KIKOSI cha KMKM kinaendelea kujifua hapa visiwani Zanzibar kujiandaa na mechi ya raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho dhidi ya As Port ya Djibouti, huku kocha mkuu wa timu huyo Ame Msimu akipiga mkwara mzito.
Kocha huyo amesema hana presha kwenda kuivaa AS Port kwa vile walishawahi kuvaana nao, hivyo wanajua namna ya kuwasulubu watakapokutana na9 mwezi ujao.
KMKM iliyotaka tiketi ya CAF kwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho (FA), kinajifua kwenye kambi ya mazoezi iliyopo Uwanja wa Mao mjini Unguja, Zanzibar ikiwa imefanya usajili kujiimarisha kikosi baada ya kuwasoma wapinzani wao hao watakaanza nao ugenini Septemba 19 na kurudia Septemba 26.
Akizungumza na Mwanaspoti, Msimu amesema wamekutana na timu hiyo katika michuano ya Kombe la Kagame iliyofanyika Dar es Salaam na waliifunga bao 1-0 na walirudiana tena Rwanda 2019 waliwafunga tena bao 1-0.
“Ni timu tunayoifahamu japo ni muda kidogo, zaidi ya miaka mitano tunaamini kutakuwa na mabadiliko kibao hilo halitupi shida, kwani tumeanza kuwafuatilia kwa kuangalia video zao za miaka ya karibuni,” amesema Msimu na kuongeza;
“Unajua mpira unakua msimu hadi msimu hata wao naamini wanajua timu yetu ni ya aina gani hivyo mipango ni kusomana kimya kimya ili tujiweke katika mazingira mazuri kuvuka hatua hii na kwenda inayofuata.”
Akizungumzia maandalizi kwa ujumla amesema yanaendelea vizuri na wachezaji wanaonyesha kuwa na uhitaji wa kuutaka mchezo huo ili kuandika rekodi ya kujindoa unyonge wa rekodi ya kutolewa hatua ya awali kila msimu kwa timu za visiwani.
“Tuna faida kubwa kwenye kikosi chetu hatujafanikiwa kufanya biashara yoyote dirisha hili zaidi tumeongeza nguvu ili kujiimarisha na matarajio yetu ni makubwa kuhakikisha tunavuka hatua hii.”
KMKM ikifanikiwa kuiondoa AS Port ya Djibouti itakutana na mshindi wa mechi kati ya Azam FC na El Merriekh Bentiu ya Sudan Kusini.