Matumizi ya kuni, mabadiliko ya tabianchi yanavyochochea utoro shuleni Mwanza

Mwanza. Pamoja na Mkoa wa Mwanza kuonesha mafanikio makubwa katika kupunguza kiwango cha utoro na kuongeza mahudhurio ya wanafunzi shuleni, bado changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi na matumizi ya nishati duni ya kupikia zinaendelea kuathiri mazingira ya ujifunzaji.

Kwa familia nyingi, hasa zile zenye kipato cha chini, kuni ndizo nishati kuu ya kupikia. Hali hii inawalazimu watoto kutumia muda mwingi kutafuta kuni badala ya kuhudhuria masomo.

Siwema Alex, mwanafunzi wa kidato cha kwanza na mkazi wa Bulale, anasema familia yake hutegemea kuni kwa sababu hawawezi kumudu gharama za mkaa au gesi.

“Nyumbani tunatumia kuni mara nyingi kwa sababu mfuko wa mkaa unauzwa kuanzia Sh1,000, na kwa familia yenye mahitaji makubwa ya chakula, kiasi hicho hakitoshi. Gesi ni ghali zaidi, hatuwezi kuimudu,” anasema.

Siwema, mtoto wa kwanza nyumbani kwao, husaidia mama yake kutafuta kuni na kupikia wadogo zake. Mara nyingi huchelewa shuleni au hukosa kabisa vipindi.

“Kuni tunazipata bure kwenye misitu au miti iliyokauka. Hata kama tunanunua, bei yake si kubwa ukilinganisha na gesi. Hivyo, pamoja na kutamani kutumia nishati safi, uwezo wa kifedha hauturuhusu,” anasema.

Kulwa Missango, ambaye ni mama wa Siwema, akizungumza kwa masikitiko, anasema anatamani watoto wake wasikose masomo kwa sababu ya kuni.

“Kama tutapata mtungi wa gesi, bado tatizo litakuwa ni gharama za kujaza. Serikali ikipunguza bei, wengi wetu tutatumia gesi. Lakini kwa sasa, maisha magumu yanatulazimisha kuendelea kutumia kuni,” anasema.

Mabadiliko ya tabianchi na maisha ya wanafunzi

Mbali na changamoto za nishati, mabadiliko ya tabianchi nayo yanaathiri ustawi wa wanafunzi. Wanahabari watoto wa Shirika la Mtandao wa Watoto na Vijana Mwanza (MYCN) wanasema hali ya hewa isiyo ya kawaida imekuwa ikivuruga maisha ya jamii na shule.

Samweli Fides, mwanafunzi wa Shule ya Msingi Magaka, wilayani Ilemela, anasema familia zinazotegemea kilimo, ufugaji na uvuvi hukumbwa na ukata mkubwa wakati wa mafuriko au ukame.

“Mara nyingi mazao hufa au kusombwa na maji, mifugo hufa kwa kukosa malisho, na samaki hupungua. Hali hii inapunguza kipato cha familia na watoto hukosa mahitaji ya msingi, ikiwemo chakula na ada za shule,” anasema.

Anabainisha kuwa mabadiliko hayo yameathiri afya na elimu ya watoto.

“Kama awali familia ilikuwa ikitoa milo mitatu kwa siku, sasa huenda ikashuka hadi mlo mmoja. Hali hii huwafanya wanafunzi washindwe kuzingatia masomo.”

Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Martine Nkwabi, anakiri kuwa changamoto hizo zinachangia utoro.

“Endapo familia haina uwezo wa kununua kuni, na anayelazimika kuzitafuta ni mtoto, basi ni dhahiri ataathirika kielimu. Vilevile, ukame na upungufu wa mvua huchangia kukauka kwa visima ambavyo shule nyingi hutegemea. Shule zisizo na maji husababisha wanafunzi kukimbia kutokana na changamoto za usafi,” anasema.

Nkwabi anasema hatua zimeanza kuchukuliwa kuhakikisha shule zinatumia nishati safi.

