Mwendokasi Mbagala kuanza Septemba mosi

Dar es Salaam. Hatimaye kiu ya muda mrefu ya wakazi wa Mbagala inakwenda kupata ahueni baada Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) kusema huduma ya mabasi ya ‘Mwendokasi’ kwa Barabara ya Kilwa itaanza siku kumi zijazo yaani Septemba mosi mwaka huu.

Mradi huo wa awamu ya pili wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) unaanza kutoa huduma baada ya mabasi yaliyokuwa yakisubiriwa kuwasili chini ya mwekezaji mzawa, Kampuni ya Mofat aliyepewa dhabuni ya kusimamia utoaji huduma hiyo.

Uzinduzi huo uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu unatarajiwa kuwa mkombozi kwa wakazi wa Mbagala na maeneo ya jirani ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za usafiri kwa miaka mingi na sasa wataona ahueni baada ya njia hiyo yenye urefu wa kilomita 20.3 kutoka katikati ya jiji kuanza kupata huduma hiyo.

Ujenzi wa awamu hiyo ulikamilika mwaka 2023, lakini utoaji wa huduma uliahirishwa mara kadhaa kutokana na kuchelewa kufikishwa kwa mabasi na miundombinu inayosaidia huduma hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Dart, Dk Athumani Kihamia ameliambia gazeti dada la The Citizen leo Jumatano, Agosti 20, 2025, kuwa mabasi 99 yanatarajiwa kukamilisha taratibu katika Bandari ya Dar es Salaam kesho Alhamisi huku waendeshaji wakikamilisha taratibu za kodi ili kuruhusu usambazaji wa haraka.


“Tuna matarajio kwamba Kampuni ya Lake Energies itakabidhi kituo cha kujazia gesi asilia (CNG) kwa Dart wiki ijayo kwa ajili ya ukaguzi wa mwisho. Ujenzi unaendelea vizuri na huduma zitaanza kama ilivyopangwa,” amesema wakati wa ziara ya ukaguzi katika Kituo cha Kivukoni, Depo ya Mbagala na bandari akiwa na bodi ya wakurugenzi ya Dart.

Dk Kihamia amebainisha hadi sasa kadi milioni moja za kielektroniki zimeagizwa kwa ajili ya abiria huku mageti ya kielektroniki ya tiketi yaliyoagizwa kutoka Uingereza na China yakitarajiwa kuwasili ndani ya mwezi huu.

Amesisitiza hata kama kutakuwa na ucheleweshaji wa vifaa vingine, huduma zitaanza kama ilivyopangwa:“Changamoto pekee inayoweza kuchelewesha uzinduzi ni iwapo waendeshaji watashindwa kukamilisha taratibu za kupokea mabasi bandarini. Vinginevyo, tuko tayari.”

Kuhusu nauli za mabasi, Dk Kihamia amesema ni jukumu la Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (Latra) kutangaza viwango rasmi vya nauli, kufuatia maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Ametumia nafasi hiyo kuonya taasisi na watu binafsi wanaoomba vibali vya kutumia njia za BRT, akisisitiza ni mabasi pekee yatakayopewa ruhusa:“Tumekuwa tukipokea maombi ya aina hiyo, lakini Dart haitatoa vibali. Dharura zinapaswa kushughulikiwa kwa mipango sahihi.”

Awamu ya Pili ya BRT imepangwa kuendeshwa kwa kutumia jumla ya mabasi 755, ambayo yatawasili kwa awamu. Mbali na mabasi 99 yaliyopo bandarini sasa, mengine 51 yanatarajiwa kuwasili kati ya Agosti 25 na 27.

Mwenyekiti wa Bodi ya Dart, Dk Florence Turuka ameonesha kuridhishwa kwake na maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa.

“Tumevutiwa na kile tulichokiona mabasi bandarini, ujenzi wa kituo cha Kivukoni na maendeleo ya kituo cha kujazia gesi cha Mbagala. Ujumbe wetu ni mmoja, huduma lazima zianze Septemba Mosi na kila kitu kiwe tayari,”amesema Dk Turuka.

Mapema mwezi huu, Serikali ilithibitisha kupokea sehemu ya kwanza ya mabasi ya BRT 99 yaliyotengenezwa na Kampuni ya Golden Dragon nchini China, huku mengine 101 yakitarajiwa kufikishwa ifikapo katikati ya Agosti.

Mabasi hayo yenye urefu wa mita 18 yanatarajiwa kupunguza msongamano na muda wa kusafiri kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam kwenda maeneo ya Mbagala.

Katika maandalizi ya uzinduzi, Kampuni ya Mofat Company Limited, moja ya waendeshaji waliopewa kandarasi imetangaza ajira.

Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa kampuni hiyo, Mabrouk Masasi aliiambia The Citizen  Juni, 2025 kuwa nafasi zaidi ya 423 zilitangazwa ikiwa ni pamoja na madereva 255 na wasaidizi wa vituo 158.

“Hii ni mwanzo tu. Mara mabasi yatakapowasili ajira zaidi zitatangazwa, jumla ya wafanyakazi wanaohitajika watafikia takribani 1,100,” alisema.

Haya yanaelezwa ikiwa ni siku chache tangu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutembelea na kukagua miundombinu ya mradi huo Agosti 13, 2025 na kuagiza kazi iliyosalia ikamilishwe ili huduma hiyo ianze kutolewa mwezi huu.

Akiwa katika ziara yake, Majaliwa aliwaagiza waendeshaji wa awamu ya pili ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT-2) kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha maeneo yaliyobaki yatakayowezesha mradi huo kuanza kutoa huduma ndani ya muda mfupi.

“Tunataka mradi huu uanze kutoa huduma kwa Watanzania hasa wakazi wa Dar es salaam, mradi huu utaongeza ufanisi wa usafiri wa umma katika jijini la Dar es Salaam na kutoa huduma ya kisasa, salama na ya haraka kwa wananchi,” alisema.

Majaliwa pia alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya utoaji huduma ya Usafiri ya Mofat, Mohammad Kassim kuhakikisha anakamilisha haraka taratibu za utoaji wa mabasi 99 yaliyopo bandarini ili kuwezesha huduma hiyo kuanza kwa wakati.

Majaliwa alisema Serikali inataka kuona katika awamu ya pili ya mradi wa BRT, tiketi za usafiri kupitia mabasi hayo zinakuwa za kielektoniki badala ya tiketi za karatasi kama ilivyokuwa awali. “Tukifanya hivi itatusaidia kumonitor kiasi cha fedha kinachokusanywa.”