CHAN 2024: CAF yazuia wapigaji Uganda

WAKATI timu ya taifa ya Uganda Cranes ikijiandaa kwa mechi ya nusu fainali ya CHAN 2024 dhidi ya Senegal, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limechukua hatua ya kupunguza idadi ya tiketi ambazo shabiki anaweza kununua mtandaoni.

Hadi sasa, kila shabiki ataruhusiwa kununua tiketi tatu tu, kutoka tano zilizokuwa zikiruhusiwa awali.

Taarifa hiyo imetolewa na Dennis Mugimba, msemaji wa Wizara ya elimu na michezo pamoja na kamati ya maandalizi ya CHAN Uganda.

Mugimba alisema hatua hii inalenga kuzuia ulaghai na biashara haramu ya tiketi, ambayo mara nyingi husababisha mashabiki kukosa nafasi au kulazimika kununua kwa bei za juu sokoni.

“Lengo letu ni kuzuia watu kununua tiketi kwa wingi kisha kuzisambaza kwa bei ya juu. Hakutakuwa na tiketi za karatasi; kila kitu kitafanyika mtandaoni kwa njia rasmi,” alisema Mugimba.

Aidha, Mugimba alionya tiketi zozote za karatasi zinazozunguka sokoni ni batili. Mfumo wa kielektroniki wa uuzaji tiketi kwenye Uwanja wa Taifa wa Mandela, Namboole, unaweza kugundua mara moja tiketi bandia au zile zinazojirudia.

Cranes itakabiliana na Senegal Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Namboole kuwania kutinga nusu fainali ya michuano hiyo.