Tarime. Serikali imetoa zaidi ya Sh900 milioni kwa ajili ya kukarabati na kuboresha miundombinu na majengo ya Hospitali ya Mji wa Tarime mkoani Mara kufuatia hospitali hiyo kuzidiwa na idadi ya wagonjwa wanaofika kupata huduma, ikilinganishwa na miundombinu iliyopo.
Hospitali hiyo yenye uwezo wa kupokea na kuhudumia wagonjwa 150 kwa siku hivi sasa inapokea wagonjwa zaidi ya 300 hivyo kuwapa wakati mgumu madaktari na wauguzi kutimiza wajibu wao.
Akitoa taarifa ya mradi huo kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa, Ismail Ussi, leo Jumatano Agosti 20, 2025 Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dk Elias Makima amesema fedha hizo tayari zimeanza kutumika kuboresha miundombinu ya hospitali hiyo utekelezaji ambao umefika asilimia 90.

Dk Makima amesema fedha hizo zinatarajiwa kutumika kukarabati na kuboresha jengo la mama na mtoto na baada ya ukarabati litakuwa na uwezo wa kutoa huduma zote za uzazi kwa wajawazito.
Pia fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kufanya upanuzi wa jengo la kuhifadhia maiti ambalo baada ya ukarabati litakuwa na uwezo wa kuhifadhi miili 24 kutoka miili 12 ya sasa.
Hospitali hiyo ilijengwa mwaka 1952.
“Baada ya ukarabati huu sasa tutakuwa na uwezo wa kuwahudumia wateja wetu bila kikwazo chochote na ukarabati wetu unaelekea ukingoni, tunaishukuru Serikali kwa kuliona tatizo hili na kutoa fedha ili kupata suluhisho la kudumu,” amesema Dk Makima.
Amesema ukarabati huo pia utasaidia hospitali hiyo kuongeza idadi ya vitanda kutoka 150 vya sasa hadi kufika 220 hivyo kukidhi mahitaji ya hospitali hiyo ambayo mbali na kupokea wagonjwa kutoka ndani ya mji wa Tarime, pia imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka wilaya za jirani sambamba na nchi jirani ya Kenya.
“Jengo letu la mochwari lina jokofu moja tu ambalo likiharibika tunalazimika kuhifadhi miili kule Sirari ambapo ni mbali lakini maboresho haya yanahusisha ununuzi wa majokofu mawili mapya na upanuzi wa jengo, hivyo changamoto za sasa zitakuwa zimekwisha,” amesema Dk Makima.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi huo, kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Ismail Ussi amesema ukarabati huo umefanywa na Serikali ikiwa ni kutimiza malengo ya kutatua changamoto za wananchi kwenye sekta ya afya.
Ussi amesema awali huduma za afya zilikuwa zikikumbwa na changamoto nyingi ikiwamo ukosefu wa huduma mbalimbali kama vipimo kutokana na kutokuwepo na vifaatiba vya kutosha katika vituo vya kutolea huduma za afya changamoto ambayo kwa kiasi kikubwa Serikali imeipatia ufumbuzi.
“Mazingira ya vituo yakiwa bora hii sio kwamba ina faida kwa wananchi tu hata madaktari na wauguzi pia wanapata faraja, kwani wanafanya kazi kwenye mazingira mazuri na matibabu yanafanyika kwa wepesi,” amesema Ussi.
Baadhi ya wakazi wa Mji wa Tarime wameipongeza Serikali kwa mradi huo;
“Kuna wakati ukifika pale unakuta mochwari imejaa hivyo unalazimika kusafirisha maiti hadi sehemu nyingine kama kituo cha afya Utegi Rorya au Sirari ili kuhifadhi mwili, kwa kweli huu ni usumbufu mkubwa tunaomba mradi ukamilike haraka ili utunufaishe,” amesema Joseph Marwa
Anna Timothy amesema kukamilika kwa wodi ya wazazi kutaongeza hamasa ya wajawazito kwenda kujifungulia hospitalini hapo.
“Unajua wakati mwingine mtu haoni sababu ya kwenda kujifungulia hospitalini kwa sababu anajua baada ya kujifungua watalala wawili kwenye kitanda kimoja jambo ambalo ni kero, lakini pakiwepo na nafasi ya kutosha kila mama atataka kujifungulia hospitalini kwa usalama wake na mtoto,” amesema Timothy.