Jinsi mke wa Trump, Zelenskyy wanavyosaka amani Ukraine

Dar es Salaam. Moja ya tukio lililogonga vichwa vya habari katika mkutano wa Rais Donald Trump wa Marekani na Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine jijini Washington DC jana Jumatatu ni barua za wake wa marais hao, katika kutafuta amani ya Ukraine na Russia.

Kabla ya mkutano na viongozi wa Ulaya pamoja na Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, Keir Starmer Waziri Mkuu Uingereza, Emmanuel Macron, Rais wa Ufaransa, Friedrich Merz, Kansela wa Ujerumani, Zelenskyy alimkabidhi Trump barua hiyo na kumwambia ‘ni ya mkeo Melania sio ya kwako’.

Barua hiyo ya mke wa Rais wa Ukraine, Olena Zelenska, inahusu shukurani kwa mke wa Rais wa Marekani, Melania Trump, kwa hatua yake ya kumkosoa Rais wa Russia, Vladimir Putin.

Melania amekuwa mkosoaji wa wazi wa Putin na wiki iliyopita aliandika barua akimtaka alinde watoto, kufuatia ripoti kwamba angalau watoto 20,000 wamechukuliwa na wanajeshi wa Russia tangu uvamizi wa mwaka 2022. Kwa mujibu wa dazeti la Daily Mail la Uingereza.

Taarifa zingine zinaonyesha idadi hiyo inaweza kufikia hadi watoto 300,000 waliotekwa kutoka Ukraine na kupelekwa Russia au maeneo wanayoyakalia bila ridhaa ya familia zao.

Zelenska alitaka kushukuru kwa hatua hiyo na kupitia mumewe, Rais Volodymyr Zelenskyy, alikabidhi barua hiyo kwa Rais Trump ili aipate Melania. Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Zelenskyy ameandika:

“Ninataka kumshukuru Mama wa Taifa wa Marekani, Melania, kwa kulipa kipaumbele suala moja la maumivu na gumu zaidi la vita hivi utekaji wa watoto wa Kiukraine na Russia. Tunathamini huruma yake na barua yake kwa Putin.”

Aliongeza kuwa suala hilo ndilo kiini cha janga la kibinadamu nchini Ukraine watoto, familia zilizovunjika na maumivu ya kutengana. Pia, alisisitiza Serikali yake inaendelea kufanya kila juhudi kuwarudisha watoto, wafungwa wa vita na raia waliokamatwa na Russia tangu mwaka 2014.

Kwa upande wake, Rais Trump amesema suala la watoto waliotekwa limejadiliwa pia katika mazungumzo yake na Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, na kwamba dunia itashirikiana kuwarudisha nyumbani kwa familia zao.

Katika barua yake, Melania amemwambia Putin kama kiongozi wa dunia, jukumu la kulinda watoto ni la lazima:

“Kila mtoto ana ndoto moyoni mwake ndoto za upendo, matumaini na usalama. Ni jukumu letu kama wazazi na viongozi kuhakikisha kizazi kijacho kinapata hifadhi na heshima,” aliandika.

Alimuhimiza Putin achukue hatua ya kurejesha furaha ya watoto na kwa kufanya hivyo hatatumikia Russia pekee bali pia ubinadamu mzima.

Hata hivyo, haijulikani matokeo ya mazungumzo ya Trump na viongozi hao wawili yatakuwa nini. Baada ya kukutana na Putin, Trump alisema walikuwa na mazungumzo yenye tija ingawa hakupata makubaliano ya kusitisha mapigano mara moja.

Alipokutana na Zelenskyy, Trump aliahidi msaada wa kijeshi iwapo makubaliano ya amani yatafikiwa, akisisitiza kuwa Marekani itatoa ulinzi kuhakikisha usalama unakuwepo.

Zelenskyy, kwa upande wake, amesema mazungumzo na Trump yalikuwa ya ukaribu na yenye tija, na akaeleza kuwa yupo tayari kwa kikao cha viongozi wakuu ili kutatua masuala magumu na yenye maumivu ya vita.