Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na viongozi wa Ulaya wamefanya mazungumzo kuhusu vita vya Ukraine na Rais wa Marekani, Donald Trump katika Ikulu ya White House.
Mkutano huo wa kihistoria kati ya Zelensky na Trump na vigogo wa Ulaya umekuja ikiwa ni siku chache baada ya mkutano wa Alaska wa Rais wa Marekani na Rais wa Russia Vladimir Putin kuhusu mazungumzo ya kusitisha mapigano nchini Ukraine, ambayo yaliisha bila makubaliano ili kupata amani.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kuanzia jana saa tisa mchana kwa saa za Marekani, Rais Zelensky amesema yuko tayari kuzungumza na mwenziye Putin ikiwa ni juhudi za kumaliza vita hivyo vilivyoanza baada ya uvamizi wa Februari 24, 2022.
Mkutano huo uliwakutanisha viongozi wa Ulaya akiwemo Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, Keir Starmer Waziri Mkuu Uingereza, Emmanuel Macron Rais wa Ufaransa, Friedrich Merz Kansela wa Ujerumani.

Katika mazungumzo hayo ya jana kati ya Trump na Zelensky yalionekana yenye urafiki zaidi ikilinganishwa na mkutano wao wenye mvutano mwezi Februari yaliyogonga vichwa vya habari kutokana na namna Zelensky alivyoingia na kutoka White House.
Hata hivyo baada ya mkutano huo Rais Trump amesema amempigia simu Rais wa Urusi, Vladimir Putin ili kupanga mkutano kati yake na Zelensky.
Kwa mujibu wa BBC, Zelensky ameseema yuko tayari kukutana na Putin ana kwa ana, au hata kwa ushirikiano na Trump.
Akieleza zaidi, Trump amesema dhamana za usalama kwa Ukraine zitatolewa na nchi za Ulaya na Marekani kwa uratibu.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer amesema mazungumzo juu ya dhamana hizo yataendelea leo.
Rose Goettemoeller, aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Nato, amesema kauli ya Putin kutambua haja ya dhamana za usalama na ushiriki wa Marekani ni hatua kubwa kuelekea amani na faraja kubwa kwa nchi za Nato.
Waziri Starmer amesema kulikuwa na mshikamano wa kweli na hakuna uamuzi utakaofanywa bila Ukraine kushirikishwa.
Kansela Merz amesema mkutano ujao hauwezi kufanyika bila kusitishwa mapigano.
Rais Macron amesema wanajeshi wa Ulaya wanaweza kushiriki kusaidia Ukraine.
Waziri Mkuu wa Finland, Alexander Stubb ameonya hakuna uhakika wa ushiriki wa Marekani kwenye dhamana hizo na asema Putin “Hawezi kuaminika”.
Waziri Mkuu Meloni amesema swali kubwa ni jinsi ya kuhakikisha hali hii haitajirudia.
Kwa upande wake Ursula von der Leyen, amesema Urusi inapaswa kuwarejesha watoto wa Ukraine waliotekwa.
Katibu Mkuu wa Nato, Mark Rutte (Katibu Mkuu wa Nato): Amemweleza Trump kama “mpatanishi mwenye uhalisia”.
Zelensky baada ya kikao amesema yupo tayari kwa mkutano wa na Putin na huenda pia wa pande tatu akihusishwa na Trump.
Amesema amezungumza na Putin na maandalizi yanafanywa kwa ajili ya mkutano kati ya Zelensky na Putin, kisha mkutano wa pande tatu.
Asema dhamana za usalama zitashirikishwa na nchi za Ulaya huku Marekani ikiratibu.
Mke wa Rais wa Ukraine, Olena Zelenska amemuandikia barua mke wa Trump, Melania Trump ikiwa ni tukio la nadra kwa wenza hao.
Jana Jumatatu Rais Zelensky aliwasilisha barua iliyoandikwa na mke wake, kwenda kwa Melania Trump na akatoa shukrani kwa ombi lake la kuwalinda watoto.

“Sio kwako, ni kwa mke wako,” Zelensky amemwambia Rais Trump.
Hata Melania ameandika barua kwa Putin akitaka ulinzi wa watoto duniani.
“Kila mtoto huwa na ndoto zilezile za utulivu moyoni mwake, iwe alizaliwa kwa nasibu katika eneo la kijijini au katikati mwa jiji lenye fahari. Wana ndoto ya upendo, uwezekano, na usalama kutokana na hatari,” Melania ameandika kwamba Putin, anaweza kurejesha kicheko.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari takriban watoto 20,000 wameondolewa kwa lazima au kufukuzwa kutoka Ukraine.