Dar es Salaam. Wafanyakazi, ndugu na jamaa wa aliyekuwa Mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Sharon Sauwa wamemwelezea kama mtu aliyekuwa na bidii, upendo na mshauri kwa watu wote waliomzunguka.
Sharon alifariki dunia alfajiri ya jana (juzi), akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili – Mloganzila.
Alijiunga na MCL Agosti 2013, akitokea kampuni ya The Guardian Limited, na alihudumu kwa kipindi chote akiwa kituo cha Dodoma.
Waliomfahamu wanasema aliitumikia tasnia ya habari kwa weledi, moyo na kujituma kwa kiwango cha juu pamoja na changamoto kadhaa zinazoikumba tasnia hiyo.

Wafanyakazi, ndugu na jamaa wa aliyekuwa Mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Sharon Sauwa wakiwa wakiwa msibani Pugu jijini Dar es Salaam leo Agosti 20, 2025. Picha na Pelagia Daniel
Akizungumza nyumbani kwao Pugu Mwakanga jijini Dar es Salaam, Mwanasiasa mkongwe nchini Joseph Selasini amesema Sharon alikuwa mtu muhimu ndani ya familia, mwenye huruma na mshauri kwa wengi.
“Msiba huu umetufika kwa ghafla, lakini tunapaswa kumshukuru Mungu. Yeye ni Baba wa wote na siku yetu itafika kwa namna tofauti kwa kuugua, kwa ajali au vinginevyo,” amesema Selasini ambaye pia ni jirani wa familia ya Sharon.

Mhariri Mwandamizi wa Gazeti la Mwananchi, Lilian Timbuka akiwa msibani kwa Mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Sharon Sauwa leo Agosti 20, 2025. Picha na Pelagia Daniel
Selasini ameongeza kuwa pamoja na majonzi waliyonayo, wamepata faraja kuona jinsi wafanyakazi wenzake walivyoshiriki kuwafariji.
“Sharon alikuwa wa kwenu zaidi hata kuliko kwetu nyumbani, alirudi akiwa amechoka, kesho yake anarudi kazini. Pole sana kwa hili pigo,” ameongeza.
Amesisitiza kuwa waandishi wa habari hufanya kazi katika mazingira magumu na changamoto nyingi. “Nawapa pole kutoka moyoni, nafahamu ugumu wa maisha na kazi hii. Ni Mungu tu awe faraja yenu, kwani kazi mnayofanya ni wito.”
Pia ametoa wito kwa Serikali na jamii kutambua mchango wa wanahabari, akipendekeza tasnia hiyo iwe sehemu ya Katiba kama njia ya kushughulikia changamoto wanazopitia.
“Waandishi mnaelimisha, mnaburudisha na mnatoa taarifa muhimu, mnahitaji kutazamwa kwa jicho pana zaidi,” amesisitiza.
Amesema kwamba alianza kufanya kazi na Sharon kama mwanasiasa tangu akiwa katika gazeti la Alasiri mpaka anapofika katika magazeti ya Mwananchi.
Kwa upande wake, Lilian Timbuka, mmoja wa wahariri wa Gazeti la Mwananchi, amesema alimfahamu Sharon kwa zaidi ya miaka 20, tangu akiwa kwenye vyombo vingine vya habari kabla ya kujiunga na MCL.
“Alikuwa jembe kweli. Alikuwa mwepesi wa kazi, mshauri na mtu wa ushirikiano mkubwa,” amesema.

Wafanyakazi, ndugu na jamaa wa aliyekuwa Mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Sharon Sauwa wakiwa wakiwa msibani Pugu jijini Dar es Salaam leo Agosti 20, 2025. Picha na Pelagia Daniel
Aliongeza kuwa Sharon hakuwa mtu wa kuchoka. “Hata ukimwamsha alfajiri kwa habari, alinyanyuka na kurudi na taarifa iliyokamilika,” amesema na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kumwombea Sharon na kumsaidia mtoto wake ambaye bado yuko shule.
Ruth Liana, mfanyakazi mwenzake, amesema Sharon alikuwa na uchapakazi wa hali ya juu, alikuwa mcheshi na alipenda kushirikiana na jamii hata nje ya mazingira ya kazi. “Tutamkumbuka kwa moyo wake wa upendo na msaada kwa wengine,” amesema.
Steven Lamlembe Sauwa, baba mzazi wa marehemu, amesema mwili wa Sharon ulitarajiwa kuwasili nyumbani jana jioni na kulala hadi asubuhi.

Wafanyakazi, ndugu na jamaa wa aliyekuwa Mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Sharon Sauwa wakiwa wakiwa msibani Pugu jijini Dar es Salaam leo Agosti 20, 2025. Picha na Pelagia Daniel
Amesema baada ya kifungua kinywa na chakula, wataanza kuaga mwili kuanzia saa tano asubuhi kabla ya kuelekea Kanisa Katoliki la Mtakatifu Francis Pugu kwa misa ya mazishi.
Baadaye, mwili ulitarajiwa kuzikwa kwenye shamba lililopo karibu na nyumbani kwao, Pugu Mwakanga.