Wananchi wataja miaka 20 ya kupunguza vifo vya mama mtoto Nzega

Nzega. Shirika la World Vision Tanzania limetimiza miaka 20 ya kutoa huduma za afya kwa watoto na jamii wilayani Nzega, mkoani Tabora, likielezwa kuwa chachu ya kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kuimarisha ustawi wa familia.

Kwa muda wote huo shirika imetekeleza miradi ya afya ya mama na mtoto, lishe, maji na usafi wa mazingira safi na elimu ya afya shuleni, hatua ambayo imepunguza magonjwa ya mlipuko katika jamii.

Hayo yameelezwa leo  Jumatano Agosti 20, 2025 katika Kijiji cha Upungu, Wilaya ya Nzega katika hafla ya makabidhiano ya miradi ya maendeleo ya jamii iliyotekelezwa kwa miaka 20 katika Mradi wa Mpango wa Maendeleo ya Jamii Ndala (NdalaAP) unaojumisha kata tatu za Ndala, Puge na Nkiniziwa zenye vijiji 11 katika wilaya hiyo.

Mary John ni mkazi wa Kijiji cha Nkiniziwa wilayani humo amesema kuwa miradi ya shirika hilo imesaidia kupunguza umbali wa kutafuta huduma za afya, kuboresha maisha ya watoto kwa kuwapatia vyakula vyenye virutubisho na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu lishe na usafi wa mazingira.

Mwanafunzi Zawadi Israel wa Shule ya Msingi Puge amesema kuwa katika kuahakikisha wanakuwa na lishe bora shirika hilo limekuwa likitoa mbegu za viazi lishe katika kila shule na kuhakikisha wanapata chakula wanapokuwa shuleni.

“Hizi mbegu za viazi lishe zimekuwa zikiletwa shuleni na sisi tunazilima na hatimaye tunaopata chakula shuleni chenye lishe bora kwa ajili ya afya zetu sisi wanafunzi,” amesema.

Bertha John mkazi wa Kijiji cha Nkiniziwa amesema kuwa kujengwa kwa zahanati katika kijiji hicho kumesaidia wakinamama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kupata huduma za afya.

“Tumejengewa zahanati katika kijiji chetu sasa hatutembei umbali mrefu kama ilivyokuwa awali kufuata huduma za afya  katika vijiji jirani hasa ya akinamama wajawazito pamoja na watoto chini ya miaka mitano,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Sauda Mtondoo ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, akizungumza katika makabidhiano hayo amesema kuwa mchango wa World Vision umeleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya afya ya msingi.

“Wanawake wajawazito wamepatiwa elimu ya afya ya uzazi na kaya nyingi sasa zinapata maji safi na salama pia watoto wengi wamefikiwa katika mradi huu katika masuala ya afya na lishe. Haya ni mafanikio makubwa kwa wilaya yetu.

“Serikali itaendelea kusimamia na kulinda miradi yote iliyoachwa na World Vision ili iwe endelevu na kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu zaidi,” amesema.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa World Vision Tanzania, Simon Moikan amesema kuwa shirika hilo limekuwa likifanya kazi kwa kushirikiana na Serikali za vijiji na halmashauri ya wilaya ya Nzega ili kuhakikisha huduma zinabaki endelevu.

“Tunajivunia kuwa sehemu ya safari hii ya miaka 20. Lengo letu ni kuona kila mtoto anafurahia maisha ya afya njema, anapata lishe bora na fursa ya kujifunza hivyo kwa miradi ambayo tumeiacha ni vizuri ikaendelezwa katika eneo hili la Ndala na katika miradi yetu tumewafikia zaidi ya watoto 86,000,” amesema.

Shirika hilo limewataka wananchi kutunza na kuendeleza miundombinu hiyo kwa manufaa ya vizazi vijavyo, likisema lengo lake kuu ni kuikomboa jamii ya Ndala na maeneo jirani kutokana na changamoto za kimaendeleo.

Kwa sasa, World Vision inaendelea kutekeleza miradi mipya katika eneo hilo ya ukuzaji wa kipato cha kaya kupitia kilimo, mifugo na vikundi vya kuweka na kukopa pamoja na mnyororo wa thamani.