SAFARI ya Simba kukamilisha dili la usajili wa nyota wawili kutoka JKT Tanzania, kipa Yakoub Suleiman na beki wa kati Wilson Nangu halikuwa rahisi kutokana na masharti ambayo Wekundu hao walipewa ikiwamo kuchomoa wachezaji watatu katika kikosi walichonacho sasa.
Hakuna ubishi ni wazi kwamba Yakoub na Nangu ni mali ya Simba baada ya mazungumzo ya kina yaliyoambatana na masharti, lakini dili hilo limewang’oa kiungo Awesu Awesu, beki David Kameta ‘Duchu’ na mshambuliaji Valentino Mashaka ambao watapisha na wachezaji hao wawili.
Ugumu wa Simba kuwasajili wachezaji hao ulitokana na mikataba kuwa mirefu, ambapo wa Nangu ulikuwa unaishia 2028 wakati wa Yakoub ungeishia 2027, hivyo ikalazimika kukubaliana na masharti hayo kutokana na uhitaji wa huduma zao.
Chanzo cha ndani kimeliambia Mwanaspoti namna Simba ilivyolazimika kuwatoa kina Awesu kwa mkopo kwenda JKT Tanzania pamoja na kiasi cha pesa ndipo ilipokubaliwa kupata saini za nyota hao wanaosubiri kumaliza jukumu la timu ya taifa ‘Taifa Stars’ inayoshiriki fainali za CHAN 2024 ili kwenda kuungana na wenzao.
“Isingekuwa majukumu ya Stars kucheza CHAN wangekuwa wameondoka, maana wote wawili wapo katika jukumu hilo na wanapata nafasi ya kucheza, hivyo inasaidia miili yao kukaa fiti,” kilisema chanzo hicho kilichodokeza kuwa kina Awesu waliopo kambini Misri wameshajulishwa kujiandaa kuitumikia JKT msimu ujao unaoanza Septemba 2025.
“Simba imemsajili Yakoub kwa mkataba wa miaka mitatu ili kuziba pengo la Ally Salim anayetafutiwa timu kwenda kucheza kwa mkopo ama kumuuza, Nangu kuongeza nguvu ya ulinzi na kiwango cha msimu uliopita alimaliza na mabao mawili na asisti mbili kilimshawishi kocha Fadlu Davis kuhitaji huduma yake,” kilisema chanzo hicho.
“Wachezaji hao wanaweza wakawapishana angani wakati Nangu na Yakoub ambaye alimaliza na ‘clean sheets’ nane wanakwenda Misri, huku Awesu, Duchu na Mashaka wanajiandaa kurejea Tanzania kujiunga na JKT Tanzania. Ndio maisha ya soka kikubwa ni kupambana.”
Kabla ya Simba kufanikisha saini ya Yakoub, Yanga ndiyo ilifungua dimba la kuhitaji huduma yake ikitoa dau la Sh100 milioni kwa mkataba wa miaka mitatu, lakini halikuwa na maslahi kwa mchezaji kwani angeambulia Sh50 milioni na iliyobaki ingechukua JKU waajiri wake.