Dar es Salaam. Takribani asilimia 63 ya shule za msingi za serikali nchini zina upungufu wa walimu mwaka 2025, takwimu za Msingi za Elimu (Best 2025) zinaonyesha.
Kwa mujibu wa takwimu hizo jumla ya shule 11,436 kati ya 18,158 za msingi za serikali, mwalimu mmoja anafundisha zaidi ya wanafunzi 45 katika darasa moja jambo linalotilia mashaka ubora wa upatikanaji wa elimu.
Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mwalimu mmoja wa shule ya msingi anatakiwa afundishe darasa lenye wanafunzi 45 kama ilivyoandikwa kwenye nyaraka mbalimbali ikiwemo “mwongozo wa walimu wa kujitolea katika elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vya maendeleo ya wananchi Tanzania bara” 2023.
Wastani wa Taifa, Mwalimu mmoja wa shule ya msingi ya serikali anafundisha angalau wanafunzi 56 badala ya 45 kama mwongozo unavyosema.
Walimu katika mikoa 23 kati ya 27 Tanzania Bara wanakibarua cha kufundisha zaidi ya wanafunzi 45 darasani huku mikoa ya Kilimanjaro, Iringa na Njombe pekee ndio ina uwiano uliopendekezwa.
Mikoa ya Katavi, Simiyu, Geita na Tabora ndio ilikuwa na uwiano hafifu zaidi kwani Mwalimu anafundisha zaidi ya walimu 70 darasani.
Kwa mujibu wa Best 2025, ni asilimia 82.2 pekee ya walimu wanaohitajika ndio walikuwepo katika shule mbalimbali nchini, hali inayofanya baadhi ya maeneo walimu kuendelea kubeba mzigo mkubwa.
Uchambuzi wa mwananchi umebaini shule za msingi za serikali zinahitaji walimu 42,255 zaidi ili kufikia idadi inayohitajika ya 237,981, tofauti na walimu 195,726 waliopo.
Kuajiriwa kwa walimu hao kutafanya angalau mwalimu kuwa na uhakika wa kufundisha wanafunzi wasiozidi 45 kwa darasa, ikilinganishwa na wanafunzi 10,709,153 waliopo kati ya darasa la kwanza hadi la saba.
Ripoti hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), inabainisha kuwa shule 17 nchini mwalimu mmoja anafundisha wastani wa wanafunzi 200 au zaidi, huku shule 975 mwalimu mmoja akifundisha wanafunzi kuanzia 100.
Shule ya Chilinda, iliyopo mkoani Mtwara, ndiyo inayoongoza kwa hali mbaya, kwani takwimu zinaonesha kuwa ina mwalimu mmoja anayelazimika kufundisha wanafunzi 495 waliopo.
Shule hiyo inafuatiwa na ile ya Nyakwi, iliyopo mkoani Kigoma, yenye walimu wawili wanaopambana kufundisha wanafunzi 708. Shule ya Madodomya iliyopo mkoani Songwe nayo ina mwalimu mmoja anayefundisha wanafunzi 336.
Maeneo mengine yenye hali mbaya ni shule za msingi Nyamkombe-Taboa (327), Mwabulugu-Simiyu (325), Msimba Mikumi-Morogoro (316), Kabatinu-Katavi (251), Afya-Geita (245), Mahale-Kigoma (237), Mshiha-Katavi (227), Losirwa-Arusha (224), Sasawala-Ruvuma (219), na Rukoma-Kigoma (214).
Nyingine ni Mwamanyanza, Kombe, Usinga, Ikonda, zote zikiwa mkoani Tabora, zikiwa na wastani wa wanafunzi 210, 209, 202 na 202 mtawalia kwa mwalimu mmoja.
Uchambuzi wa kina unaonesha kuwa mkoa wa Katavi unaongoza nchini kwa kuwa na wastani mkubwa wa wanafunzi kwa kila darasa (77), ukifuatiwa na Simiyu (72), Geita (71), Tabora (71) na Kigoma (69).
Mmoja wa walimu anayefundisha zaidi ya wanafunzi 150 darasani, amesema hali hiyo inaathiri ubora wa ufundishaji na analazimika kutumia nguvu zaidi katika utendaji wake.
“Wanafunzi zaidi ya 100 hadi 200 kwa darasa inaathiri uwezo wangu wa kuwafikia na kuwasaidia wanafunzi wote ipasavyo. Mzigo wa kazi unakuwa mkubwa, hali inayopunguza ufanisi katika kufundisha, kufuatilia maendeleo ya kila mwanafunzi na kutoa msaada unaohitajika kwa wakati,” amesema.
