Namba zaibeba Stars, hesabu za robo zikianza

KATIKA msimu huu wa mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN 2024), takwimu zimeonyesha kuwa timu ya taifa la Tanzania ‘Taifa Stars’ ndio timu iliyofanya vizuri zaidi katika hatua ya makundi ambayo ilitamatika juzi, Jumanne kwa mechi mbili za kundi D.

Katika mechi hizo, zilishuhudiwa Sudan na Senegal zikiungana na wenyeji, Tanzania, Uganda na Kenya pamoja na Morocco, Algeria na Madagascar kutinga hatua ya robo fainali ambayo itaanza kuchezwa kesho (Ijumaa) kwa wababe wawili kutoka Afrika Mashariki kutupa karata zao.

Takwimu zinaonyesha kuwa Taifa Stars iliyokuwa kundi B imeibwaga Kenya maarufu kama Harambee Stars kutoka kundi A kama timu bora zaidi katika hatua hiyo, licha ya wote kuongoza hatua ya makundi wakiwa na pointi sawa 10, hizo ni idadi kubwa zaidi ya pointi kufikiwa mwaka huu.

Timu hizo za Afrika Mashariki zinatofautishwa wa mabao ya kufunga na kufungwa katika hatua hiyo Stars imefunga mabao matano na kuruhusu moja (4+), Harambee Stars yenyewe imefunga manne na kuruhusu moja (3+).

Na kama haitoshi, Stars imeweka rekodi kwa kuwa timu ya kwanza kutinga robo fainali huku ikiwa na mechi moja mkononi huku Harambee Stars ilibidi kusubiri hadi mechi ya mwisho ambapo iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Zambia.

Kigezo kingine ambacho kinaibeba Stars mbele ya Kenya katika hatua hiyo ni nidhamu. Stars imemaliza hatua ya makundi ikiwa haina kadi nyekundu, lakini Harambee Stars ilionyeshwa kadi nyekundu moja kwa moja katika mechi mbili mfululizo dhidi ya Angola (Marvin Nabwire dakika ya 21) na Morocco (Chris Erambo dakika ya 45+4).

Mbali na Stars na Kenya, timu nyingine zilizomaliza hatua ya makundi na idadi kubwa ya pointi ni Morocco iliyoshika nafasi ya pili kundi A ikiwa na pointi tisa, imefunga mabao manane na kuruhusu matatu (5+).

Pamoja na hilo hayo ni mambo mengine yaliyotokea katika hatua ya makundi ya michuano hiyo ambayo kwa mara ya kwanza yanafanyika Afrika Mashariki na wenyeji wote watatu, Kenya, Tanzania na Uganda wameweka historia kwa kutinga robo fainali haijawa kutokea kwenye mashindano ya CAF.

Ramandimbisoa Michel Toldo wa Madagascar ndiye mchezaji aliyechukua tuzo nyingi zaidi za mchezaji bora wa mechi katika hatua ya makundi ya michuano ya CHAN 2024, baada ya kushinda mara tatu huku akifuatiwa na kiungo wa Taifa Stars, Feisal Salum mara mbili.

Toldo aling’ara kwa mara ya kwanza katika mechi ya kwanza ya timu yake dhidi ya Mauritania iliyomalizika suluhu. Alirudia tena dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), ambapo aliiongoza timu yake kushinda kwa mabao 2-0. Mechi yake ya tatu bora zaidi ilikuwa dhidi ya Burkina Faso, akiisaidia Madagascar kuibuka na ushindi muhimu wa mabao 2-1.

Kwa jumla, Toldo ambaye ni kipa, ameshinda tuzo hizi tatu kati ya mechi nne za hatua ya makundi, jambo linaloonyesha ubora wa kiwango chake. Hatua hii inamweka kwenye ramani ya wachezaji bora zaidi wa michuano na kumfanya kuwa nembo ya mafanikio ya Madagascar. 

Mbali na Toldo, wapo wachezaji wengine waliobeba tuzo zaidi ya mara moja, akiwemo Feisal Salum Abdallah wa Taifa Stars, aliyeibuka mchezaji bora wa mechi mara mbili dhidi ya Burkina Faso na Afrika ya Kati (CAR).

Pia, Abdelrazig Taha Yagoub Omer wa Sudan na Alhassane Bangoura wa Guinea kila mmoja alipata tuzo mara mbili.

Jumla ya mabao 74 yamefungwa katika mechi 36, sawa na wastani wa mabao 2.18 kwa kila mechi. Takwimu hizi zinaonesha kiwango cha ushindani kilichopo ambapo kila timu inapambana kuhakikisha inapata matokeo chanya katika kila hatua.

Ni wachezaji watatu tu ambao wamefikisha mabao matatu katika hatua ya makundi ambao ni Oussama Lamlioui wa Morocco, Thabiso Kutumela wa Afrika Kusini na Allan Okello wa Uganda.

Nyota hawa wamekuwa nguzo muhimu kwa timu zao, wakionesha ubora wa kiufundi na ubunifu mbele ya lango. Uwepo wao unatoa taswira ya namna michuano hii imekuwa chachu ya kupandisha vipaji vya wachezaji wa ndani barani Afrika.

Kundi la wafungaji wenye mabao mawili pia limekuwa na mvuto, likiongozwa na Mtanzania, Clemen Mzize wa Taifa Stars, Austin Odhiambo na Ryan Ogam wa Kenya, Mohamed Rabie Hrimat wa Morocco.

