Sowah kuikosa Dabi ya Kariakoo Ngao ya Jamii

Mshambuliaji mpya wa Simba, Jonathan Sowah, ataikosa mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga itakayopigwa Septemba 16, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Hii ni baada ya kufungiwa kufuatia kadi nyekundu aliyoonyeshwa kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB msimu uliopita wakati akiwa na Singida Black Stars.

Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara, mchezaji anapopata kadi nyekundu katika michezo ya FA anatakiwa kutumikia adhabu hiyo kwenye mechi zinazofuata za mashindano ya ndani, ikiwemo Ligi Kuu Bara, na pia Ngao ya Jamii.

Hii inamaanisha kwamba Sowah hataruhusiwa kushiriki mchezo huo wa ufunguzi wa msimu mpya.

Sowah alijiunga na Simba katika usajili wa dirisha hili la kiangazi akitokea Singida Black Stars, na amekuwa akihesabiwa kama moja ya silaha mpya za kikosi cha kocha wa Simba, Fadlu Davids kuelekea msimu mpya wa 2025/26.

Kukosekana kwake kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii ni pigo kwa Wekundu wa Msimbazi ambao walihitaji nguvu ya kikosi chao kipya kuonyesha ubora dhidi ya watani wao wa jadi.

Kwa upande mwingine, hii ni nafuu kwa Yanga ambayo sasa itakutana na Simba bila mshambuliaji huyo hatari aliyeonyesha kiwango kizuri msimu uliopita akiwa na Singida kwani alifunga mabao 13 katika mechi 14 alizocheza.

Sowah alijiunga na Singida Black Stars kwenye usajili wa dirisha dogo la Januari 2025 akitokea Al Nasr ya Libya.

Kabla ya kwenda Al Nasr mshambuliaji huyu alikuwa akikipiga kwenye Klabu ya Medeama ya Ghana ambako ndiko alianza kuonekana baada ya timu hiyo kukutana na Yanga katika hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Afrika msimu wa 2023/2024.

Hata hivyo, mashabiki wa Simba watarajie kumuona Sowah akiichezea timu yao mara tu atakapokamilisha adhabu hiyo na kuanza kampeni za Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la CRDB na michuano ya CAF ya msimu ujao wa 2025/2026.