NAHODHA wa timu ya taifa ya Afrika ya Kati, Cherubin Basse-Zokana ameipongeza Taifa Stars kwa kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) 2024 na kutabiri kuwa inaweza kuing’oa Morocco na kutinga nusu fainali.
Basse-Zokana, ambaye alikuwa mhimili wa kikosi cha Afrika ya Kati katika mechi zote za Kundi B, alisema Tanzania imeonyesha kiwango kizuri na haina sababu ya kuogopa wapinzani wowote hasa inapocheza nyumbani.
“Tanzania ni timu yenye vipaji. Nimecheza dhidi yao na kushuhudia ubora wao uwanjani. Hawajavuka hatua ya makundi kwa bahati, bali kwa uwezo na mpangilio mzuri wa kikosi,” alisema beki huyo wa kati.
Kwa mujibu wa nyota huyo, faida kubwa kwa Stars ni kucheza mbele ya mashabiki wao wenye shauku ya mafanikio, kitu ambacho kinaongeza ari na morali kwa wachezaji kila wanapokuwa dimbani.
“Wana mashabiki bora sana na kwa bahati nzuri nilikuwa nikisikia habari zao muda mrefu hasa zikicheza Simba na Yanga, naamini wanaweza kuhamasika zaidi katika hatua inayofuata. Hili ni jambo la kuzingatiwa kwa kuwa linaweza kuleta tofauti kubwa,” aliongeza.
Stars inatarajiwa kuvaana na Morocco katika robo fainali wikiendi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, mechi inayotarajiwa kuwa ya ushindani mkubwa kutokana na rekodi nzuri ya Waarabu hao katika michuano ya CHAN.
Afrika ya Kati iliaga mashindano mapema baada ya kukwama hatua ya makundi, ikimaliza mkiani mwa Kundi B kwa kujikusanyia pointi moja pekee. Walipoteza michezo mitatu dhidi ya Mauritania (1-0), Madagascar (2-0) na Burkina Faso (4-2).
Licha ya safari yao kufika mwisho, Basse-Zokana alisema uzoefu walioupata ni msingi muhimu kwa maendeleo ya soka la taifa hilo.