NIGERIA imehitimisha safari yake kwenye mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) 2024 kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Congo katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, lakini matokeo hayo hayakuzuia kufungasha virago vyao.
Kocha wa Nigeria, Eric Chelle, alisema ingawa timu yake imetolewa mapema, kiwango walichoonyesha katika mechi hiyo ya mwisho kimeonyesha ubora na heshima ya Super Eagles.
“Tumeonyesha uwezo wetu wa kiufundi, hasa katika sehemu ya mwisho ya mchezo. Ninasikitika kwa sababu tulifanya makosa katika mechi mbili za mwanzo, lakini leo (juzi) tumethibitisha kwamba tunastahili ushindi,” alisema.
Chelle aliongeza kuwa vijana wake walikuwa katika presha kubwa na mara kadhaa walicheza kwa hofu, lakini mechi dhidi ya Congo imeonyesha dhamira yao ya kulinda hadhi ya taifa.
“Sidhani kama vijana wangu wameniburuza. Walijua hatutaki kwenda nyumbani bila pointi. Walicheza kwa heshima na ndiyo maana walipambana hadi mwisho,” alisema kocha huyo.
Akizungumzia changamoto kubwa, Chelle hakusita kueleza ukweli kwamba Nigeria haikuwa tayari kushiriki CHAN kutokana na maandalizi duni.
“Mashindano kama haya yanahitaji maandalizi ya mwaka mzima. Hatujakuwa tayari, hata kisaikolojia. Hata mchezaji Alex aliyekuwa bora katika mchezo huu, nilimuita wiki moja kabla ya kuondoka, na wengi walishangaa. Hii inathibitisha jinsi tulivyokuwa hatuko tayari,” alisema.
Licha ya kuondolewa mapema, Chelle alisisitiza kuwa uzoefu huu utakuwa msingi wa kujenga timu bora ya baadaye. “Pigo kubwa kwetu lilikuwa ni kichapo kizito dhidi ya Sudan, lakini tutalichambua kwa makini na kuhakikisha tunajipanga kwa mashindano yajayo,” alisema.
Kwa upande wa Congo, kocha Barthelemy Ngatsono alikiri kuwa walipoteza kwa timu bora zaidi, akifananisha Nigeria na “simba aliyejeruhiwa.”
“Nilisema kabla ya mchezo kuwa hautakuwa rahisi, na kweli Nigeria si timu rahisi. Walidhibiti mpira vizuri na tulipojaribu kufanya mabadiliko kipindi cha pili, tulikosa umakini. Ndiyo maana tukapoteza,” alisema.
Ngatsono aliongeza kuwa vijana wake walipata mafunzo muhimu licha ya maumivu ya kutolewa. “Wachezaji wetu ni vijana na walikosa maandalizi ya kutosha kabla ya mashindano. Lakini hawakukata tamaa. Hii ni hatua ya kwanza ya safari yao na naamini itawajenga kwa siku za usoni,” alisema.
Matokeo hayo, yameifanya Nigeria kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi D ikiwa na pointi tatu huku Congo ikiburuza mkia, Sudan na Senegal wao wakitinga robo fainali ya michuano hiyo.