KUFUATIA Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kufuzu kwa mara ya kwanza hatua ya robo fainali ya michuano ya CHAN 2024, mjadala umeibuka kuhusu kikosi hicho kinakwenda kuikabili vipi Morocco ili kutinga nusu fainali.
Mjadala uliofanyika leo Agosti 20, 2025 kwenye Mwananchi X Space wenye mada isemayo; ‘CHAN 2024 ipo robo fainali, nini kifanyike Taifa Stars kutoboa kwenda nusu fainali?’, wadau mbalimbali wa michezo wakiwemo wachezaji wa zamani na makocha wametoa maoni yao huku wakiipa timu hiyo nondo saba za kuigaragaza Morocco.
Mbali na nondo hizo, wadau hao wamepongeza mafanikio hayo, lakini pia wametoa ushauri kwa benchi la ufundi na wachezaji kitu cha kufanya ili kuiondosha Morocco, bila ya kusahau kuwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani kuisapoti Taifa Stars.
Nondo hizo saba zilizotolewa na wadau hao ni wachezaji kuwa na utulivu, kujitoa, kujiandaa kisaikolojia, kumsoma mapema mpinzani, kuongeza umakini, kutoruhusu bao la mapema na mwisho kutokata tamaa hadi dakika ya mwisho ikitokea timu ipo nyuma kwa matokeo.
Tanzania ni mwenyeji wa fainali hizo zilizoanza Agosti 2 na kutarajiwa kufikia tamati Agosti 30 mwaka huu kwa kushirikiana na Kenya na Uganda ambazo zote zimefuzu robo fainali kwa kuongoza makundi yao.
Katika hatua ya robo fainali, Tanzania itaikabili Morocco, mechi ikipangwa kuchezwa Ijumaa hii Agosti 22, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 2:00 usiku.
Mwandishi mwandamizi wa habari za michezo wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Charles Abel amesema Taifa Stars haihitaji kupewa presha kubwa wakati ikijiandaa kuikabili Morocco.
“Hakuna haja ya kuwapa presha kubwa wachezaji kwa sababu inaweza kuwatoa mchezoni na kushindwa kufanya makubwa kama ambavyo tunatarajia, hii ni mechi ambayo timu moja ni lazima isonge mbele kwa kwenda nusu fainali,” amesema Abel.
Aidha, Abel amesema kitendo cha timu wenyeji wa michuano hiyo kwa maana ya Tanzania, Kenya na Uganda kuongoza makundi yao, ni ishara tosha ya kuonyesha ushindani mkubwa, hivyo kwake hana deni kuona wakiendelea kusonga hatua inayofuata.
“Kuongoza makundi yao maana yake wanajua kupambana, sitoshangaa kuona wakizidi kufika mbali zaidi na kutangaza ukanda huu wa Afrika Mashariki, kikubwa ni kuendelea kuwapa sapoti hususani wachezaji wetu wa timu ya Tanzania,” amesema.
Mbali na utulivu, mdau wa michezo hapa nchini, Richard Alphonce, amewataka wachezaji wa Taifa Stars kujitoa kwa asilimia zote pamoja na benchi la ufundi ili kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo.
“Mchango wangu utajikita kwa wachezaji, mchezaji ndiye anayecheza uwanjani kitu ambacho kinatakiwa kufanyika, wachezaji wanatakiwa kutambua kuwa wao ndio wanaenda uwanjani na sisi kazi yetu itakuwa kuwapa tu moyo, lazima wachezaji wawe na morali ya kujituma wakishajua tunachohitaji ni kitu fulani naamini watatia nia na kupambana uwanjani,” amesema na kuongeza.
“Wachezaji wa Taifa Stars wanatakiwa kutambua kama taifa tunahitaji hilo kombe kwa hiyo sisi tutawasifia, sasa je hizo sifa utasifia mtu asiyejituma, tunachoomba ni kwamba sisi tunahitaji hilo kombe tunataka kocha asiingie na checheto kwa kutugeuzia kikosi kwa kupanga anavyotaka. Tunataka kikosi kiwe kitu kimoja.
