Dar es Salaam. Watu 79 wakiwemo watoto 19, wamefariki dunia baada ajali ya basi iliyotokea katika jimbo la Herat, kaskazini magharibi mwa Afghanistan.
Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo, Abdul Mateen Qani, imeeleza kwamba ajali hiyo imesababishwa na basi walililokuwa wakisafiria watu hao kugongana na lori na pikipiki wakati wakiwa njiani kurejea nchini Afghanistan.
Watu hao walikuwa wakitoka Afghanstan baada ya kufukuzwa katika maeneo waliyokuwa wamehifadhiwa nchini Iran.
“Ajali imetokea saa 8:30 usiku kwa saa za Mkoa wa Herat baada ya basi hilo kugongana na lori na pikipiki na kusababisha moto mkubwa ulioua watu wengi papo hapo,” amesema Qani.
Amesema jumla ya waliofariki kwenye ajali hiyo ni 79, wakiwemo watoto 19 huku watu wawili wakijeruhiwa.
Kwa upande wake, daktari mkuu wa hospitali ya kijeshi, Mohammad Janan Moqadas amesema miili mingi haijatambuliwa kwa sababu imeungua vibaya.

Ameongeza kuwa ajali hiyo imeleta athari zaidi kutokana kukwama kwa jitihada za uokoaji kwa sababu ya moto mkubwa uliowaka baada ya ajali na kusababisha ugumu kwa vikosi vya ukoaji.
“Majeruhi hawakuweza kuokolewa kutoka kwenye basi kwa sababu ya moto huo uliokuwa unawaka na hata baadhi ya waokoaji walikuwa wakiungua,” amesema Maqadas.
Wizara ya Mambo ya Ndani nchini humo imesema zaidi ya Waafghani milioni 1.5 wamerudi kutoka Iran na Pakistan mwaka huu pekee, kwa mujibu wa Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa.
Nchi zote mbili zimeongeza kasi ya kuwafukuza baada ya miongo kadhaa ya kuwahifadhi. Wengi wao hurejea wakiwa hawana kitu na hukabiliana na hali ngumu katika taifa linalopambana na umasikini na ukosefu wa ajira.
Ajali hii ni mwendelezo wa ajali zingine ikiwemo ile iliyotokea Desemba 2023, ajali mbili tofauti za mabasi zikihusisha malori ya mafuta na kuua watu 52 na baadaye Machi 2024, wengine 20 walifariki dunia katika ajali ya barabarani mkoani Helmand.