“Kati ya shule 27 za bweni zenye kidato cha tano na sita, shule mbili pekee ndizo bado zinatumia kuni. Hata hivyo, kuanzia mwaka huu nazo zitahamia kutumia gesi. Kwa shule za msingi na sekondari zinazopika chakula cha mchana, bado nyingi zinatumia kuni, lakini tunatafuta namna ya kuzihamasisha kubadilika,” anasema.

Anaeleza kuwa visababishi vya utoro viko kwenye familia, shule na tabia za mwanafunzi mwenyewe, japo anakiri kwa kiasi kikubwa utoro huchangiwa na maisha ya familia ya mtoto na mazingira yanayomzunguka.

“Familia zinachangia zaidi ya asilimia 60 ya utoro. Watoto hutumwa kutafuta maji au kuni, na umaskini huwa chanzo kikubwa. Pia, baadhi ya shule hujenga mazingira yasiyofaa kwa wanafunzi, ikiwemo adhabu kali zisizoendana na makosa,” anasema.

Nkwabi anasema kutokana na maboresho yaliyofanywa, kiwango cha utoro kimepungua kutoka asilimia 21 mwaka 2020 hadi wastani wa asilimia 3.2 sasa kwa shule za mkoa huo.

“Tunalenga kufikia asilimia moja au sifuri mwishoni mwa mwaka huu,” anasema.

Hatua za kuhifadhi mazingira

Katika kukabiliana na changamoto hizo, halmashauri za Mwanza hupanda miti milioni moja kila mwaka, hasa shuleni.

“Tangu mwaka 2021, tumeshajenga shule mpya 37 za msingi na sekondari, na ujenzi huo umeenda sambamba na utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti,” anasema Nkwabi.

Ofisa Mradi wa Ustahimilivu Endelevu wa Mabadiliko ya Tabianchi kwa Watoto mkoani Mwanza, Nuru Massanja, anasema mradi wa majaribio wa mwaka 2024/25 katika wilaya za Ilemela na Nyamagana ulibaini changamoto ­­kubwa mbili zinazochangia utoro ambazo ni ukosefu wa maji na uhaba wa chakula.

“Watoto hutumwa kila asubuhi kutafuta maji kabla ya kwenda shule. Wengine huchelewa au huamua kujificha ili kuepuka kwenda darasani. Pia, njaa ni tatizo kubwa. Baadhi ya wanafunzi huondoka shule mchana kwenda kula nyumbani au mashambani na kisha hawarudi tena,” anasema.

Ameeleza kuwa wazazi kutoka kata zilizoshiriki mradi, kama Sangabuye na Kayenze, walieleza jinsi ukame na upungufu wa samaki vinavyopunguza kipato cha familia.

“Wakati mazao hayavuni vizuri au samaki wanapopatikana kwa shida, familia hupunguza idadi ya milo. Matokeo yake ni watoto kushindwa kusoma kwa sababu ya njaa au kushiriki shughuli za kujiongezea kipato,” anaeleza.

Takwimu za Energy Access Situation Report 2020/21 zinaonesha zaidi ya asilimia 85 ya Watanzania wanategemea kuni na mkaa kwa kupikia, hali inayojitokeza pia Mwanza kutokana na wingi wa kaya zenye kipato cha chini.

Katika Tanzania, takribani asilimia 90 ya kaya zinategemea kuni na mkaa kama chanzo cha kupikia, ambapo kuni zinachangia karibu asilimia 63.5 na mkaa asilimia 26.2. Kwa ujumla, ni kidogo sana (chini ya asilimia 10) ya Watanzania wanaopata nishati safi ya kupikia.

Kwa mujibu wa tovuti ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kuanzia Desemba 2024, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) imeanza kusambaza mitungi ya gesi (LPG) kwa bei ya ruzuku, ambapo kila wilaya imepangiwa mitungi 3,255 huku jumla ya mitungi 19,530 ikiuziwa kwa nusu ya bei halisi.

Pia, taasisi za umma kama Gereza la Butimba zimeanza kutumia nishati safi kama gesi na mkaa mbadala, hatua inayoadhimishwa na Bodi ya Nishati Vijijini kama ishara ya utekelezaji wa sera za Serikali.

Kwa malengo ya kitaifa, Tanzania inalenga asilimia 80 ya kaya kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2034, chini ya Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034.

Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.