Wakulima 5,000 kunufaika na mradi wa kilimo rafiki Geita

Geita. Zaidi ya wakulima 5,000 kutoka katika kata tatu za Butundwe, Kagu na Nyawanzaja zilizopo Wilaya ya Geita mkoani Geita wanatarajia kunufaika na kilimo rafiki kitakachowasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuvuna mazao mengi zaidi.

Wakulima hao watajengewa uwezo wa namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kupatiwa mbegu bora zinazostahimili ukame, pamoja na kupewa elimu ya kilimo bora kupitia mashamba darasa ambayo ni hatua muhimu ya kuwasaidia wakulima kufanya vizuri.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kijani Consult, Mandolin Kahindi wakati wa ugawaji mbegu bora za mahindi kwa wakulima wa kijiji cha Nyakagomba, Kata ya Butundwe ambapo amesema kwa kuanzia, wakulima 200 wamepatiwa mbegu bora na mafunzo ya kilimo bora ambao nao watatoa elimu kwa wakulima wengine katika maeneo yao.


Amesema mradi wa kilimo rafiki unatekelezwa na taasisi ya Kijani Consult Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la DIB la nchini Denmark chini ya ufadhili wa CISU utawawezesha wakulima kujua mbinu bora za kilimo kuanzia maandalizi ya shamba, upandaji, utunzaji mimea hadi uvunaji.

Kahindi amesema kupitia mradi huo, wameanzisha mashamba darasa kwenye vijiji ambayo yatatumika kuwafundisha wakulima ili nao wakatekeleze kilimo bora kwenye maeneo yao.

“Changamoto kubwa inayowakabili wakulima ni mabadiliko ya tabianchi. Tumewaletea mbegu zinazohimili mabadiliko haya ambazo pia zinatoa mavuno mengi. Vilevile, tunapunguza gharama za uzalishaji kwa kuwapatia mbegu na kuwafundisha namna ya kuzalisha mbolea ya asili badala ya kutegemea mbolea za dukani ambazo ni ghali na pia zinaharibu afya ya udongo,” amesema Kahindi.

Baadhi ya wakulima wa kijiji cha Nyakagomba wamesema athari za mabadiliko ya tabianchi zimekuwa kikwazo kikubwa cha uzalishaji na kusababisha wakabiliane na lindi la umaskini na njaa kutokana na wao kuishi kwa kutegemea kilimo.

Zablon Ondego ambaye ni mkulima katika kijiji hicho, amesema kwa miaka ya hivi karibuni, mvua zimekuwa chache, hali iliyosababisha mazao mengi kunyauka mashambani na hata wanayofanikiwa kuvuna yanashambuliwa na wadudu.

“Mwaka jana tulipata hasara kubwa kwa sababu mbegu tulizopanda awali hazikuota. Tulilazimika kupanda mara ya pili, lakini hata tulipopata mahindi yalishambuliwa na wadudu, unamenya unakuta zaidi ya wadudu 20 wapo ndani, na hatujui namna ya kukabiliana nao,” amesema Ondego.


Mkulima mwingine, Shoma Mahundi amesema wakulima wanakabiliwa na changamoto ya pembejeo za kilimo kama mbegu na mbolea, hivyo kusababisha wapate mazao dhaifu kutokana na wao kushindwa kulima kilimo bora.

Amesema kupitia mradi wa kilimo rafiki, wamefundishwa namna ya kuandaa mashamba kwa kutegemea mbolea ya samadi na mboji inayotengeneza afya ya udongo badala ya kutegemea mbolea za viwandani ambazo ni za gharama lakini pia sio rafiki kwa udongo.

“Hizi mbolea za viwandani zinafanya kazi pale tu unapoitumia lakini baada ya hapo haifanyi kazi na udongo unakuwa umeharibika, rutuba yote imeisha ndio maana hawa wametufundisha namna bora ya kuufanya udongo uwe na afya,” amesema Mahundi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Nyakagomba kilichonufaika na mradi huo, amesema mafunzo ya kilimo bora yaliyotolewa kwa wakulima yatakuwa suluhisho la changamoto za muda mrefu zilizokuwa zikiwakabili wakulima.