Kiungo Sudan bado haamini kilichotokea CHAN 2024

BAADA ya kufanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mchezo dhidi ya Senegal, kiungo mkabaji wa Sudan, Salah Eldin Adil Ahmed Al Hassan amesema haikuwa rahisi kuwazuia mabingwa watetezi, ila juhudi na kufuata maelekezo ndio siri ya kuambulia suluhu.

Salah alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwa sehemu ya ukuta imara wa Sudan ambao ulifanikiwa wa asilimia zote na kuweka wazi kuwa licha ya kufanikisha hilo kwao haikuwa rahisi walihitaji kuhimizana zaidi.

“Ni kweli tuliingia kwa kujilinda zaidi na mpango wetu ulifanikiwa japo haikuwa rahisi kwani tumecheza na mpinzani bora na ndiye bingwa mtetezi ili kufanikisha ilihitajika nguvu ya ziada na maelewano ya hali ya juu,” alisema na kuongeza;

“Nawashukuru wachezaji wenzangu kwa kufanya kazi kwa umoja na kufanikisha jambo kwa kuongoza kundi ambalo lilikuwa gumu likiwa na bingwa mtetezi na tumeweza kufanikiwa kufanya vizuri na kuongoza.”

Alisema mpango haukuwa kujilinda tu na ndio maana mara nyingi walifanikiwa kufika lango la Senegal lakini walikosa umakini kwenye umaliziaji anafikiri hilo kocha kakuona na atalifanyia kazi mchezo unaofuata huku akiweka wazi kuwa mpango wao utakuwa ni ule ule safu ya ulinzi.

“Kazi ya walinzi ni kufanya kazi ya kulinda ukuta wao ili kumpunguzia kazi golikipa hivyo matarajio ni kuendelea kufanya hivyo hatua inayofuata na nafikiri tutafikia malengo ya kucheza fainali.”