Biteko akerwa na kasi ndogo mradi wa umeme Chalinze-Dodoma

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameeleza kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 400 kutoka Chalinze hadi Zuzu Dodoma.

Mradi huo uliopaswa kuwa umefikia asilimia 31 lakini hadi sasa umefikia asilimia 24 tangu kuzinduliwa kwake Novemba mwaka 2024.
Hali ya kusuasua kwa mradi imebainika leo Agosti 20, 2025 katika kijiji cha Manchali wilayani Chamwino ambako  Biteko alitembelea kukagua maendeleo ya mradi huo.


New Content Item (1)

Kufuatia hilo amemuagiza mkandarasi Kampuni ya TBEA ya China kuhakikisha anafidia muda wa kazi uliopotezwa wa asilimia saba ili mradi ukamilike kwa wakati kutokana na umuhimu wake nchini.

Novemba, 2024 Serikali ilikubaliana na mkandarasi kuwa mradi huo ufanyike ndani ya miezi 19 tu badala ya miezi 22 kwa kuwa, wakati mradi unazinduliwa tayari kazi kubwa za awali zilikuwa zimeshafanyika ikiwamo za upembuzi yakinifu na utoaji wa maeneo.

“ Leo ni miezi saba imepita tangu tuzindue mradi sawa na asilimia 32 ya muda wote tuliokuwa tunahitaji kutekeleza mradi huu, na tulitegemea mradi kwa sasa ufikie asilimia 31 lakini katika hali ya kushangaza mradi umefikia asilimia 24 tu jambo ambalo halikubaliki,” amesema Dk Biteko.


Naibu Waziri Mkuu huyo  amesema sababu zilizotolewa na mkandarasi za kuchelewesha mradi ikiwamo ya wananchi kugoma kutoa maeneo kwa madai ya fidia na kukutana na miamba katika mkuza wa mradi, hazikubaliki.

Amesema wananchi wana haki ya kudai fidia na lazima walipwe hivyo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutumia mapato yake ya ndani kulipa fidia wananchi waliopisha mradi.

Biteko amemtaka  mkandarasi kutoutekeleza  mradi huo kwa mazoea kutokana na umuhimu wake kwa kile alichoeleza unahitajika ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati katika Mkoa wa Dodoma.

“Kwa sasa miundombinu inayosafirisha umeme kwenda Dodoma kutoka mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) kupitia Kituo cha Chalinze inabeba umeme kidogo kwa takriban megawati 240 tu ambayo ni sawa na mashine moja tu kati ya mashine tisa za JNHPP, hivyo njia hiyo mpya ya umeme ya kV 400 inayojengwa ni muhimu,”amesema Biteko.

Amesisitiza kuwa njia mpya ya umeme ya kV 400 ni muhimu kwa kuwa, katika Mkoa wa Dodoma mahitaji ya umeme yanaongeka kila siku huku mkoa huo pia ukiwa ni kitovu cha usambazaji umeme katika mikoa yote ya Magharibi.

“Singida, Tabora, Shinyanga Mara na Kigoma  inayotegemea utulivu wa umeme katika mkoa wa huo na kwamba Rais, Samia alishaagiza kuwa mradi huo usichezewe hivyo mkandarasi ahakikishe kuwa anaupa umakini mkubwa,”amesema.

Pia, amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, kutengeneza timu itakayoungana na Tanesco kuusimamia mradi huo na kila wiki taarifa itolewe kuwa umefikia wapi.

Katika hatua nyingine, Dk Biteko amewaasa wananchi kutozuia utekelezaji wa miradi pale inapopita kwenye maeneo yao na Serikali kwa upande wake itahakikisha kuwa wanapata haki wanazostahili.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema mradi huo wa usafirishaji umeme wa kV 400 unaenda kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha usambazaji umeme nchini.
Rosemary ameahidi kuyasimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Dk Biteko ya kuhakikisha kuwa, mradi huo unakamilika kwa wakati ili kuwezesha umeme huo utakaofikishwa Dodoma, kusambazwa pia kwenye maeneo mengine nchini.

Akitoa taarifa ya utekelezaji Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco , Lazaro Twange amesema mradi huo unakusudia kusafirisha umeme wote unaozalishwa kutoka katika Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (Megawati 2,115) na kuingiza kwenye gridi ya Taifa kisha kuufikisha kwenye maeneo yote yenye mahitaji ya umeme.

Amesema mkataba na mkandarasi wa Kampuni ya TBEA ulisainiwa mwaka 2024 na mradi kuanza kutekelezwa Novemba 2024 na mkandarasi ameshalipwa awamu ya kwanza ya malipo ambayo ni Sh107 bilioni na mhandisi mshauri ameshalipwa asilimia 15 ya malipo yake.


Ameeleza kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati yatafanyiwa kazi ikiwamo ya kuhakikisha mradi unakamilika Juni au kabla ya Juni 2026 kwa mujibu wa mkataba.

Mradi huo utakaogharimu Sh513 bilioni utakuwa na urefu wa kilometa 345 na kuhusisha minara ya umeme ipatayo 917 kutoka Chalinze mkoani Pwani hadi Zuzu mkoani Dodoma.