Hiki hapa chanzo wanafunzi kuacha shule

Dar es Salaam. Mwanafunzi mmoja kati ya 24 wa shule za msingi nchini amechelewa kuanza shule, kwa mujibu wa takwimu mpya za umri wa wanafunzi hao mwaka 2025.

Wadau wanasema, watoto wanaoanza shule kwa kuchelewa hukumbana na changamoto mbalimbali za kifikra na kihisia kwani wanakuwa na tofauti ya kimakuzi na rika lao darasani.

Hii inaweza kuathiri uwezo wao wa kujifunza, kushirikiana kijamii na kujiamini, huku hali hii ikiwaongezea uwezekano wa kushindwa kumaliza masomo, hali inayochangia kiwango kikubwa cha uachaji shule kwa wanafunzi.

Hayo yanaelezwa na wadau mbalimbali, wakati ambao wanafunzi 443,805 wa shule ya msingi wa ngazi tofauti nchini katika mwaka 2025 wakibainika kuwa na umri wa zaidi ya miaka 13. Hii ni kati ya wanafunzi milioni 10.71 waliokuwepo.

Ripoti ya Takwimu za Msingi (BEST 2025) inayotolewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Ofisi ya Rais – Tamisemi) ilionesha mikoa yenye wanafunzi wakubwa ni Mwanza ikiwa na asilimia 4.8, Kigoma asilimia 4.7, huku Geita, Dodoma, Kagera na Mara zikiwa na asilimia 4.6 kila moja.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, mikoa hii inaongoza pia kwa wanafunzi kuacha shule. Geita ndiyo kinara kwa wanafunzi 19,262 walioacha shule ya msingi mwaka 2024, ikifuatwa na mikoa ya Mwanza, Tabora, Kagera, Simiyu na Dodoma. Je, umri mkubwa unachangia?

Kwa mujibu wa kifungu cha 35(1) cha Sheria ya Taifa ya Elimu ya Mwaka 1978, kama ilivyofanyiwa marekebisho, kila mtoto aliyefikisha miaka saba na ambaye hajazidi miaka 13 ni lazima aandikishwe darasa la kwanza. Huku kifungu cha 35(2) kikimpa mzazi wa mtoto aliyeandikishwa shule ya msingi jukumu la kuhakikisha mtoto anakwenda shule ipasavyo na anamaliza elimu ya msingi.

Kuchelewa kuanza shule kunatajwa kuwa na sababu kadhaa, ikiwemo umbali wa shule husika na hata mwamko wa wazazi kupeleka watoto shule.

“Kuna baadhi ya maeneo, jiografia ni kikwazo kupeleka watoto. Wanalazimika kutembea umbali mrefu, wavuke mito, misitu. Mzazi anaona hana muda wa kumpeleka mtoto kila siku, hivyo ni vyema asubiri,” amesema Said Said, mdau wa elimu.

Amesema, hali hiyo imefanya watoto wengi hasa wa vijijini kutomaliza masomo yao, ambapo wavulana wanalazimika kuingia katika shughuli za kiuchumi, huku wale wa kike wakipata ujauzito kabla ya kumaliza masomo.

“Pia, umaskini unafanya vijana waamue kuingia katika shughuli za uzalishaji ili wawasaidie kulea familia, na hii inatokana na wazazi wao kukosa mwamko wa elimu. Shule zikisogezwa karibu na makazi zaidi, watoto watasoma kwa wakati wakiwa na umri mdogo kabla akili zao hazijaanza kuwaza fedha na kupitia vishawishi,” amesema Said.

Kuhusu ujenzi wa shule aliozungumzia, katika bajeti ya Tamisemi mwaka 2025/2026, Sh1.44 trilioni za ruzuku ya matumizi mengineyo, fedha za maendeleo za Serikali Kuu na washirika wa maendeleo zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli katika sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa shule.

