Aliyembaka aliyekuwa mwanafunzi jela miaka 30

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imebariki adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela aliyohukumiwa Said Mohamed, baada ya kukutwa na hatia katika kesi ya ubakaji.

Said alikutwa na hatia ya kesi ya ubakaji wa aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tano mwenye umri wa miaka 15, kinyume na kifungu cha 180 (1) (2)  (e) na kifungu cha 131 (1) cha Kanuni ya Adhabu.

Mwathirika wa tukio hilo alidaiwa kwenda jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufanya kazi, lakini Said alimchukua na kukaa naye kwa muda wa wiki moja kama mke na mume ambapo alikuwa akifanya naye ngono mara kwa mara, kabla ya kumpeleka kufanya kazi ambako aligundulika kufanyiwa vitendo hivyo vya ukatili.

Hukumu hiyo imetolewa Agosti 15, 2025 na Jaji Awamu Mbagwa, aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo ya jinai namba 26790/2024 ambaye baada ya kuchambua hoja za pande zote mbili, amesema kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa bila kuachwa shaka.

Said alikuwa akipinga uamuzi wa Mahakama ya chini ambapo alidaiwa kati ya Novemba na Desemba 2022, katika eneo la Vingunguti, jijini Dar es Salaam alimbaka mtoto huyo.

Katika kuthibitisha kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watano ambao ni mwathirika wa tukio hilo, Rotaya Mohamed, Sajenti Sylvester, Sajenti Amir na Dk Gaudensia Edward pamoja na vielelezo vitatu.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa mwathirika wa tukio hilo akitokea wilayani Bunda Mkoa wa Mara mwaka 2022 akiwa mwanafunzi wa darasa la tano, ambapo alimpigia simu dada yake aliyekuwa akiishi Arusha kumweleza nia yake ya kwenda Dar es Salaam kufanya kazi.

Ilidaiwa dada yake alimuunganisha na mtu (Peter), ambaye alimweleza atamtafutia kazi, muda mfupi baadaye, Peter alimwita mwathirika wa tukio hilo kwamba ameshampatia kazi, akamtumia nauli.

Ilidaiwa kuwa alipokewa katika stendi ya Mabasi ya Magufuli, Mbezi na kupelekwa kwa mama Nabiri, ambako alifanya kazi kwa nusu mwezi, baadaye, Peter alimshawishi aache kazi hiyo akisema kwamba alikuwa amempata kazi bora zaidi.

Mahakamani hapo ilielezwa kuwa baada ya mwathirika wa tukio hilo kuacha kazi hakupelekwa sehemu nyingine kufanya kazi kama alivyokuwa ameahidiwa na badala yake Peter alimpeleka nyumbani kwake na kumgeuza kama mke wake.

Baada ya wiki moja, Peter alimkabidhi mwathirika wa tukio hilo kwa Said na kumwambia aishi naye kama mume wake ambapo kwa mujibu wa shahidi huyo wa kwanza mrufani alimpeleka nyumbani kwake na kuishi naye kwa muda wa wiki moja, huku akijamiiana naye mara kwa mara.

Alidai kuwa baada ya muda huo Peter alienda kwa Said na kumrudisha mwathirika wa tukio hilo nyumbani kwake na kuendelea kufanya mapenzi  kwa siku kadhaa, kisha akapelekwa kwa shahidi wa pili.

Akitoa ushahidi mahakamani hapo, shahidi wa pili alidai kuona mwathirika wa tukio hilo hakuwa sawa kwani hakuweza kutembea wala kukaa vizuri, na alipomuhoji alimwelezea changamoto alizopitia tangu awasili Dar es Salaam.

Shahidi huyo wa pili alimwita Ofisa Ustawi wa jamii kutoka shirika liitwalo Suma Ujata, linaloshughulikia ukatili wa kijinsia, ambaye alimuhoji mwathirika wa tukio hilo na kutoa taarifa polisi ambapo walipewa fomu ya polisi namba tatu (PF3).

Baada ya kupewa fomu hiyo walimpeleka Hospitali ya Mwananyamala ambako alifanyiwa uchunguzi na shahidi wa tano, ambaye alieleza uke wa mwathirika wa tukio hilo ulikuwa umevimba na ilionekana amepenyezewa kitu butu ambapo kutokana na hali yake alilazwa kwa siku tano.

Shahidi huyo alidai kumpigia mtu aliyempelekea binti huyo ambapo mtego ulifanikiwa kumkamata Peter katika hospitali hiyo.

Januari mosi 2023,ilidaiwa shahidi wa tatu, nne, mrufani na mwathirika walitembelea eneo la tukio (makazi ya mrufani) ambapo kwa mujibu wa shahidi wa tatu,   walikuta sofa, subwoofer na vyombo kwenye chumba cha mrufani kama ilivyoelezwa na mwathirika wa tukio hilo.

