Morogoro. Licha ya kuenea kwa elimu kuhusu madhara ya kiafya yatokanayo na nishati chafu za kupikia, bado familia nyingi nchini zinaendelea kutumia kuni na mkaa.
Wataalamu wa afya wanasema hatari hizo mara nyingi huchukuliwa kwa wepesi hadi pale mwathirika anapozidiwa, hatua ambayo wakati mwingine huchelewa na kusababisha ugonjwa wa kudumu au hata kifo.
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani katika Hospitali ya Rufaa ya Morogoro, Dk Hadija Bushahu, anasema moshi unaotokana na kuni na mkaa unaleta madhara makubwa zaidi unapovutwa kwa muda mrefu katika maeneo yenye hewa hafifu.
“Hili huweza kuathiri mfumo wa upumuaji, moyo, mishipa ya damu, macho, ngozi na hata mfumo wa uzazi,” anasema.
Dk Bushahu anasema moshi wa kuni na mkaa huzalisha gesi ya kabonimonoksidi ambayo ikivutwa kwa muda mrefu huathiri mapafu. Anasema dalili za awali ni kubanwa mbavu na kushindwa kupumua vizuri, hali inayoweza kuendelea hadi mgonjwa alazimike kuishi kwa msaada wa mitungi ya oksijeni hospitalini au nyumbani.
Anaongeza kuwa moshi huo pia husababisha mishipa ya damu kusinyaa na kuwa migumu, hali inayoweza kusababisha shinikizo la damu.
“Shinikizo hilo lisipotibiwa mapema, mgonjwa anaweza kupata kiharusi, kupooza viungo, kupoteza kumbukumbu na kushindwa kuzungumza,” anasema. Aidha, moyo unaweza kusimama ghafla na kusababisha kifo endapo hatapatiwa matibabu ya haraka.
Akieleza zaidi, Dk Bushahu anasema athari za kiafya zinaweza kugundulika kupitia dalili za kuvimba mwili na kupumua kwa shida. Wagonjwa wengi, anasema, wamekuwa wakifika hospitalini wakiwa hawaamini kabisa kama chanzo cha matatizo yao ni moshi wa kuni na mkaa.
Kwa upande wa uzazi, anatahadharisha kuwa mjamzito anapovuta moshi huo kwa muda mrefu anaweza kujifungua mtoto njiti, mwenye uzito mdogo au mwenye matatizo ya mfumo wa upumuaji.
Vilevile, athari za macho ni kuwashwa, kutokwa na machozi na uwezekano wa kupoteza uwezo wa kuona. Majivu yanayotokana na kuni na mkaa pia huchoma ngozi, kusababisha muwasho na hata saratani.
“Ndani ya moshi wa kuni na mkaa kuna kemikali hatari, ikiwemo Benzine inayosababisha saratani ya damu na Formaldehyde inayoweza kusababisha saratani ya pua na koo,” anaeleza.
Anasema miti inayochomwa kwa ajili ya mkaa hubeba sumu mbalimbali zinazojidhihirisha wakati wa kuchomwa.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani katika Hospitali ya Rufaa ya Morogoro, Dk Hadija Bushahu.
Mbali na athari za moja kwa moja kwa afya, anasema matumizi ya nishati chafu yamekuwa chanzo cha uharibifu wa misitu.
“Misitu inapokosekana, hewa safi ya oksijeni hupungua, mvua hazinyeshi, kilimo hushuka na jamii huingia kwenye matatizo ya njaa, utapiamlo na udumavu,” anasema.
Anabainisha pia kuwa kutafuta kuni na kuchoma mkaa huweka wanawake na watoto kwenye hatari ya ukatili wa kijinsia. “Wanawake wanapokwenda porini hukutana na hatari ya kubakwa au kuuawa. Hata mijini, watoto wanapotumwa kununua mkaa usiku hukutana na watesi wanaoweza kuwadhuru,” anasema.
Kutokana na madhara hayo, anashauri jamii kuachana na mazoea ya kuni na mkaa na kuchagua nishati safi kama gesi na umeme.
Anahoji imani kuwa chakula cha kuni ni kitamu zaidi, akisema hoteli kubwa hutumia gesi na umeme na bado wateja wanavutiwa na vyakula vinavyopikwa humo.
Mbali na maelezo ya kitaalamu, waathirika wanathibitisha madhara ya nishati chafu. Paulo Masunga, mchomaji na muuzaji mkaa kutoka Kijiji cha Mkata, Wilaya ya Kilosa, anakiri kazi hiyo kuwa imemletea athari za kiafya katika nyakati tofauti.
Masunga anasema miongoni mwa athari hizo ni kuugua ugonjwa wa kifua kikuu (TB), ambapo aliugua kwa zaidi ya mwaka mmoja, hata hivyo alipata matibabu na kupona.
Athari nyingine aliyoipata kwenye shughuli zake za kuchoma mkaa ni kujikata na shoka mguuni wakati akipasua magogo.
“Nilipata jeraha kubwa kwenye mguu ambalo lilinifanya nitumie fedha nyingi kujitibu, na mpaka leo hii kuna wakati nasikia maumivu makali kwenye kivu,” anasema Masunga akionyesha kovu lake mguuni.
Naye Mariamu Mgonde, mpishi katika shule ya sekondari Morogoro, anasema kabla shule hiyo haijaingia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia ya gesi na mkaa poa, alikuwa anatumia kuni, ambapo mara kwa mara alikuwa akiugua kifua na macho kutokana na kuvuta moshi mwingi na hivyo kulazimika kushindwa kwenda kazini na kutumia fedha nyingi kujitibu.
“Kuna wakati nilikuwa naletewa kuni mbichi, nyingine zina moshi mkali unaofukuta kwenye macho na pua, hivyo mara kwa mara nilikuwa nabanwa na kifua, nakohoa, mafua hayaniishi.
“ Kila siku nilikuwa mtu wa kunywa dawa za kifua tu, na kwa kweli nikiwa kwenye hali hiyo siwezi kuja kazini maana siwezi kupika huku napiga chafya, ilinibidi nipumzike nyumbani,” anasema Mariamu.
Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati nchini, takribani watu 33,000 hufariki dunia kila mwaka nchini kutokana na magonjwa ya mfumo wa hewa yanayosababishwa na uchafuzi wa hewa majumbani.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.