Kariakoo Dabi kufungua pazia la Ligi Kuu Bara Septemba 16  

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza kuwa mchezo wa Ngao ya Jamii kufungua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2025/26 utapigwa Septemba 16, 2025 jijini Dar es Salaam.

Katika taarifa iliyotolewa na Shirikisho hilo imesema mchezo huo utawahusisha mabingwa wa Ligi Kuu Bara 2024/25 klabu ya Young Africans dhidi ya mshindi wa pili wa ligi Simba SC.

Taarifa imeeleza kuwa mfumo wa mashindano hayo hauta husisha tena timu nne kama ilivyokuwa msimu uliopita bali timu mbili tu kutokana marekebisho ya kanuni yaliyopitishwa katika kikao kilichopita cha Kamati ya Utendaji ya TFF.

“Mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kuzindua msimu mpya wa mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kati ya Young Africans na Simba itachezwa tarehe 16 Septemba 2025 jijini Dar es Salaam”.

“Mfumo wa mashindano ya Ngao ya Jamii umebadilika kutokana na marekebisho ya Kanuni yaliyopitishwa katika kikao kilichopita cha Kamati ya Utendaji ya TFF”.

“Moja ya marekebisho yaliyofanyika ni katika kanuni hiyo ambapo ikitokea mazingira kama ya sasa ambapo mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) yamebana ratiba za TFF, itachezwa mechi moja tu ya Ngao ya Jamii badala ya tatu ambapo huanzia na nusu fainali mbili na kumalizia na fainali”.

“Tanzania ni mwenyeji wa Fainali za CHAN zilizoanza tarehe 2 Agosti, na zitamalizika Agosti 30 mwaka huu. Pia mwanzoni mwa Septemba timu ya Taifa (Taifa Stars) itacheza mechi mbili za mchujo za Kombe la Dunia, na baada ya Ngao ya Jamii, klabu za Tanzania zitacheza mechi za raundi ya awali ya mashindano ya CAF”.