JACKLINE ISARO ACHUKUA FOMU RASMI KUGOMBEA UDIWANI NGOKOLO

Mgombea Udiwani Mteule Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Ngokolo, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Jackline Isaro, akipokea Fomu za Uteuzi za kugombea nafasi ya Udiwani kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi kata ya Ngokolo Jacob Mwakaluba (kushoto).

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Mgombea Udiwani Mteule Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Ngokolo, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Jackline Isaro, amechukua Fomu za Uteuzi za kugombea nafasi ya Udiwani zilizotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) katika ofisi za kata ya Ngokolo.
Fomu hizo zimetolewa leo Jumanne Agosti 19,2025 na Msimamizi wa Uchaguzi kata ya Ngokolo Jacob Mwakaluba.

Shamra shamra za kuchukua fomu zilianzia katika Ofisi za CCM Kata ya Ngokolo kuelekea ofisi za Kata ya Ngokolo ambapo wanachama wa CCM wakiwemo waendesha bodaboda, vijana na akinamama pamoja na madiwani wateule viti maalum Veronica Masawe na Mwanakhamis Kazoba wamejitokeza kwa wingi kumsindikiza mgombea wao huku shangwe na nderemo zikitawala mwanzo mwisho.

Tukio hilo limeashiria mapokezi makubwa ya kisiasa kwa Isaro na kuonesha nguvu kubwa ya Chama cha Mapinduzi katika kata hiyo.

Jackline Isaro pia amesindikizwa na makada wa CCM kutoka kata jirani ya Ndembezi iliyoanzia kutoka Ngokolo, ambapo makada hao wameongozwa na Mgombea mteule wa udiwani wa kata ya Ndembezi, Pendo Sawa.

Kulia ni Mgombea Udiwani Mteule kata ya Ndembezi Pendo Sawa, katikati ni Mgombea Udiwani Mteule kata ya Ngokolo Jackline Isaro

Hatua hiyo imeonesha mshikamano wa makada wa chama, ishara kwamba CCM imejipanga kwa ushindi wa kishindo kupitia viongozi wake thabiti.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Jackline Isaro amesema sasa kazi imeanza rasmi kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu kuanzia nafasi ya Diwani, Mbunge na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mgombea Udiwani Mteule kata ya Ngokolo Jackline Isaro

“Aliyesimama hapa mbele yenu ni mwanamke mwenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi na kuleta maendeleo katika kata hii. Hii ndiyo sababu Chama cha Mapinduzi kimeniteua. Nawaomba tuungane kwa pamoja kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo,” amesema Isaro.

Aidha, wachambuzi wa siasa za ndani ya Shinyanga wamesema kuungwa mkono na makundi mbalimbali ya wananchi kunampa Isaro taswira ya kiongozi kijana na mwanamke jasiri anayeaminiwa na chama na jamii, hatua inayodhihirisha dhamira ya CCM ya kuendeleza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi wa kisiasa.

Kwa hatua hii, Jackline Isaro ameibuka si tu kama mgombea wa Udiwani, bali pia kama nembo ya matumaini na kiongozi wa kizazi kipya atakayeendelea kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwaletea wananchi maendeleo kupitia utekelezaji wa Ilani ya CCM.