitu kama vya sanaa.
Udadisi na ubunifu hustawi panapokuwa na tofauti ya mazingira na uzoefu. Mtoto anapopelekwa kwenye makumbusho, maonyesho ya sanaa, mashamba au maeneo ya kihistoria, anapata mtazamo mpya wa dunia.
Mazingira haya humfunulia mitazamo mipya, kukuza maswali, na kumhamasisha kuunda mawazo yake binafsi.
Nikwambie kitu mzazi, hata kumtaka abadilishe ratiba ya kila siku au kumruhusu apange shughuli zake mwenyewe kwa siku moja, kunaweza kuleta mabadiliko makubwa katika njia anavyofikiri na kujieleza.
Katika karne ya 21, udadisi na ubunifu si nyongeza, bali ni misingi ya mafanikio. Mtoto aliye mdadisi hujifunza zaidi na haraka na anaweza kukabiliana na changamoto kwa mbinu bunifu.
Wazazi, walezi na walimu wana nafasi muhimu ya kusaidia watoto kukuza sifa hizi kwa kutoa mazingira yanayowahimiza kuuliza, kujaribu, kushindwa, na kujaribu tena bila woga.
Kwa kuwapa watoto nafasi ya kufikiri kwa uhuru, kuchunguza bila mipaka, na kujifunza kwa shauku, tunawajengea msingi imara wa kuwa wachanganuzi wa kesho, wabunifu wa suluhisho na viongozi wa mabadiliko. 0754990083