Kama hujasomea darasani, hakuna kutumia cheo cha udaktari wa heshima

Wizara ya Elimu nchini Ethiopia imepiga marufuku wanaopewa shahada ya heshima ya udaktari kutumia cheo cha daktari nje ya taasisi walizotunukiwa heshima hiyo.

Agizo hilo limetolewa kutokana na malalamiko ya muda mrefu kuhusu matumizi yasiyo rasmi ya vyeo vya kitaaluma, hatua ambayo wizara imesema inalenga kulinda heshima na taaluma ya udaktari wa kitaaluma unaopatikana baada ya masomo ya kina na tafiti za kitaaluma.

“Ni muhimu kutofautisha kati ya shahada ya kitaaluma na shahada ya heshima. Tunataka kulinda heshima ya taaluma na kuondoa mkanganyiko kwa jamii,” imesema wizara hiyo kupitia taarifa yake.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, watu waliotunukiwa shahada za udaktari wa heshima wanaweza kutumia cheo hicho wakiwa ndani ya taasisi zilizowatunuku pekee, lakini si katika nyanja za umma au kazi zao za kila siku.