Algeria yachekelea kucheza robo Zanzibar 

KOCHA wa timu ya taifa ya wachezaji wa ndani wa Algeria, Madjid Bougherra, amesema safari za mashindano ya CHAN yanayoandaliwa kwa mara ya kwanza na Tanzania, Kenya na Uganda hayajawa changamoto kwao, bali yamekuwa fursa kwa wachezaji.

Baada ya kupata sare tasa dhidi ya Niger katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi, matokeo yaliyowapeleka robo fainali, Bougherra alisema hali ya safari za kwenda Kenya, Uganda na sasa Zanzibar imekuwa chachu ya kuimarisha morali ya kikosi chake.

“Hakuna kilichobadilika kwa sababu ya safari. Kwa kweli ninafurahi kwamba mashindano haya yanafanyika katika nchi tatu. Angalau wachezaji wanapata nafasi ya kusafiri na kuona Kenya, Uganda na Tanzania. Ukiwa sehemu moja kwa muda mrefu unaweza kuzoea na hali ikawa ya kuchosha kwa wachezaji,” alisema Bougherra. Katika mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Niger, kocha huyo alisema mvua ilinyesha na kufanya nyasi za Uwanja wa Nyayo kuwa nzito, lakini hakutaka kutumia hali ya hewa kama kisingizio.

Alisema uwanja ulikuwa mzuri na ingawa ulikuwa mzito kidogo kwa sababu ya mvua na hali ya hewa kuwa baridi zaidi kuliko Kampala, Uganda ambako walicheza mechi tatu za makundi, hakukuwa na mabadiliko yoyote kwenye utendaji wa wachezaji wake.

Kwa mujibu wa Bougherra, lengo la kwanza la Algeria lilikuwa kufuzu hatua ya robo fainali, jambo ambalo sasa limefanikiwa. Alisema sasa wanajiandaa kwa lengo jipya ambalo ni kushinda mechi inayofuata.

Algeria imemaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi C ikiwa na pointi sita nyuma ya Uganda kwa tofauti ya pointi moja.