Dante mbioni kutua Kagera Sugar

BAADA ya aliyekuwa beki wa kati Andrew Vincent ‘Dante’ kuachana na KMC kutokana na mkataba kumalizika, kwa sasa yupo katika mazungumzo ya mwisho ya kujiunga na Kagera Sugar.

Dante aliyeitumikia KMC kwa miaka mitano, huku akizichezea pia Yanga na Mtibwa Sugar kwa nyakati mbalimbali, anafanya mazungumzo hayo ya kujiunga na Kagera Sugar ambayo kwa msimu wa 2025-2026, kikosi hicho kitacheza Ligi ya Championship.

Kagera Sugar iliyoshuka daraja baada ya miaka 20 ikishiriki Ligi Kuu Bara, msimu wa 2024-2025, ilimaliza nafasi ya 15 na pointi 23, kufuatia kushinda mechi tano, sare nane na kupoteza 17, ikiungana na KenGold iliyomaliza ya 16 na pointi 16.

Chanzo kutoka ndani ya uongozi wa Kagera, kililiambia Mwanaspoti Dante ni miongoni mwa mabeki wanaofanya mazungumzo na kikosi hicho, ambapo mchezaji mwenyewe ameonyesha nia ya kuichezea pia kutokana na kiasi kikubwa cha fedha alichowekewa.

“Licha ya ushiriki wetu wa Championship kwa msimu wa 2025-2026, ila tunahitaji kuwekeza sana kuwapata wachezaji wazoefu wataotimiza malengo ya kuturudisha Ligi Kuu Bara, tumeanza na Dante na tunaendelea na wengine,” kilisema chanzo hicho.

Kilisema wapo wachezaji wengine ambao baada ya timu kushuka waliamua kutokuwa tayari kuendelea nayo, hivyo kwa sasa inapambana na wale waliobakisha mikataba, japo sio wote watakaobaki kwa sababu itafanya pia biashara.