Polisi Mbeya yawashikilia tisa utapeli mtandaoni Facebook, WhatsApp

Mbeya. Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu tisa kwa tuhuma za utapeli wa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ikiwepo kupitia mitandao ya kijamii ya Facebook na WhatsApp.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema leo Jumatano, Agosti 20, 2025 watuhumiwa hao wamekamatwa katika msako wa Polisi uliofanywa Mamlaka ya Mji wa Mbalizi na Kata za Iyunga na Nzovwe.

Amesema Agosti 18, 2025 saa 6.00 mchana katika Kata ya Nsalaga, Tarafa ya Usongwe mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi waliwakamatwa watu wanne wanao jihusisha na utapeli wa fedha kutumia simu za mkononi na mitandao ya kijamii ya Facebook na WhatsApp.

Amesema kupitia mitandao ya kijamii watuhumiwa walikuwa wakitumia mbinu ya kudanganya wanatafuta wafanyakazi wa kuuza ‘super market’ yenye jina la Kajala iliyopo jijini Dar es Salaam.

Amewataja watuhumiwa hao ni Nehemia Njonga (23) fundi rangi, Ombeni Ambilikile (22), dereva bodaboda, Jacob Hamis (23), fundi rangi, Mkazi wa Mwakapangala.

Wengine ni Baraka Mgala (22), dereva bodaboda, mkazi Mamlaka ya Mji wa Mbalizi Wilaya ya Mbeya ambao wote walikamatwa katika doria iliyofanywa na Polisi Agosti 18, 2025.

Amesema watuhumiwa hao walikuwa wakigushi kiunganishi cha mitandao ya kijamii Facebook na WhatsApp (link) kwa watu wanaomba ajira.

Kuzaga amesema baada ya kujiunga hutumiwa ujumbe wa kuwataka kutuma wasifu wao ‘CV’ na fedha za kujazwa taarifa zao kwenye fomu sambamba na kulipia gharama za sare za kufanyia kazi.

“Watuhumiwa baada ya kupekuliwa wamekutwa na simu mbalimbali pamoja na laini ambazo hutumika kupokea fedha na kufanyia mawasiliano kwa watu wanao tapeliwa,” amesema.

Katika tukio lingine, Agosti 18, 2025 saa 12.00 jioni katika Mtaa wa Mapelele Polisi wakiwa doria waliwakamata watu watatu kwa tuhuma za utapeli na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Watuhumiwa hao ni Lusajo Jeremia (45), Adili Mbeyale (19), na Shaban Thabiti (23) wakiwa na simu tano za mkononi na laini 20

Imeelezwa laini hizo za mitandao tofauti walikuwa wakitumia kufanya udanganyifu wa fedha zikiwepo ujumbe mfupi wa maneno wa ‘tuma kwa namba hii.

Wakati huohuo, Ester Kimaro (28) na Abdi Awadhi (21) wote wafanyabiashara wakazi wa Kata za Nzovwe na Iyunga wanashikiliwa kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Watuhumiwa hao wamedaiwa kuwarubuni watu mbalimbali ili waungwe kuwa wamiliki wa Kampuni ya Q NET yenye makao makuu nchini Malaysia.

Kutokana na taarifa hiyo ya Polisi, Mkazi wa Nzovwe, Solomon Nick amesema Jeshi la Polisi linapaswa kufanya uchunguzi wa kina kwa watuhumiwa kutonana na kukithiri kwa matukio ya utapeli mtandaoni.

“Laini ya simu ni siri ya kampuni za simu na mteja sasa tunashindwa kuelewa hao matapeli wanapata wapi namba za watu na kufanya utapeli,” amesema.