“Suala la mashabiki kujaa uwanjani ni kitu kingine kwa sababu tumeona kuna mashabiki wanajaa na bado timu zinafungwa.”
MBINU ZA KUIFUNGA MOROCCO
Aliyekuwa Kocha wa Tanzania Prisons, Aman Josiah, amepongeza mafanikio ya Taifa Stars kufika hatua ya robo fainali ya CHAN 2024 na kuwataka wachezaji pamoja na benchi la ufundi kujiandaa kisaikolojia kuelekea mchezo mgumu dhidi ya Morocco.
Josiah amesema hatua ya robo fainali, nusu fainali na fainali ni ngumu sana, hivyo kinachohitajika kwa sasa ni kuandaa kikosi katika hali bora ili kisibanwe na presha kubwa.
“Jambo kubwa kwanza ni kupongeza kwa hatua tuliyofika. Pili ni kupongeza benchi la ufundi, TFF, Serikali, wadau na mashabiki kwa sapoti yao. Morocco ni timu kubwa, kinachohitajika ni kuandaa wachezaji kisaikolojia. Lazima tuwape hamasa ili waingie uwanjani bila presha, wakacheze kwa ubora wao,” amesema Josiah.
Amefafanua kuwa, kiufundi Taifa Stars inapaswa kuamua kama itacheza kwa ubora wake binafsi au itajaribu kuiga mfumo wa Morocco. Amesema Morocco ni timu yenye uwezo mkubwa wa kushambulia kwa kasi na kutumia nafasi chache, hivyo Stars inapaswa kuingia na mpango thabiti.
“Ukiangalia Kenya walivyocheza dhidi ya Morocco, walifanikiwa kwa sababu hawakupishana nao. Walikaa nyuma, walipopata bao walilinda. Sasa sijui mwalimu wetu ataamua kuingiaje, je, tutacheza kwa ubora wetu au kukaa nyuma? Jambo muhimu ni kujijenga kama timu ya nyumbani kwa sababu ni mechi moja tu, tunapaswa kuwa imara,” amesema.
Josiah aliongeza kuwa Taifa Stars ina faida ya kuwa na wachezaji wakomavu ambao tayari wamecheza mechi kubwa za kimataifa, hususan wale waliocheza hatua za juu za Kombe la Shirikisho Afrika.
Naye nyota wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mussa Hassan Mgosi, amesema anaamini kikosi hicho kinaweza kubeba Kombe la CHAN ikiwa kitachanga vyema karata zake.
“Kwanza nalipongeza benchi la ufundi kwa jitihada kubwa walizofanya hadi kufika hapa tulipo leo, kikubwa tumeonyesha tuna nia ya dhati ya kufika mbali zaidi, naamini tumewasoma vizuri wapinzani wetu na tutatumia umuhimu wa kucheza nyumbani,” amesema.
Mgosi aliyewahi kuichezea Simba huku akifundisha pia Simba Queens, amesema endapo wachezaji kwa umoja na jitihada zao watajitoa kwa asilimia 100, anaamini wanaweza kufanya vizuri na kuandika rekodi mpya ya kipekee.
Nyota huyo wa zamani anakumbukwa kwa kuweka rekodi ya kuwa Mtanzania pekee kujumuishwa kwenye kikosi bora cha mashindano ya CHAN yaliyofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2009 nchini Ivory Coast ambapo Tanzania ilikuwa miongoni mwa timu nane zilizoshiriki.
Pia Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’, amesema nyota wa timu ya Taifa Stars, wanahitaji kuandaliwa vizuri kisaikolojia wakati wanapojiandaa kuikabili Morocco.
“Kwa hatua waliyofikia wanahitaji kuandaliwa kisaikolojia kwa sababu ni hatua ngumu na muhimu pia kwetu kama waandaaji wa michuano hii, bila kusahau tunatakiwa sisi wengine mashabiki tuonyeshe thamani yetu kwa kuipambania timu,” amesema Zaka.
