MSHAMBULIAJI wa Morocco, Oussama Lamlioui, amesema mshikamano wa timu ndiyo msingi wa mafanikio ya Simba wa Milima ya Atlas kufuzu hatua ya robo fainali katika mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN 2024.
Lamlioui alikuwa shujaa wa Morocco mjini Nairobi baada ya kuonyesha kiwango bora katika eneo la kiungo na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya DR Congo uwanjani Nyayo.
“Hakika ilikuwa mechi ngumu, lakini tulikuwa na lengo moja kama timu kutoka uwanjani, kushinda na kuhakikisha tunapata nafasi ya robo fainali. Ninafurahi kupata heshima ya kuwa mchezaji bora, lakini hii ilikuwa jitihada za pamoja za kikosi. Tukiwa na mshikamano tangu mwanzo, tulipata matokeo,” alisema Lamlioui.
Nyota huyo aliongeza kwa kusema: “Tunashukuru kwa hatua hii na sasa macho yote yameelekezwa kwenye robo fainali. Lengo letu ni kucheza mechi kwa mechi na kuendelea hadi fainali.”
Ijumaa ya Agosti 22, Morocco itakabiliana na Taifa Stars katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ambayo inafanyika kwa mara ya nane huku ikiwa ya kwanza kwa ukanda wa Afrika Mashariki. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Taifa Stars kukutana dhidi ya Morocco katika michuano ya CHAN 2024, Morocco imetwaa mara mbili ubingwa wa CHAN 2024 huku Stars ikitinga hatua hii kwa mara ya kwanza. Kwa ujumla katika mashindano yote Morocco na Tanzania zimekutana mara saba, Morocco imeshinda mara sita huku Stars ikishinda mara moja.
Mara ya mwisho timu hizi kukutana ilikuwa Machi 26 mwaka huu katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Dunia na Stars ilipoteza kwa mabao 2-0.