“Miongoni mwa yatakayofanyika ni ujenzi wa madarasa 8,402, kati ya hayo 8,057 ni shule za msingi na 345 ni sekondari, matundu ya vyoo 19,095, umaliziaji wa maboma ya maabara 350, mabweni 129 kwenye shule za sekondari na maboma ya madarasa 700 shule za msingi,” alisema Waziri wa Tamisemi, Mohammed Mchengerwa alipowasilisha bajeti bungeni jijini Dodoma.

Kuchelewa kuanza shule hakuathiri tu ujifunzaji wa mtoto, bali pia kuna athari za moja kwa moja katika ukuaji wa uchumi wa mtu na Taifa kwa ujumla.

Akizungumzia suala hilo, Mtaalamu wa Uchumi, Andambike Kyombo amesema kuchelewesha watoto shule kunawafanya washindwe kufanya kazi katika umri sahihi wa uzalishaji, kwani mara nyingi watu wenye nguvu ni kati ya miaka 18 hadi 45.

Umri huo ndiyo huwafanya kuwa na nguvu ya kufanya uzalishaji, lakini badala yake wao ndiyo watakuwa wakiwa ngazi mbalimbali za elimu, ikiwemo vyuo au wakisomea fani mbalimbali.

Si tu kumaliza masomo, pia hali hiyo huwachelewesha kuingia kwenye soko la ajira, hivyo kupunguza muda wa uzalishaji na ufanisi katika maisha yao ya kikazi. Hali hiyo huathiri ukuaji wa Pato la Taifa, kwani huchelewesha upatikanaji wa rasilimali watu wenye ujuzi na nguvu za kutosha.

“Mtoto akianza shule mapema ataingia katika uzalishaji mapema na si kukimbizana na muda kwa sababu anakuwa katika kipindi ambacho hakupaswa kuwepo, na matokeo yake wakija kwenye ajira wanatumia muda mfupi tofauti na matarajio,” amesema Kyombo.

Hilo pia huathiri hata uzalishaji wa nguvu kazi kupitia kiwango cha kuzaa, hususani kwa wanawake ambao mara nyingi huwa na ukomo wa kuweza kushika ujauzito.

Amesema, ikiwa wanachelewa kuanza masomo husogeza pia umri wa wao kupata watoto wa kwanza, hali inayopunguza uwezo wa wao kupata watoto wengi, ikilinganishwa na kama wangeanza kuzaa mapema.

“Unakuta mtu ambaye huenda angekuwa na uwezo wa kuzaa watoto saba kama angeanza kuzaa akiwa na miaka 25, lakini anashindwa kuwapata kwa sababu alianza kuzaa akiwa na miaka 35, hivyo anaishia kupata watoto watatu hadi wanne,” amesema.

Amesema, jambo hilo linapunguza uwezo waTtaifa kupata nguvu kazi ambayo ingeweza kumudu kufanya baadhi ya shughuli za uzalishaji, kwa sababu kiwango cha kuzaliana kimepungua.

“Hii inafanya kile kilichopaswa kuzalishwa na nguvu kazi hiyo kutopatikana kwa kiwango kinachotakiwa,” amesema.

Kuhusu umri mkubwa kuwa kichocheo cha wanafunzi kuacha shule kwa kudhani wanapoteza muda, huenda likawa lina ukweli ndani yake, kwani mikoa inayoongoza kwa kuchelewesha watoto shule, baadhi yake imo katika orodha ya kuwa na wanafunzi wengi wanaoacha shule.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa mikoa ya Geita na Mwanza pia ni miongoni mwa mikoa minne nchini inayoongoza kwa watoto kuacha shule, ikiungana na Kagera na Tabora.

Mikoa hiyo minne, kwa ngazi ya elimu ya msingi, inabeba asilimia 44.7 ya wanafunzi wote walioacha masomo kwa mwaka 2024, na asilimia 28.98 ya wanafunzi wote walioacha masomo ngazi ya sekondari mwaka 2024.