Tanzania, Kenya, Uganda zaandika rekodi CHAN 2024

TIMU za taifa za Tanzania, Kenya na Uganda zimeandika rekodi mpya katika soka la Afrika baada ya zote kwa pamoja kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) 2024 huku wakiongoza makundi yao.

Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa mashindano hayo, Tanzania, Kenya na Uganda zimepenya hatua ya mtoano, jambo linaloibua sura mpya kwenye ramani ya soka Afrika Mashariki.

Kenya imekuwa moja ya timu zilizoshangaza baada ya kushiriki mara ya kwanza na kuongoza Kundi A ilipokusanya pointi 10 na kuzizidi Morocco, Angola, DR Congo na Zambia.

Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Zambia katika mchezo wa kuhitimisha hatua ya makundi kupitia mfungaji Ryan Ogam dakika ya 75, uliwapa heshima Kenya kumaliza kileleni.

Tanzania nayo imekuwa kivutio baada ya kuibuka kinara wa Kundi B kwa pointi 10. Taifa Stars ilishinda mechi tatu na sare dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati mechi ya mwisho. Hii ni mara ya tatu inashiriki michuano hiyo ambapo awali 2009 na 2020 iliishia makundi. Kwa Uganda, hatua hii ni historia mpya baada ya kushindwa mara sita mfululizo kuvuka hatua ya makundi katika mashindano ya CHAN ambapo ilikuwa 2011, 2014, 2016, 2018, 2020 na 2022.

Safari hii ilionyesha ukomavu wa kiuchezaji na kupambana hadi dakika za mwisho kupata sare ya mabao 3-3 dhidi ya Afrika Kusini kwenye mechi ya kumaliza makundi iliyopigwa juzi Jumatatu.

Katika mechi hiyo, Uganda ilianza kufunga mapema kupitia Jude Ssemugabi, lakini baadaye Afrika Kusini ilirejea na kufunga mabao matatu.

Mashabiki wa Uganda walidhani ndoto yao imeota mbawa, lakini dakika za majeruhi Rogers Torach alisawazisha kwa mkwaju wa penalti baada ya Allan Okello kufunga la pili pia kwa penalti. Sare hiyo iliwaweka kileleni mwa kundi na kuipa timu hiyo nafasi ya kwanza kufika robo fainali.

Ratiba ya robo fainali inaonyesha Kenya itamenyana na Madagascar jijini Nairobi, Tanzania ikikabiliana na Morocco jijini Dar es Salaam ambapo mechi hizo zitachezwa Agosti 22, huku mshindi wa Kundi D akikutana na Algeria kisiwani Zanzibar na Uganda ikiikaribisha timu iliyomaliza nafasi ya pili Kundi D ambapo mchezo utapigwa jijini Kampala. Hizi zote zitapigwa Agosti 23.