Mbeya. Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya, Mhashamu Gervas Nyaisonga amekemea tabia ya baadhi ya vijana kutumika kwenye uchaguzi, matukio ya utekaji na mauaji ya watu wasio na hatia.
Mbali na kauli hiyo amewataka vijana kuepuka kujiingiza kwenye biashara haramu, uraibu wa pombe na mmomonyoko wa maadili hususan kuelekea uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya, Mhashamu Gervas Nyaisonga.
Askofu Nyaisonga ametoa kauli hiyo leo Jumatano Agosti 20, 2025 wakati akifungua Kongamano la Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (Viwawa) lililokutanisha watu zaidi ya 4,000 na kufanyika katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki (CUoM) mkoani Mbeya.
Mhashamu Nyaisonga amewataka kuwa na hekima kwa kutenda yaliyo mema na kumpendeza Mungu.
Amesema ufike wakati kustahimili kupambana kwa yanayovuruga amani ambayo haipatikani kirahisi, hivyo ni vyema kuomba hekima ya Mungu ya kushiriki vizuri katika maisha kwa kuepuka kutumika katika matendo yasiyo ya hekima.
“Mwaka huu wa uchaguzi vijana mtatumika mkawe na dhamiri hai daima na mtakaoshirikiana nao muhakikishe wana dhamiri hai pia,” amesema.
Aidha amewataka kutokuwa chanzo cha kuchochea au kushabikia na badala yake watafute hekima za Mungu kwa kutambua jema na baya, sambamba na kujiuliza mko wapi.

Washiriki wa Kongamano la Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (Viwawa) kutoka majimbo mbalimbali ya makanisa Katoliki Tanzania Bara.Picha na Hawa Mathias.
Nyaisonga pia ametumia fursa hiyo kuonya vijana kutoshiriki kwenye dhambi ya mauaji na utekaji kwani hakuna mwenye haki juu ya uhai wa mtu mwingine, huku akisisitiza kusikitishwa mauaji au kuteswa kwa watu wasio na hatia.
“Msishiriki dhambi za mauaji, utekaji ambayo yanahusisha vijana na ninyi vijana wa Kikatoliki ni wafanyakazi na kazi ziko nyingi hujui wanaokwenda kuua, kuteka nyara na kutesa basi kama umetumwa bado unashiriki dhambi mbaya,” amesema.
Katika hatua nyingine amekemea kundi la vijana kutojihusisha na vitendo vya wizi, utapeli, rushwa na ubaguzi katika kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba, ambao utakuwa na vitendo vya hapa na pale sambamba na kuachana na tabia za uvivu.
“Fikirini kwa kujituma, lakini kuna tatizo lingine kwa vijana ni uraibu wa ulevi wa pombe na kuepuka kiburi kwa kujisifu ambako kunapelekea kukosa maarifa na msaada katika jamii,” amesema.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya, Mhashamu Gervas Nyaisonga (katikati) akiwa kwenye maandano ya Kongamano la Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (Viwawa) lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki (CUoM) leo Jumatano Agosti 20,2025. Picha na Hawa Mathias.
Kauli za washiriki onyo la Nyaisonga
Katibu Msaidizi wa Viwawa, Mkoa wa Mtwara, Lulu Jerome amesema kauli ya Askofu Nyaisomba imewapa mwanga kwenda kukemea na kutoa elimu kwa makundi mengine ili kuibua vijana ambao wanaojihusisha na matukio ya mauaji na utekaji yanayoendelea nchini.
“Tunakwenda kutumia ujumbe huu wa Askofu kufikisha maeneo mengine na ndani ya umoja wa makanisa ya Katoliki kwa lengo la kuhakikisha vijana wanajitambua nafasi yao katika kukabiliana na tabia hizo,” amesema.
Boniface Charles kutoka Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Dodoma, amesema kama vijana wamejipanga kikamilifu kupinga rushwa na mmomonyoko wa maadili katika kuelekea uchaguzi mkuu.