Shinyanga. Mwili wa mtu mmoja umeopolewa katika mgodi wa Chapakazi na kufikisha idadi ya waliofariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi kwenye mgodi huo kufikia watu watano, huku watatu wakitolewa wakiwa hai.
Agosti 11, 2025, wafanyakazi na mafundi zaidi ya 22 wa mgodi huo walifukiwa kwenye mashimo baada ya kutitia wakati wakifanya ukarabati wa mduara wa mgodi huo.
Juhudi za kuendelea kuwatoa wengine zinaendelea huku ndugu, jamaa na marafiki wakiwa eneo hilo wakiwasubiri wapendwa wao.
Akizungumza na vyombo vya habari leo, Agosti 19, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amethibitisha kutolewa kwa mtu huyu akiwa amekufa huku akisema juhudi za kuwatafuta wengine 17 zinaendelea hadi wapatikane.
Mboni amewataka wananchi kuwa wavumilivu wakati shughuli ya kuwatafuta wengine waliofukiwa kwenye mgodi huo ikiendelea.
“Leo, mtu mmoja ametolewa akiwa amefariki dunia kutoka duara namba 20C na katika duara hilo bado watu saba huku idadi ya waliotolewa wakiwa wamefariki ikifikia watano. Juhudi za kuwatafuta wengine 17 zinaendelea,” amesema Mhita.
Agosti 12, 2025 watu watatu waliokolewa wakiwa hai na kuwahishwa hospitalini kwa huduma ya kwanza, wawili wameruhusiwa lakini mmoja alipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Mwanza kwa matibabu zaidi.
Agosti 13, 2025, mtu mwingine aliokolewa akiwa amejeruhiwa, akapelekwa hospitalini lakini juhudi za madaktari hazikufua dafu kwani alifariki dunia wakati anapatiwa matibabu.
Juhudi za uokoaji ziliendelea ambapo Agosti 15, 2025, mwili wa mtu mmoja uliopolewa na Agosti 16, 2025, watu wengine wawili waligundulika kuwapo eneo la ardhini na Agosti 17, 2025 watu hao wakatolewa wakiwa wamefariki dunia.
Hata hivyo baadhi ya ndugu jamaa na marafiki wa waliofukiwa mgodi akiwemo Ernest Magese na Leticia John ni miongoni mwa wawakilishi wa familia zao walikuwa wakisubiri hatima ya ndugu zao.
“Nina mjomba wangu yuko ardhini leo ni siku ya tisa tangu tukio hili litokee, tunasubiri hatima ya ndugu zetu kwa wakati huu tumejiandaa kwa lolote hadi Serikali itakapoamua mwafaka,” amesema Leticia.
Kwa upande wake Magese, amesema: “Nina kijana wangu mmoja hadi sasa bado hajapatikana ni Mungu tu anatutia nguvu katika kipindi hiki, lakini nitabaki hapa hadi atakapotolewa hata kama akiwa amekufa.”