Mahakama hiyo baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili ilimkuta na hatia mrufani na kumuhukumu adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela.

Katika rufaa hiyo, mrufani alikuwa na sababu saba ikiwemo hakimu alikosea kisheria kumtia hatiani wakati hawakuthibitisha kosa hilo, pia alikosea kisheria kwa kumtia hatiani na kumuhukumu mrufani katika hukumu ambayo haikuzingatia matakwa ya lazima ya kifungu cha 312 (2) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Nyingine ni Hakimu alikosea kisheria  kwa kumtia hatiani mrufani kwa kuzingatia ushahidi wa upande wa mashtaka ambao haukuwa wa kutosha, wa ajabu, hauendani na kutoa hatia ya mrufani.

Katika rufaa hiyo mrufani alijiwakilisha mwenyewe mahakamani bila uwakilishi wa wakili, huku mjibu rufaa akiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Monica Ndakidemi.

Jaji Mbagwa baada ya kupitia hoja za pande zote mbili na mwenendo wa rufaa hiyo, amesema ni vema kutambua kuwa kinachohitajika katika kuthibitisha kesi ya ubakaji ni kupenya na kuwa kando ya hayo, hakukuwa na ubaya Hakimu kujadili ukatili wa kimwili ambao ulitekelezwa dhidi ya mwathirika wa tukio hilo.

Jaji amesema msingi wa kwanza, tatu, tano, sita na saba inaunganishwa na kuamuliwa kwa pamoja kwa sababu zote zinahusiana na mzozo mkuu ambao ni upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi yake dhidi ya mrufani bila shaka kinyume na kifungu cha 3(2)(a) na 110 cha Sheria ya Ushahidi.

Jaji amesema mrufani alidai kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka haukutosha, hauendani, na haukutegemewa kutoa hatia ya mrufani, hasa ushahidi wa shahidi wa kwanza kwani ulijaa utata na kukosa uaminifu.

Jaji Mbagwa amesema ameamua kutumia mamlaka kama Mahakama ya kwanza ya rufaa, kutathmini upya ushahidi na rekodi nzima ya rufaa.

“Hakika, kuna utata kuhusu watu waliokamatwa katika Hospitali ya Mwananyamala, shahidi wa nne alithibitisha kuwa ni mrufani (Said) na Kulwa ambao walikamatwa Hospitali ya Mwananyamala, huku PW2 ikieleza kuwa ni Charles na Peter waliokamatwa katika hospitali hiyo,”

“Vyovyote iwavyo, mkanganyiko huu ni mdogo na hauna maana, kilicho muhimu zaidi katika kesi hii, ni ukweli kwamba mrufai alimshikilia mwathirika wa tukio hilo chumbani mwake kwa karibu wiki, wakati ambapo alifanya ngono naye mara kwa mara,”amesema.

Jaji huyo amesema utata unaodaiwa hauendi kwenye mzizi wa jambo hilo, huku akinukuu rufaa ya jinai namba 76/2014 kati ya Lusungu Duwe dhidi ya Jamhuri.

Amesema Mahakama ilisema kuwa utata mdogo usioingilia mzizi wa kesi hiyo hauondoi ushahidi wa kuaminika, hivyo kutupilia mbali misingi hiyo ya rufaa.

Kuhusu utambulisho wa mrufani eneo la tukio, Jaji amesema ameridhika kwamba shahidi wa kwanza alimtambua mrufani kuwa ndiyo muhusika wa tukio hilo kwani alikaa kwake wiki nzima ambapo alifanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia mara kwa mara.

“Hii ilimuhakikishia fursa ya kutosha ya kumtazama mshambulizi. Kwa upande mwingine, ushahidi wa mrufani haukutikisa ushahidi wa upande wa mashtaka. Uwepo wa vitu vya nyumbani vilivyoelezewa na shahidi wa kwanza , kama vile sofa, godoro, vyombo, vilithibitisha hilo,”

Jaji amesema baada ya kutathmini ushahidi kwa ujumla wake, hajaona sababu kwa nini shahidi wa kwanza na wa pili, wangetunga kesi dhidi ya mrufani na kuwa katika mazingira hayo analazimika kuamini ushahidi wa upande wa mashtaka kuhusu kuhusika kwa mrufani katika kosa linaloshtakiwa.

“Kwa kuzingatia uchambuzi uliotangulia, ninaona kwamba malalamiko yaliyotolewa chini ya misingi ya 1, 2, 3, 5, 6, na 7 ya rufaa hayana mashiko na kesi ya mwendesha mashtaka ilithibitishwa bila shaka yoyote, hivyo natupilia mbali rufaa hii , ”