Ndugu wa ajali mgodini waishukuru Serikali

Shinyanga. Ikiwa ni siku ya 10 tangu kutokea kwa ajali ya mgodi, baadhi ya ndugu wa wafanyakazi waliokwama chini ya ardhi kutoka familia 17, bado wanaendelea kusubiri kwa matumaini ndugu zao waokolewe wakiwa salama.

Pia, wameeleza namna ambavyo Serikali imekuwa ikitoa huduma muhimu kwao katika kipindi hiki kigumu.

Wakizungumza na Mwananchi leo, Agosti 20, 2025, kwenye eneo la ajali la mgodi unaomilikiwa na Kikundi cha Wachapakazi uliopo katika Kijiji cha Mwongozo, Kata ya Mwenge, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, mkoani Shinyanga, ndugu hao wameeleza kuridhishwa na juhudi za Serikali.

“Tunashukuru Mungu kwa Serikali kuja na hili wazo. Wanatuhudumia vizuri kwa mahitaji muhimu, ikiwemo chakula na malazi. Serikali imetenga sehemu nzuri kwa ajili yetu kulala, tunaoga na kula bila shida,” amesema Robert Jacob, mmoja wa ndugu wa waathirika wa ajali hiyo.

“Kwa namna tunavyohudumiwa sehemu hii kiukweli ni vizuri mahitaji yote muhimu tunapata, katika wakati huu tunasubiri tu ndugu zetu watolewa hata wakiwa hawako hai, tuwasitiri kwa namna ya kibinadamu,” amesema Marco Ndege. 

Agosti 16, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, alitoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dk Kalekwa Kasanga, kuhakikisha anaratibu uwekaji wa ofisi ya muda ya Mtendaji wa Kijiji katika eneo la kulipotokea ajali mgodini hapo.

Lengo la ofisi hiyo ni kusajili wageni waliowasili katika eneo hilo kwa ajili ya kusubiri ndugu zao waliokwama chini ya ardhi, ili waweze kupatiwa huduma muhimu kutoka serikalini kwa utaratibu maalumu.

Pia, Agosti 18, 2025 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita alitoa maelekezo kwa familia zilizokuja kusubiri ndugu zao, kuchagua wawakilishi wawili au watatu ambao watabaki ili iwe rahisi kwa Serikali kuhudumia familia hizo, kwa sababu isingependa kuona watu wanapata changamoto ya mahitaji maalumu wakati tayari wako kwenye huzuni.

Ajali hiyo ilitokea Agosti 11, 2025 wakati maduara ya mgodi huo yakiwa yanafanyiwa ukarabati na kutitia na kufukia watu 25, Agosti 12, 2025 watu watatu waliokolewa wakiwa hai na kuwahishwa Hospitali kupatiwa huduma ya kwanza,  kati yao wawili wameruhusiwa mmoja alipewa rufaa ya kwenda Bugando, Mwanza kwa matibabu zaidi.

Agosti 13, 2025 mtu mmoja aliokolewa akiwa amejeruhiwa alipelekwa hospitalini lakini juhudi za madaktari hazikufua dafu alifariki dunia wakati anapatiwa matibabu, juhudi za kuokoa ziliendelea na Agosti 15 mwili wa mtu mmoja uliopolewa huku Agosti 16, 2025 watu wawili waligundulika walipo eneo la ardhini na Agosti 17, 2025 watu hao watolewa wakiwa wamekufa.

Hadi sasa watu wanane wametolewa huku watatu wakiwa hai na watano wakiwa wamefariki, juhudi za kuendelea kuwatoa wengine 17 zinaendelea kwa kasi kwa kutumia mashine za utambuzi wa ardhini kujua maeneo waliyopo.