Pia wapo Lalaina Rafanomezantsoa wa Madagascar, Sofiane Bayazid wa Algeria, Kaporal wa Angola na Abdel Raouf wa Sudan.

Uwanja wa Mandela, Kampala, ndiyo uliotoa mabao mengi zaidi katika hatua ya makundi ya mashindano ya CHAN ambapo katika mechi tisa zilizofanyika, jumla ya mabao 22 yamefungwa.

Miongoni mwa mechi zilizozaa mabao mengi kwenye uwanja huo, ni pamoja na ile ya mwisho ya hatua ya makundi kati ya wenyeji, Uganda dhidi ya Afrika Kusini ambayo ilimalizika kwa sare ya mabao 3-3.

Katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, yamefungwa jumla ya mabao 18 huku Taifa Stars ikichangia kwa asilimia 27.8% kwa kufunga mabao matano katika mechi dhidi ya Burkina Faso 2–0, Mauritania (1-0) na Madagascar 2–1.

Uwanja wa Nyayo, Nairobi, imeshika nafasi ya tatu kwa mabao mengi, ikifunga jumla ya mabao 15. Morocco, DR Congo, na Angola ni miongoni mwa timu zilizochangia mabao mengi.

Uwanja wa Amaan, ulichangia jumla ya mabao 12. Mechi iliyozaa mabao mengi katika uwanja huo ni kati ya Sudan dhidi ya Nigeria, Sudan iliibuka na ushindi wa mabao 4–0, ikumbukwe kuwa Zanzibar pia ilichezwa mechi moja ya kuamua kundi B kati ya Burkina Faso dhidi ya Madagascar na kufungwa mabao matatu.Uwanja wa Moi, Nairobi, ulichangia mabao saba.

Katika jumla ya mabao 74 ambayo  yamefungwa katika dakika 90, kipindi cha pili kimeonakana kutoa mabao mengi zaidi.

Katika kipindi cha kwanza, dakika za kwanza hadi 15 ziliibua mabao tisa, zikionyesha wingi wa mashambulizi mapya mwanzoni mwa mechi. Dakika 16-30 zilichangia mabao 8, huku dakika 31-45 zikiibua mabao 12, kuonyesha jinsi timu zinavyoongeza presha ya mashambulizi kabla ya mapumziko.

Kipindi cha pili kimeonekana kuwa cha hatari zaidi. Dakika 46-60 zilichangia mabao 11, dakika 61-75 zikiwa na mabao 13, huku dakika 76-90 zikifunga mabao 21, kiwango cha juu kabisa katika hatua ya makundi.

Takwimu hizi zinaonyesha kuwa timu nyingi zinapata nafasi za kufunga na hata kumaliza mechi mwishoni mwa kipindi cha pili huku Jumla ya mabao 10 yamefungwa kwenye dakika za nyongeza, ambapo kipindi cha kwanza cha nyongeza kilichangia mabao manne  na kipindi cha pili mabao sita.

Algeria ndio timu pakee ambayo inauhakika wa kutembea ukanda wote wa Afrika Mashariki kuanzia hatua ya makundi hadi mechi yake ya robo fainali ambayo itacheza visiwani Zanzibar dhidi ya Sudan.

Wababe hao ambao walianza mashindano hayo huko Uganda walijikuta wakimalizia mechi yao ya mwisho ya hatua hiyo jijini Nairobi Kenya kwa kucheza dhidi ya Niger na sasa wanatakiwa Zanzibar kwa ajili ya mechi ya robo fainali kitu ambacho hakijatokea kwa timu nyingine.

Kocha wa taifa hilo, Madjid Bougherra amesema safari hizo kwa timu yake ni hazijawa changamoto, bali zimekuwa fursa kwa wachezaji wake.

Baada ya kupata sare tasa dhidi ya Niger katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi, matokeo yaliyowapeleka robo fainali, Bougherra alisema hali ya safari za kwenda Kenya, Uganda na sasa Zanzibar imekuwa chachu ya kuimarisha morali ya kikosi chake.

“Hakuna kilichobadilika kwa sababu ya safari. Kwa kweli ninafurahi kwamba mashindano haya yanafanyika katika nchi tatu. Angalau wachezaji wanapata nafasi ya kusafiri na kuona Kenya, Uganda na Tanzania. Ukiwa sehemu moja kwa muda mrefu unaweza kuzoea na hali ikawa ya kuchosha kwa wachezaji,” anasema Bougherra.

Katika mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Niger, kocha huyo alisema mvua ilinyesha na kufanya nyasi za Uwanja wa Nyayo kuwa nzito, lakini hakutaka kutumia hali ya hewa kama kisingizio.

Inawezekana kwamba ni wachache walikuwa wakiamini kuwa Sudan inaweza kuwa miongoni mwa mataifa manane ambayo yatatinga robo fainali ya michuano hii, moja kutokana na kile ambacho kinaendelea nchini kwao.

Sudan haijapoteza mechi hata moja katika hatua ya makundi na iliwashangaza wengi kufuatia kuifungashia virago Nigeria katika mashindano hayo kwa kuishushia kipigo kizito cha mabao 4-0.

Hata hivyo licha ya ushindi huo, ikawabana mbavu mabingwa watetezi kwenye mashindano hayo, Senegal na kumaliza kinara wa kundi D.