LIGI ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), imefikia patamu baada ya timu vigogo nane kutinga robo fainali inayotarajia kuanza Agosti 23, mwaka huu katika Uwanja wa Donbosco, Upanga.
Vigogo hao ni Dar City iliyomaliza ikiwa na pointi 30, Pazi (27), JKT (26), Stein Warriors (26), UDSM Outsiders (25), Savio (24), ABC (24) na Srelio (23). Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa timu hizo kutinga robo fainali kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo katika ligi hiyo yenye timu 16.
Dalili ya timu hizo kuingia robo fainali ilianza kuonekana baada ya timu kubakiza michezo miwili kila mmoja kutokana na kuzidiana pointi chache. Katika robo fainali timu zote zinategemea kuchezesha wachezaji waliocheza hatua za mwanzo.
Dar City inatarajiwa kuwa na Sharon Ikedigwe, Amin Mkosa, Ally Abdallah, Clinton Best na Jamal Marbuary, huku Soro Geofrey, Josephat Peter na Robert Tasire wakikiwapiga Pazi), ilhali Kanyinda Dani, Mikado Ebengo na Marcus Mark (UDSM). Kwa upande wao Victor Michael, Fotius Ngaiza, Abdul Kakwaya na Cosmas wataonyeshana kazi wakiichezea Vijana, huku Jonas Mushi, Brian Mramba, Sisco Ngaiza na Evance Davies wakiwa Stein Warrriors. Baraka Sabibi, Isakwisa Mwamsope, Jackson Brown na Omary Sadiki watakuwa JKT ilhali Ntibonela Bukeng, Godfrey Swai na Oscar Mwituka watavaa jezi za Savio.
Nao Soro Geofrey, Josephat Peter na Robert Tasire watakuwa katika uzi wa Pazi, huku Alinani Msongole na Elias Nshishi wakiichezea ABC ambapo Kanyinda Dani, Mikado Ebengo na Marcus Marc watatetea jahazi la UDSM Outsiders.
Katika mechi hizo robo fainali itakuwa ni kati ya Dar City na Srelio, Pazi itaumana na ABC, JKT itakipiga na Savio, Stein Warriors itaonyeshana kazi na UDSM.
Akizungumzia hatua hiyo, Kamishna wa Ufundi na Mashindano wa BDL, Haleluya Kavalambi alisema mfumo utakaotumika katika robo fainali ni ule wa timu kucheza mara tatu maarufu kama best of three playoff.