Mhesa kurejesha majeshi Mtibwa | Mwanaspoti

KIUNGO mshambuliaji, Ismail Aidan Mhesa, yupo mbioni kurejea tena ndani ya kikosi cha Mtibwa Sugar, baada ya mkataba wa miezi sita na Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship kuisha, huku kukiwa hakuna mazungumzo ya kuongeza mwingine.

Nyota huyo alijiunga na Geita Gold katika dirisha dogo la Januari 9, 2024, akitokea Mashujaa aliyoitumikia kwa miezi sita tu akitoka Mtibwa Sugar, ambapo kwa sasa ameanza mazungumzo ya kurejea tena ndani ya kikosi hicho alichokitumikia.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru alisema wanaendelea na maandalizi kwa ajili ya msimu ujao na tayari wapo wachezaji wanaofanya nao mazungumzo, hivyo muda utakapofika watawaweka wazi.

“Ukimya wetu una kishindo ndani yake na wale wanaoona mambo yetu hayaendi watambue tunafanya kazi kwa weledi mkubwa kwa lengo la kuhakikisha tunasajili wachezaji bora na wazoefu watakaotupigania kwa msimu ujao wa Ligi Kuu,” alisema Kifaru.

Kifaru alisema hawezi kusema ni mchezaji gani wamemsajili kwa sasa, ingawa ni kweli wapo ambao wamefikia makubaliano, hivyo wameandaa mikakati mizuri ya kuhakikisha watawatangaza wote muda muafaka utakapofika.

Licha ya kauli ya Kifaru, Mwanaspoti linatambua Mhesa amerejea akiungana na kiungo Ezekia Mwashilindi aliyetoka Tanzania Prisons na mshambuliaji Kassim Shaibu ‘Mayele’ kutoka TMA. Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu uliopita, imerejea Ligi Kuu ikiwa bingwa wa Ligi ya Championship baada ya kumaliza kinara na pointi 71 katika msimamo.