Winga wa KenGold apewa mmoja Namungo

ALIYEKUWA winga wa KenGold, Herbert Lukindo amekamilisha usajili kujiunga Namungo kwa mkataba wa mwaka mmoja, huku nyota huyo akiitosa ofa ya maafande wa JKT Tanzania, ambao mwanzoni ndio iliyokuwa ya kwanza kufungua mazungumzo naye.

Awali JKT Tanzania ilifungua mazungumzo na nyota huyo na kukubaliana mkataba wa miaka miwili, ingawa baada ya kuchelewa kuingiza fedha walizokubaliana, ndipo dili hilo likafungua milango kwa Namungo ambao waliingilia kati na kulikamilisha.

Akizungumza na Mwanaspoti, Lukindo alisema muda sahihi utakapofika mashabiki wake watajua ni timu gani atakayochezea kwa msimu ujao, japokuwa alikiri kwamba ni kweli ameachana na KenGold iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara kwenda Ligi ya Championship.

“Sio heshima kutangaza timu nitakayocheza bila ya wenyewe kuweka wazi, tusubiri hadi wahusika watakaponitangaza rasmi, japo nikiri ni kweli nimeondoka KenGold baada ya mkataba wangu wa mwaka mmoja niliousaini kumalizika,”alisema Lukindo.

Nyota huyo alisema ni bahati mbaya kwake kushuhudia kikosi cha KenGold kikishuka daraja, kwani licha ya malengo ya timu hiyo na wachezaji waliokuwa nao hakutegemea kilichotokea, ingawa anaangalia fursa nyingine za kukuza karia yake ya soka.

Lukindo aliyejiunga na KenGold Agosti 16, 2024, akitokea Biashara United iliyokuwa inashiriki Ligi ya Championship, kwa msimu wa 2024-2025 wa Ligi Kuu Bara, nyota huyo alifunga mabao manne tu kati ya 22 yaliyofungwa na kikosi hicho kizima.

Nyota huyo aliyechezea pia JKT Mgambo, Ndanda, Mbao, Mbeya City na Pamba anaungana na wachzeaji wengine wakiwemo Hussein Kazi (Simba), Cyprian Kipenye na Andrew Chamungu kutoka Songea United pamoja na Abdulaziz Shahame ‘Haaland’ aliyetoka TMA.

Wengine ni Lucas Kikoti aliyerejea tena akitokea Coastal Union na beki, Abdallah Denis ‘Viva’, Heritier Makambo (Tabora United), Abdallah Mfuko (Kagera Sugar), Jackson Shiga (Fountain Gate) na Ally Saleh Machupa ‘Machupa JR’ kutokea KVZ.