Dar es Salaam. Shirika la Huduma za Elimu la Aga Khan (AKES) kwa kushirikiana na Benki ya DTB limetoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wawili kujiunga na programu ya diploma katika mtalaa wa kimataifa unaofahamika kama International Baccalaureate (IB).
Wanafunzi hao, Munir Athuman kutoka Shule ya Sekondari Istiqama mkoani Tanga na Simin Alladin kutoka sekondari ya Lake jijini Mwanza, wamepata ufadhili huo baada ya kufaulu kwa kiwango cha juu katika mitihani yao ya kidato cha nne na sasa wanajiunga na sekondari ya Aga Khan Mzizima.
Mkurugenzi Mtendaji wa AKES, Dk Shelina Walli, alisema ufadhili huo ni mwendelezo wa dhamira ya shirika hilo ya kukuza vipaji vya kielimu kwa vijana.
Dk Shelina amebainisha kuwa taasisi hiyo imeendelea kuwekeza kwenye maendeleo jumuishi ya wanafunzi, huku ikijikita katika kujenga maadili, uongozi na ufahamu wa kimataifa.
“Shule zetu zinatambulika kwa kutoa elimu jumuishi kwa kuunganisha fikra pevu na misingi ya maadili. Ni jukumu letu kuunga mkono vipaumbele vya kitaifa katika elimu huku tukiwatayarisha wanafunzi kustawi katika mazingira ya ndani na kimataifa,” amesema Dk Shellina.
Kuhusu programu ya IB, amesema inatambulika duniani kote kwa ubora wake katika kuwajenga wanafunzi si tu kielimu, bali pia katika stadi za maisha, uongozi na uwezo wa kufikiri kimkakati.

Munir Athuman (kushoto) akipokea cheti cha ushahidi wa ufadhili wa masomo, anayekabidhi cheti hicho ni mkuu wa shule ya Aga Khan Mzizima Johnson Muniro.
“Kwa kupewa fursa hii, Athuman na Simin wanajiunga na mtandao mpana wa wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali wanaoandaliwa kuwa viongozi wa baadaye wa dunia.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa cheti cha ufadhili huo, Simin amesema:
“Ninashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kusomea IB Diploma. Ufadhili huu utanisaidia katika safari yangu ya kielimu na unanipa hamasa ya kuendelea kujitahidi kwa ubora wa kitaaluma na ukuaji binafsi.”
Kwa upande wake Athuman amesema anataka kutumia fursa hiyo kujiandaa kusomea uhandisi ili siku moja awe miongoni mwa vijana watakaotoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya viwanda nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ofisa Elimu Taaluma -Sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Doreen Massawe ameipongeza AKES kwa hatua hiyo na kuyaomba mashirika mengine kuwa na utaratibu huo wa kutoa ufadhili kwa watoto wa Kitanzania ili wapate elimu bora.
Mzazi mmoja aliyeshuhudia tukio hilo, Said Masoud Said amesema ufadhili huu si msaada kwa wanafunzi pekee bali ni ujumbe kwa jamii nzima.