Aidha Zaka amesema wachezaji wengi wa Morocco wako vizuri katika mipira ya kutenga ‘Set Pieces’, hivyo nyota wa Stars wanahitaji kuongeza umakini mkubwa na kuepuka makosa ya mara kwa mara ambayo yanaweza kutugharimu na kututoa mchezoni.
“Nilimsikia Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe akisisitiza wachezaji wetu wanapaswa kukaba sana, ni kweli tunahitaji hilo lakini kama nilivyosema hapo awali wenzetu wa Afrika ya Kaskazini ni wajanja na wanajua kucheza mechi za aina hii,” amesema Zaka.
STARS WAZOEFU KULIKO MOROCCO
Zaka ameendelea kwa kusema, wachezaji wengi wa Taifa Stars wana uzoefu mkubwa tofauti na wapinzani wao Morocco ambao mara nyingi wamekuwa wakitegemea zaidi nyota wa nje ya nchi hiyo, hivyo kupitia michuano hii inayohusisha wachezaji wa ligi za ndani ya nchi zao pekee, anaona kutakuwa na nafasi kubwa kwa Stars kufanya vizuri.
“Ukiangalia kwa viwango vya ubora utaona Morocco iko juu zaidi yetu, lakini wenzetu wanabebwa sana na wachezaji wao wanaocheza nje ya nchi yao, hivyo naamini kwa hatua hii tuna uzoefu mkubwa wa kupambana nao ipasavyo,” amesema Zaka.
Aidha Zaka amesema hata Morocco iliyocheza na Tanzania katika michuano ya AFCON na ile ya kufuzu Kombe la Dunia, timu ilicheza vizuri, isipokuwa jambo lililoiangusha ni kadi nyekundu ya Novatus Dismas Miroshi.
Mdau wa michezo kutoka Kenya, Paul Mzioki, amesema katika hatua ya robo fainali ya michuano ya CHAN 2024, anaamini timu ya taifa ya Kenya haina kibarua kigumu mbele ya Madagascar, lakini amewataka wachezaji kutowadharau wapinzani wao kwa kuwa na rekodi nzuri kwenye michuano hiyo ikiwemo kutwaa medali hapo nyuma.
Akizungumzia nafasi za Tanzania na Uganda, Mzioki amesema changamoto kubwa ipo kwa majirani hao, kwa kuwa wapinzani wa Tanzania ambao ni Morocco, wamepewa nafasi kubwa na wachambuzi wengi.
Hata hivyo, Mzioki anaona Timu ya Taifa ya Tanzania maarufu Taifa Stars ina uwezo wa kufanya vizuri endapo itajipanga kimbinu.
“Kuna kitu ambacho mdau mmoja ameongea hapa kuwa watu wanaongea kuhusu ubora wa Morocco bila ya kuitazama Tanzania. Kimbinu naona Tanzania inaweza kufanya vizuri, kikubwa kocha wa Stars anatakiwa kutoruhusu bao la mapema na kuwa bora katika kujilinda,” amesema.
MAMLAKA ZIWALINDE MASHABIKI
Katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah, amesema licha ya jitihada ambazo wachezaji wanapaswa kuzifanya ndani ya uwanja, pia mamlaka husika ni lazima izingatie usalama wa mashabiki wote kwa wale ambao watajitokeza kwa wingi kwa ajili ya kutoa hamasa kwa kikosi hicho katika mechi hiyo.
“Mechi na Morocco ni kubwa na ina umuhimu wake mkubwa, ni lazima mamlaka ihakikishe usalama wa mashabiki kwa maana ya kuhakikisha anakuja uwanjani salama na anaondoka pia salama, hiyo itasaidia kutoa motisha huko mbeleni,” amesema Osiah.
Osiah ameungwa mkono na Zaka aliposema: “Unapohamasisha watu waje uwanjani kwa wingi maana yake ni lazima uhakikishe usalama unakuwa mkubwa, bado ule ukarimu ni mdogo sana na mazingira kuanzia unatoka nyumbani hadi kufika uwanjani, hivyo tunapaswa kuzingatia hilo.”
