KOCHA wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Molefi Ntseki ametoa ufafanuzi wa mambo yaliyoikwamisha Bafana Bafana kushindwa kufuzu robo fainali ya mashindano ya CHAN baada ya sare ya mabao 3-3 dhidi ya Uganda katika mechi ya kundi C.
Afrika Kusini ilikuwa katika nafasi nzuri ya kutinga hatua hiyo hadi dakika ya 83, ikiwa ikiongoza kwa mabao 3-1 lakini kibao kiligeuka na kulazimisha sare ya mabao 3-3 kwenye Uwanja wa Mandela, Kampala.
“Tulifanya mabadiliko kwa sababu maalumu, na ingawa si kila mchezaji alipewa nafasi ya kuonyesha thamani yake, nina fahari na jitihada za kila mmoja. Tulifunga mabao matatu, lakini mwishowe tulipoteza pointi ambazo kimsingi ziko mikononi mwetu,” alisema Ntseki.
Kocha huyo alionyesha kutoridhishwa na baadhi ya matukio, hasa yale yaliyoamuliwa na VAR, ikiwemo tukio la penalti ya mwisho kwa Uganda ambalo Rodgers Torach alilitumia kufunga bao la tatu dakika ya 90+6.
“Mechi kama hii inaonyesha kuwa soka si takwimu tu ni ujasiri na jitihada za kila mchezaji. Wachezaji wangu walipigana kwa moyo wote na nadhani hiyo inastahili heshima,” aliongeza Ntseki.
Kwa upande mwingine, kocha wa Uganda, Milutin Byekwaso, alionyesha utulivu mkubwa baada ya kukabiliana na ukosoaji kutokana na kupoteza mechi ya kwanza dhidi ya Algeria katika mashindano hayo.
“Nakumbuka mwanzoni mwa mashindano tulipoteza mechi yetu ya kwanza. Ilikuwa wakati wa huzuni, lakini tuliendelea kuamini. Leo, tupo hapa, tumefuzu hatua inayofuata,” alisema Byekwaso.
Byekwaso pia aliweka mkazo kwenye uongozi wa nahodha wa timu yake, ambaye alisimama kuchukua penati muhimu, hatua zilizothibitisha ujasiri wake huku akionyesha vile anaweza kuwajibika kama kiongozi.