Pia amesema msongamano darasani huathiri mazingira ya kujifunzia, kwa kufanya wanafunzi washindwe kuelewa somo vizuri kutokana na kelele, ukosefu wa vifaa vya kutosha na muda wa kutosha wa maelekezo binafsi kutoka kwa mwalimu.
“Hii inachangia kushuka kwa viwango vya ufaulu na kuongeza pengo la kielimu, hasa katika maeneo ya vijijini na hata mijini pembezoni (Ilala, Dar es Salaam). Kuajiri walimu wapya kutasaidia kuboresha uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi, hivyo kuinua viwango vya elimu na kuongeza ufanisi wa mfumo mzima wa elimu nchini,” amesema mwalimu huyo.
Suala la motisha pia ameligusia, akiitaka Serikali kuwaelimisha wananchi juu ya elimu bila ada, kwani kufanya hivyo kutasaidia kutoa michango.
“Wajue kuwa wana wajibu wa kutoa michango pale inapohitajika ili kuinua ubora wa elimu. Michango midogo iliyowekwa na shule huweza kusaidia katika kuajiri walimu wa muda na hata kutoa motisha kwa walimu walio tayari kutumia muda wa ziada kusaidia wanafunzi waliopata ugumu kuelewa,” amesema.
Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Iringa, Valerius Haule, amesema mbali na ajira kutolewa, ni vyema mazingira ya kazi kwa walimu yakaangaliwa kwa ukaribu, ili kumpa sababu ya kufanya kazi yake katika eneo alilopangiwa.
Amesema shule nyingi zenye ubora zinapatikana katika makao makuu ya kata, vijiji au wilaya, lakini zile za pembezoni zimekuwa haziangaliwi kwa ukaribu, hali inayofanya zikose mazingira rafiki ya kazi.
“Unakuta hata mwalimu anapopangiwa huko, kwa sababu kipaumbele kinachowekwa na Serikali ni mijini, anatafuta namna ya kutoka, ikiwemo kwa kuomba uhamisho au kwenda kusoma na kubadilisha fani,” amesema Haule.
Amesema walipoomba uhamisho mara zote huhamia maeneo ya mijini, ambapo kuna mazingira rafiki, hali inayofanya malalamiko yaendelee kusalia katika maeneo ya vijijini pekee.
“Hata hivyo, ajira zilizotolewa hazijatosheleza kuziba mapengo inavyostahili, hivyo ni vyema zinapotangazwa kipaumbele kiwe shule za msingi kwanza, kwani kuna shule zenye wanafunzi zaidi ya 500, lakini walimu wasiozidi 10,” amesema Haule.
Uhaba huo unaonekana wakati fani ya ualimu ni kati ya zinazoongoza kwa kudahili na kutoa wahitimu wengi kila mwaka. Ripoti ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) inaonesha kuwa mwaka 2024/2025, elimu ilishika nafasi ya pili kwa kuwa na wahitimu wengi.
Ikiwa na wahitimu 13,834, ilitanguliwa na fani ya biashara yenye wahitimu 14,321, huku nafasi ya tatu ikibebwa na sayansi ya jamii (8,216), udaktari na afya (7,568) na sheria (5,008).
Mdau wa Elimu, Nicodemus Shauri, amesema hilio linashuhudiwa wakati wastani wa walimu 5,000 kila mwaka wanaondoka katika ajira kwa kustaafu, kutafuta kazi nyingine au kufariki dunia.
Amesema hali hiyo inaonekana wakati bajeti ya Wizara ya Elimu haikubariki kuajiri hata walimu 5,000 kwa mwaka.
“Suala la uhaba wa walimu linaweza kutatuliwa kwa kuchukua maamuzi magumu, kama ilivyokuwa wakati wa kuhamia Dodoma; bila kufanya hivyo, pengo hili haliwezi kuzibika kwa miaka yote,” amesema.
Amesema walimu wapo wengi mitaani na hata wakisema mshahara utakaolipwa ni Sh300,000, bado wapo watakaotaka kuajiriwa, lakini kipaumbele cha ajira hizo hakijawekwa.
“Ni vyema kuangalia namna ya kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo wazazi, ili kusaidia kupunguza pengo hili,” amesema.
Haya yanasemwa wakati Serikali imeweka dhamira ya kuendelea kuajiri walimu ili kuendana na mahitaji kupitia bajeti ya Wizara ya Elimu ya mwaka 2025/2026, iliyowasilishwa na Waziri Profesa Adolf Mkenda.
“Serikali itaendelea kuandaa na kusambaza mwongozo wa utekelezaji wa kiunzi cha mahitaji na usambazaji wa walimu ili kuimarisha msawazo wa walimu kulingana na mahitaji,” alisema.