Kigoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kigoma, imebaini uwepo wa dosari mbalimbali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika mkoa huo na kutoa maelekezo ili kuboresh a utekelezaji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Takukuru kwa vyombo vya habari Agosti 20, 2025, na Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kigoma, John Mgallah, imeeleza kuwa katika kipindi cha kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu, Taasisi hiyo ilifuatilia utekelezaji wa miradi 10 ya maendeleo yenye thamani zaidi ya Sh3.61 bilioni na kubaini dosari kadhaa katika utekelezaji wa miradi nane ya maendeleo.
Katika miradi ya elimu, Mgallah amebainisha kuwa ujenzi wa nyumba ya mwalimu katika Shule ya Msingi Mahaha, vipimo vya majengo kutoendana na vipimo vilivyopo kwenye ramani pia ujenzi wa Shule ya Sekondari Buhigwe kamati zilizoundwa hazikushirikishwa katika kufanya maamuzi hasa katika ununuzi wa vifaa.
Aidha, katika ujenzi na ukamilishaji wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo Shule ya Sekondari Kirando, Takukuru ilibaini mafundi kutokuwa eneo la mradi hivyo kupelekea baadhi ya miradi kutokamilika kwa wakati.
Pia, katika ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya amali Buhigwe,Takukuru ilibaini vifaa kutoingizwa kwenye madaftari ya kumbukumbu za stoo kwa wakati.
‘’Kutokana na dosari hizo, wasimamizi wa mradi walishauriwa kuhakikisha kamati za utekelezaji wa miradi zinashirikishwa katika kila hatua, aidha msimamizi wa miradi alishauriwa kurekebisha tofauti ya vipimo ambavyo vilitofautiana ili kupata uwiano halisi wa mchoro,’’ amesema Mgallah.
Aidha katika miradi ya ujenzi na uchukuzi, Mgallah ameeleza kuwa ujenzi wa Barabara ya Uswahilini-Sokoni, Juakali Road wilayani Kibondo Mkandarasi alitekeleza mradi bila kuweka alama za tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara ambapo alishauriwa kurudia kuchonga barabara kabla ya kuendelea hatua nyingine.
Pia, ujenzi wa barabara ya Nyakiyobe, Kambiyimigina hadi Nyakavyiru yenye urefu wa kilomita 20, Takukuru ilibaini upana kuwa mdogo ikilinganishwa na mchoro ulivyo na hivyo mkandarasi kushauriwa kuweka alama za tahadhari kabla ya kuendelea na ujenzi.
Katika ujenzi wa vyumba 34 vya biashara katika Soko la Kakonko na ujenzi wa matundu ya vyoo katika masoko ya Mugunzu, Katanga, Gwanumpu na Kikulazo, Takukuru ilibaini uwepo wa nyufa katika baadhi ya kuta na kupasuka kwa sakafu katika baadhi ya maeneo ya kuingilia katika vyoo hivyo.
Kufuatia dosari hizo, mkandarasi alishauriwa kurekebisha kuta pamoja na sakafu zenye nyufa hatua ambayo ilitekelezwa na mkandarasi wa mradi huo.
Katika hatua nyingine, Takukuru ilibaini upotevu wa mapato katika mikopo ya asilimia 10 kutokana na ufuatiliaji hafifu na hivyo kushauriwa kuongeza ufuatiliaji
“Halimashauri zimeshauriwa kuongeza usimamizi ili kuepusha upotevu wa mapato pia kufanya tathmini ya uwezo wa vyanzo vya ukusanyaji wa mapato kabla ya kuviingiza kwenye mpango wa mapato wa mwaka,’’ amesema Mgallah.