Devotha aahidi ubwabwa kwa wote Chaumma ikiingia Ikulu

Morogoro. Katika harakati za kushawishi wadhamini kwa mtiania wa urais wa Tanzania wa Chaumma, Salum Mwalimu, mtiania mwenza wake, Devotha Minja ameahidi kuboresha lishe nchini.

Makamu huyo wa Mwenyekiti wa Chaumma Taifa, Hashim Rungwe upande wa Bara, amesema msimamo wa chama hicho ni kuwa na taifa la watu wanaoshiba kikiongoza Serikali.

“Ndugu zangu kwa kutumia rasilimali za nchi hii, tunakwenda kuboresha kilimo tutoe lishe bora kwa Watanzania kupitia sera ya ubwabwa kwa wote inayolenga kuondoa njaa nchini,” amesema, alipohutubia wakazi wa Magubike, Kilosa mkoani Morogoro leo Jumatano Agosti 20, 2025.

“Ndoto ya Mwenyekiti wetu, Wakili msomi Hashim Rungwe ni kuwapatia Watanzania lishe bora ili kuondoa njaa na magonjwa ya lishe duni, Ndugu zangu hilo tunakwenda kulimaliza,” ameongeza.

Mtiania mwenza wa Mtiania urais wa Tanzania wa Chaumma, Devotha Minja akizungumza na wananchi wa kata ya Magua alipokuwa njiani kuelekea Dodoma katika ziara hiyo ya kusaka wadhamini 200 katika mikoa 10 ya Tanzania  kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi nchini.



Chama cha Ukombozi wa Umma kimekuwa maarufu baada ya aliyegombea urais wa Tanzania kwa chama hicho uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Hashim Rungwe kuibuka na kaulimbiu ya ubwabwa kwa wote iliyompa jina maarufu la utani, Mzee wa Ubwabwa.

Sera hiyo, ameiendeleza mtiania wa kiti hicho mwaka huu, Salum Mwalimu ambaye pia ni katibu mkuu wa chama hicho, akiahidi kutimiza ndoto hiyo ya Mwenyekiti wake.

“Tutaanzisha maghala ya kuhifadhi chakula kila wilaya na kuuza chakula kwa hati punguzo ili kila Mtanzania aweze kupata chakula bora,” amesema Devotha na kuongeza;

“Tutahakikisha bei ya chakula inapungua, mchele uuzwe Sh500 kwa kilo kila mtu apige ubwabwa,” amesisitiza.

Amesema, mpango wa ubwabwa kwa wote ni mkakati maalumu utakaowezesha shule zote kuwa na huduma ya chakula bure na katika hospitali zote nchini ambapo kila mgonjwa atapatiwa milo mitatu kama sehemu ya matibabu katika huduma za afya.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Taarifa kwa Umma wa chama hicho, John Mrema ametoa wito kwa wanasiasa kuacha siasa za chuki na visasi ili kuwapa wananchi fursa ya kuamua sera na chama wanachokitaka.

Ziara ya Mwalimu itaendelea kesho mkoani Dodoma kwa ajili ya kupata wadhamini kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ili aweze kuteuliwa kuwania nafasi hiyo, ikiwa imebaki wiki moja tu kabla ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kufanya uteuzi wa watiania watakaokuwa wamekidhi vigezo, Agosti 27, 2025.