Wakati mashabiki wakitakiwa kulindwa, mchezaji wa zamani wa Taifa Stars na Yanga, Ally Mayay Tembele, amesema hamasa ya mashabiki hao ndiyo nguzo kubwa itakayoweza kuwapa nguvu wachezaji wa Taifa Stars kuelekea mchezo dhidi ya Morocco.
“Kwanza kikubwa kwenye kuhamasisha mashabiki waingie uwanjani, ile kauli ya kuwa shabiki ni mchezaji wa 12 huwa na hamasa kubwa kwa wachezaji. Kitu cha msingi mashabiki wanatakiwa kuhamasika. Unaweza kutazama Kenya wakiwa pungufu dhidi ya Morocco, nguvu ya mashabiki ilitoa hamasa kwao na kufanya vizuri,” amesema Mayay na kuongeza.
“Katika mechi ya robo fainali kikubwa ni kupata matokeo chanya. Kingine kiufundi kwa makocha naamini Hemed Suleiman Morocco na Jamhuri Kihwelo watakuwa wameshafanya utafiti wa wapinzani kwa sababu kiukweli wenzetu wapo vizuri.
“Mwalimu anatakiwa kuangalia mbinu ambayo anataka kuingia nayo ili kuhakikisha tunapata matokeo chanya, na naamini hadi sasa kocha atakuwa ameshapata mbinu za kuitumia.”
Mdau wa michezo aliyetambulika kwa jina la Soka la Bongo, amesema Taifa Stars ina nafasi kubwa ya kuweka historia kwenye michuano ya CHAN 2024 kutokana na ubora wa benchi la ufundi na uimara wa ligi ya Tanzania.
“Kiufundi benchi la ufundi lina nafasi kubwa ya kutupeleka kule ambako tunahitaji. Hapa tunaenda kuonyesha ubora na uimara wa ligi yetu. Kwa sasa Ligi ya Tanzania ni miongoni mwa ligi bora za juu Afrika, hivyo tunaenda kupambana ili kuthibitisha ubora wetu. Sina shaka na makocha wetu kutokana na uzoefu mkubwa walionao,” amesema.
Aidha, amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuiunga mkono Stars akisema wao ni sehemu muhimu ya mchezo na wanaweza kuipa nguvu kufanikisha malengo yake.
Mdau wa michezo hapa nchini aliyejitambulisha kwa jina la Malcom, amesema ni jambo la kujivunia kuona timu zote za Afrika Mashariki zikifuzu hatua ya robo fainali ya CHAN 2024, lakini amesisitiza kuwa Tanzania inapaswa kuongeza juhudi na kucheza kwa kutokata tamaa kama ilivyokuwa kwa Uganda.
“Ukiangalia kwa ukanda wa Afrika Mashariki timu zote zimefuzu; Uganda, Kenya na Tanzania. Tukiangalia kwa nchi kama Uganda wametuzidi. Lazima tujiandae kwenda kwenye AFCON, ni vyema tukifanikiwa wote kwa pamoja, ni jambo zuri. Hivyo tupimane uwezo ili ukifika wakati huo tufanye vizuri. Napenda wachezaji wetu kuwa na ‘spirit’ kama Uganda, wacheze bila kukata tamaa,” amesema Malcom.
Wadau mbalimbali wa michezo wamechangia mada hiyo kuelekea michezo ya robo fainali ya michuano ya CHAN 2024 inayofanyika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda ambapo hatua hiyo itaanza Ijumaa hii Agosti 22, 2025 kwa Tanzania kuikaribisha Morocco kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, saa 2:00 usiku. Kabla ya mchezo huo, utatanguliwa na ule wa Kenya dhidi ya Madagascar, mechi ikichezwa jijini Nairobi kuanzia saa 11:00 jioni.
Jumamosi Agosti 23 mwaka huu, Uganda itakabiliana na Senegal jijini Kampala nchini Uganda saa 11:00 jioni, wakati Sudan ikicheza dhidi ya Algeria saa 2:00 usiku pale Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.