Morogoro. Ziara ya Chaumma kusaka wadhamini wa mtiania wa urais wa Tanzania wa chama hicho, Salum Mwalimu imeendelea leo Jumatano Agosti 20, 2025.
Ziara hiyo iliyoongozwa na mtiania mwenza wa kiti hicho, Devotha Minja leo imetokea Morogoro kuelekea Dodoma ikifanya mikutano katika vituo kadhaa njiani.
Akizungumza na wakazi wa Dumila katika safari hiyo, Devotha amesisitiza umuhimu wa Serikali kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji ili kumaliza migogoro hiyo.

Mtiania wa urais wa Tanzania wa Chaumma, Devotha Minja akizungumza na wananchi wa kata ya Magua alipokuwa njiani kuelekea Dodoma katika ziara hiyo ya kusaka wadhamini 200 katika mikoa 10 ya Tanzania kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi nchini.
“Nilipokuwa mwandishi wa habari, niliripoti kuwa kuna matatizo hapa, hadi leo migogoro ya ardhi imeshamiri hapa Morogoro, CCM imekosa mipango ya kuwapa hatimiliki ya ardhi wananchi ili kila mmoja awe na sehemu yake na afuate utaratibu.”
“Tuungeni mkono Chaumma tukaipumzishe CCM, ili tuwape haki ya kumiliki ardhi wakazi wakulima na wafugaji tuondoe tatizo hili,” ameongeza.
Devotha amesema serikali ya Chaumma ikiingia madarakani itatenga maeneo maalumu ya wakulima na wafugaji ili kuondoa msuguano kati ya makundi hayo.
“Tunawahitaji wote wakulima na wafugaji, tunatakiwa kutenga maeneo ya ardhi yenye rutuba kwa ajili ya wakulima na kutenga mapori yenye nyasi nzuri kwa ajili ya wafugaji, amesema.

Mtiania wa urais wa Tanzania wa Chaumma, Devotha Minja akizungumza na wananchi wa kata ya Magua alipokuwa njiani kuelekea Dodoma katika ziara hiyo ya kusaka wadhamini 200 katika mikoa 10 ya Tanzania kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi nchini.
Mtiania mwenza huyo amemwakilisha Mtiania wa urais wa chama hicho, Salum Mwalimu ambaye ametangulia Dodoma kwa ajili ya shughuli zingine za chama kabla ya kuungana naye baadaye mjini Dodoma na kuendelea na ziara.
Mkoani Morogoro, Chaumma imejikita katika kuelezea suluhu ya migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikiripotiwa mara kwa mara katika maeneo kadhaa mkoani humo.
Katika miaka ya hivi karibuni, baada ya jamii za wakulima na wafuaji kuhamia kwa wingi katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo yakiwemo, Kilosa, Mahenge na Kilombero.
Akiwa Mikumi jana Jumanne Agosti 19, 2025, Mtiania wa urais wa Tanzania kwa chama hicho, Salum Mwalimu alitoa ahadi kuwa akishinda uchaguzi wa Jumatano ya Oktoba 29, 2025, atashughulikia tatizo hilo katika siku 100 za kwanza madarakani.